Ni lazima kukua

5:46:00 PM Unknown 0 Comments

NI LAZIMA KUKUA.
Mwenyehekima mmoja amewahi kusema, ukuaji [wa mwili] ni jambo la asili; lakini maendeleo ni matokeo ya maamuzi ya mtu (Growth is natural but development has to be intentional). Hakuna mtu amewahi kuendelea kwa bahati mbaya [accidentally]; iwe ni kiroho, kiuchumi, kiuongozi n.k! Mpaka mtu ameamua [nuia] kuendelea katika eneo fulani, atabaki katika hali ile ile. Kanuni hii inafanya kazi kwa mtu mmoja mmoja, jamii hata taifa.
Nimewahi kusoma makala katika gazeti moja, ambapo mchambuzi alikuwa akieleza ni kwa namna gani bara la afrika linaweza kujifunza kutoka nchi ya China katika vita dhidi ya umasikini. Anasema mwaka 1966, China haikuwa na uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha watu wake lakini leo hii inauwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha watu wake na kuuza nje ya nchi. Kumbe, kila mtu au jamii au taifa, lazima kwanza linuie kuendelea [Develop] katika eneo mahususi [specific] vinginevyo maendeleo hayawezi kutokea. Jambo kubwa tunalotaka uelewe hapo ni kwamba, kila mtu anawajibika binafsi katika kuhakikisha anapiga hatua kubwa ili leo iwe bora kuliko jana, na kesho iwe bora kuliko leo.
“Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto” 1Kor 13: 11
Wataalamu wanasema, “kwa siku mwanadamu anafanya maamuzi karibu elfu kumi [10,000]” kwa mawazo ya haraka haraka unaweza ukaona kwamba chaguzi hizo {decisions} ni nyingi  kwa sababu tu tunapofanya maamuzi hayo hatufikiri sana. Si wengi wanaofikiri sana kwa nini hawakui, si wengi wanafikiri sana kwa nini ubora wao hauongezeki, si wengi wanaowaza kuhusu ubora wa afya zao. Kila kitu ni uchaguzi wako, hata wokovu ni matokeo ya uchaguzi na uamuzi wako. Aliandika Mt Agustino anaandika: “Mungu ambaye amekuumba bila kutaka, hawezi kukuokoa bila kutaka.”
Ili kukua ni lazima uchague maeneo ambayo unataka uone ukikua katika mwaka husika. Ukuaji lazima uzingatie muda, One day at a time! Maeneo yafuatayo ni muhimu kwa ukuaji wako:
  1. - Kitaaluma-Unaweza kusema mwaka huu lazima nisome shahada ya uzamili au ya uzamivu na ukatekeleza
  2. - Kiroho- Ni muhimu uwe na shauku ya kukua ili kufanana na Yesu. Yeye ni nuru hivyo ni lazima uwe nuru pia, yeye ni Mtakatifu na hivyo ni lazima uweke mkakati wa kuwa mtakatifu pia. 1 Yohana1:5-6
  3. - Kiuchumi- Mkakati wa kuongeza kipato na uwekezaji ni muhimu ufanyike kwa kuzingatia muda. Ni muhimu kuweka nia ya kuanzisha mradi au kuwekeza katika biashara ili kujiongezea kipato.
  4. - Sayansi na Teknohama- Ni lazima kila unachokifanya uchanganye na sayansi na teknolojia. Angalau ujue Microsoft Word, Power Point, Excel nakadhalika. Sayansi ya usindikaji ni muhimu ili kuongeza thamani ya bidhaa ghafi na mazao. Ukiipenda teknolojia utafanikiwa, mitandao ya kijamii pia ikitumika vizuri inaweza kukutangaza na kukupa fursa ya kipawa chako.
  5. - Kipaji chako- Kama unaimba basi ungalau jifunze pia kupiga hata chombo kimoja cha muziki, nenda chuo kinachokuza kipaji chako. Soma vitabu vinavyotoa mwongozo wa kipaji chako.
Mchakato wa ukuaji, unakutaka ukubali baadhi ya mambo, na ukatae baadhi ya mambo ili nguvu zako zielekee katika jambo moja. Ili kukua kwa haraka ni lazima ujifunze kuwa mtu wa jambo moja, bobea katika jambo moja, zamia kabisa katika fani yako. Hakikisha unakuwa na misuli katika kipaji chako hata watu wakutambue kama guru na kisha ujenge ufalme wa Mungu kwa kipaji hicho. Tukutana kileleni…..

0 comments :

Laiti kila mwenye dhambi angalitambua hili

9:44:00 PM Unknown 0 Comments

LAITI KILA MWENYE DHAMBI ANGELITAMBUA HILI!
[Wana ujumbe nusu na hivyo hauleti maana kamili]
Kila mwenye dhambi anajua fika kwamba yeye ni mwenye dhambi.  Kujua kwamba tuna dhambi haitoshi, lazima tujue kwamba, Mungu yuko tayari kutusamehe. Kujua kwamba, unadhambi kunaleta uchungu lakini kujua kwamba, Mungu yuko tayari kusamehe kunaleta amani ikiwa utalifanyia kazi wazo hilo. Kama kila mdhambi angelijua hilo angeliomba toba mapema.
Mungu hafanyi maandalizi ili ajiweke tayari kusamehe bali yuko tayari hata sasa kusamehe. Laiti kama kila mwenye dhambi angelijua hili, wengi wangetubu, shida yao wana ujumbe nusu, wanajua wazi ni wenye dhambi, bali hawajui  kama Mungu yuko tayari kusamehe.
Yohana 8:1-8 inaeleza, nyakati zile Mafarisayo walipomkamata [mfumania] yule mwanamke katika zinaa walimpeleka mbele za Yesu wakiwa na wazo la kumpiga kwa mawe mpaka kufa kama ilivyokuwa katika sheria ya Musa. Lakini Yesu aliposema, “asiye na dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe”, biblia inasema, wote waliokuwa pale kuanzia watoto wadogo mpaka wazee walishtakiwa mioyoni mwao, ikiwa na maana mioyoni mwao walishuhudiwa kwamba, wao pia ni wenye dhambi. Hakuna mwenye dhambi asiyejua kwamba yeye ni mwenye dhambi. {Yohana 8:7-8}
John Newton mtunzi wa wimbo maarufu duniani, ‘amazing grace’ anasema, “nijualo mimi ni hili, mimi ni mwenye dhambi mkuu, na Yesu Kristo ni Mwokozi mkuu”. Anajua yeye ni mwenye dhambi na anaifahamu na tiba pia.  Hakuna mwenye dhambi asiyejijua wala asiyeijua hukumu yake. Imeandikwa:  Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.” Waefeso 5:5
Paulo anasema, neno hilo tunalijua hakika, tunafanya tunachokijua, tunajua madhara yake na hasara zake tunazijua pia. Je, ni nani hajui kama Mungu anachukia wizi, udhalimu, uchafu na ubaya wote? Bila shaka sote tunajua.
Yesu aliposema asiye na dhambi na awe wa kwanza kumtupia mwanamke huyu jiwe, biblia inasema wote walisutwa nafsini mwao yaani, hakusalia hata mmoja asiyekuwa na dhambi wala ambaye hakujua kwamba anadhambi. Kumbe kila mwenye dhambi anajua anazo lakini hataki kuzipeleke kwa Yesu, maana hata hawa baada ya kushtakiwa mioyoni mwao hawakumwendea Yesu, badala yake waliondoka zao wakamwacha Yesu na yule mwanamke.
Ni muda muafaka sasa tumejua kwamba tunadhambi na tunachukua uamuzi wa busara wa kuzipeleka mbele za BWANA badala kukimbia au kuendelea kukaa nazo kama walivyofanya wayahudi hawa. Mungu yuko tayari kusamehe muda wote ungalipo hai, Mungu ni wa rehema na ni mwenye huruma nyingi; hatamdharau mtu mwenye dhambi atubuye, wala hawezi kumwacha aliyeumizwa katika ukosaji. Napenda kukualika leo mwendee kwa kusema maneno haya: “Ee BWANA uniwie radhi mimi mwenye dhambi, nimejua makosa yangu na nimejua wokovu wako. Unioshe kwa damu yako na unioneshe na wokovu wako leo. Amina”
Aksante kwa kuja na kushiriki katika msimu wa nne [4] wa weekend of purpose, makala zijazo tutakujuza  mafundisho yatokanayo na weekend of purpose kwa uchache.

0 comments :

Watu wake ni akina nani?

6:44:00 PM Unknown 0 Comments

 
WATU WAKE NI AKINA NANI?
Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Yohana 13:1

Unaposoma maandiko kwamba, Yesu aliwapenda watu wake swali unaloweza kujiuliza ni hili, watu wake ni akina nani hao? Ni kwa nini awapende kwa upendo wote. Neno aliwapenda upeo lina maana aliwapenda kwa upendo wote au kwa utimilifu wa upendo. Upendo huu Yesu alionesha wakati mauti yake imekaribia, alipata shida kuachana na wale aliowapenda na alitamani kuendelea kukaa  nao kwa kitambo kirefu. Ni kama mtu anapotoa wosia wa mwisho kwa watoto aliowapenda mno.

Katika tafakari yangu ninaamini walio wake ni hawa: 

  1. ~ Ni wale walioacha vyote wakamfuata [Mathayo 9:27].
  2. ~ Ni wale waliojikana na kuchukua msalaba [Marko 8:34-35].
  3. ~ Ni wale waliaminio jina lake [Yohana 1:12].
  4. ~ Ni wale waliokaa katika neno lake [Yohana 8:31-32].

Makundi hayo manne ni makundi ya watu ambao BWANA aliwapenda upeo wala hakupenda kuachana nao. Walikuwa watu waliochukua msalaba na kumfuata, walikuwa watu wenye kusikia neno lake na kulitenda.  Hawa ni watu walioacha mashamba, ndugu wa kike na kiume, ni ambao waliacha mambo mazuri wakaamua kumfuata BWANA.

Sharti la kuwa mwanafunzi wa Yesu si gumu wala huhitaji kuwa myahudi ili uwe mwanafunzi wake, unachohitaji kukifanya ni kukaa katika neno lake. Kulisoma kila siku na kulitenda. Ni vema kutenga muda ili kupata wasaa angalau nusu saa ya kusoma  neno na robo saa ya kutafakari.

Kama alivyowapenda waliomwamini nyakati zile, ndivyo anavyowapenda waamini wa leo, waliaminio Jina lake hata sasa. Anatupenda kwa upendo wote tena kwa upendo mtimilifu.

Mungu akubariki tukutane Boko Karmeli kwa masista kwa ajili ya programu ya Weekend of Purpose itakayofanyika Jumamosi na Jumapili, tarehe 15 na 16 mwezi wa kumi . Usikose

0 comments :

Tazama zaidi ya uonanyo

11:14:00 AM Unknown 0 Comments


TAZAMA ZAIDI YA UONAVYO

Watu wanapokutana na ukinzani/changamoto  katika jambo, mambo mawili huweza kutokea; kukosa nguvu na  ujasiri wa kuendelea mbele hadi kupata mpenyo,  au kukosa  uvumili na hivyo kutafuta njia mbadala hata kama si salama ili kufikia tamanio lake. Mtu wa namna hii huona changamoto kama mwisho au kikwazo cha kufikia mafanikio yake. Mfalme Sauli alipokutana na Goliath, yeye na Israeli yote isipokuwa Daudi walikosa nguvu na ujasiri wa kuendelea mbele [1Sam 17:11]; wakati Ibrahimu alipokutana na changamoto ya kupata mtoto, aliingia kwa mfanyakazi wake kama njia mbadala ili kufikia matamanio yake, na gharama yake ilikuwa kubwa. 

Robert H. Schuller, mwandishi wa kitabu cha “Tough times never last but tough people do”, anasema “Tofauti ya mtu anayeshinda na mtu anaishindwa katika changamoto [hiyo hiyo] wanayokutana nayo wote wawili au mazingira hayo hayo, ni namna ambavyo watu hao wamechagua kulitazama jambo hilo [Tafasiri ya mwandishi]”. Hivyo kumbe, namna ambavyo mtu anatazama au kuchagua kuona jambo au changamoto iliyopo mbele yake ndio huamua hatima ya mtu huyo katika jambo hilo; yaani kushinda au kushindwa kwake. [The ability to see beyond the situation is the key to overcome the challenge/crisis].

Musa alipokuta na vikwazo katika kuwakomboa wana wa Israeli kutoka katika utumwa wa Misri; hakuona kama tatizo la kumrudisha nyumba, bali aliona nafasi kwa yeye kuona Nguvu na Udhihirisho wa Mungu katika maisha yake na wana wa Israeli. Ndio maana kila alipokutana na tatizo au changamoto alikimbilia mbele za Mungu, kwa kuwa alijua ilikuwa ni fursa kwake ya kuona Ukuu wa Mungu; na kupitia ugumu wa Farao, Mungu atukuzwe na watu wote wapate kujua kuwa Mungu Anaishi.  Leo hii anajulikana kama mshindi [Kutoka 9:11, 29].

Wakati kila mtu anamuona Goliath kama tatizo katika Israeli, Daudi alimuona Goliath kama fursa ya kudhiirisha Ukuu na uweza wa Mungu; na ili dunia wapate kujua yuko Mungu katika Israeli. Lakini pia kwake, aliona kama fursa kwa yeye kuoa mtoto wa Mfalme bila kutoa mahari na mwanzo wa kuishi maisha bora, pia fursa kwa yeye pamoja na familia yake kuishi huru [1Sam 17:25, 46-47]. Leo hii anajulikana kama mshindi.

Mama Teresa wa Calcutta, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel alipoona maskini na watu wasio na msaada kule India; hakuona kama tatizo la kumkatisha tamaa, bali aliona fursa ya kumtumikia Mungu kwa kugusa maisha ya watu. Leo hii anajulikana kama mshindi.

Nimewahi kusikia habari za mama mmoja ambaye alikuwa amempa Yesu maisha yake; na alikuwa anafanyakazi katika kampuni fulani, lakini baada ya muda aliachishwa kazi; akaenda kwa mchungaji wake analia, mchugaji wake akamuuliza kwanini alikuwa analia!!!? Akamuuliza, “Je una kitu gani ambacho unaweza kufanya?” Yule mama akamjibu kuwa anaweza kutengeneza keki tu. Baada ya mazungumzo na mchungaji wake; akamuambia aende akatengeneze keki kisha apelekee pale alipoachishwa na kuwagawia wafanyakazi wenzie bure kama sehemu ya kuagana nao; mara ya kwanza hilo wazo halikuingia akilini mwa yule mama lakini akafanya kama alivyoambia na mchungaji wake. Alipomaliza, wakati anarudi nyumbani, watu mbalimbali pale ofisini wakamtafuta na kumuuliza kama anaweza kuwatengenezea keki kwa “oda” maalumu, kwa kuwa keki zake ni nzuri. Baada ya muda kidogo yule mama alikuwa na ofisi yake, akanunua mashine kubwa zaidi na kuajiri watu wengine katika ofisi yake.

Mara kadhaa tumesikia watu wakisema, “Tatizo sio tatizo bali tatizo ni namna ambavyo mtu analitazama tatizo”; ukitafakari usemi huu utagundua kuna ukweli ndani yake. Kumbe, hatua ya kwanza kwa mtu ili aweze kuvuka katika changamoto fulani, ni kuangalia namna ambavyo analitazama jambo hilo vinginevyo mtu anaweza kufanya kosa kama la Ibrahimu au kukubali kuwa dhaifu mbele ya changamoto kama mfalme Sauli na wana Israeli . Wiki ijayo tutangalia mambo kadhaa ya kumsaidia mtu aweze kuona zaidi ya anachoona ili kupata matokeo bora zaidi….

See you at the Top

0 comments :