Kata kiu yako
KATA KIU YAKO
(Hakuna mbadala wa Mungu)
Mwanzoni
nilizani ni gari, baadaye nilidhani ni kazi nzuri, mwishowe nilifikiri ni
katika kuoa na kuolewa; kumbe ni uweponi mwa Mungu pekee ndimo ulimo utoshelevu
wangu. Mtakatifu Agustino anasema, “Moyo wa mwanadamu hauta tulia mpaka
umekutana na muumba wake”. Ambao hawajaoa hudhani wakioa mioyo
yao itatulia, wasio na kazi hufikiri kazi inatoa kitulizo na wasio na pesa nao
hutamani kutulizwa kwa kupata pesa.
Nyakati
za Ibrahimu, Nuhu, na waamuzi hakukuwa na mabasi ya mwendo kasi,wala hapakuwa
na ipad na kompyuta. Lakini bado watu hawa walikuwa na utoshelevu na
amani ya ajabu. Je, amani hiyo waliipata wapi? Watu hawa hawakuwa na lift
kwenye majengo yao, wengine hawakuwa hata na nyumba bali waliishi hemani.
Lakini sasa licha ya kuwepo kwa mambo mengi mazuri bado wengi wana hali mbaya
kuliko zamani, ni wenye uhitaji usiokwisha. Hakuna utoshelevu katika vitu.
Paulo ananukuu fikra za Musa kwamba, hata upewe milki zote za Misri bado hautapata
utoshelevu. Wakati huo Misri ilikuwa ni tajiri mno na kitovu cha uchumi wa nchi
nyingi, pamoja na hayo Musa alijua hakuna utoshelevu ndani yake. [Ebr11:26]
Kuna
nyakati nimekuwa na rafiki mzuri anayenipenda sana kila kitu kinakuwa murua
kabisa [double double] lakini bado nafsi yangu ililia kwamba, inamtaka Mungu.
Hakika, moyo wangu hautatulia popote ila kwa BWANA naam, BWANA peke yake.
Hata
umpate mtu atakaye kupenda sana bado moyo wako hautatulia, nafsi yako italilia
uwepo wa Mungu. Ayala ambaye ni ndege wa jangwani [kusiko na maji na unyevu]
huvitamani sana vijito vya maji vivyo hivyo moyo wa mwanadamu hautanyamaza hata
ukipewa vilivyo vinono utaendelea kumhitaji Mungu. Kukosekana kwa Mungu
kutakuwa ni kama ukame ndani ya nafsi ya mtu.
Katika
kisima cha Yakobo Yesu alikutana na mwanamke Msamaria,aliyekuwa ameolewa na
wanaume wa tano na aliyekuwa naye ni wa sita. Lakini Je, alikuwa anatafuta nini
kwa waume hao wote sita? Jibu ni rahisi alikuwa anatafuta utoshelevu yaani,
alitaka kukata kiu yake. Yesu akamwambia maji haya unayochota hayakati
kiu. Pesa, sigara, wanaume, uasherati, hamu ya kuona picha chafu, wanawake,
urembo, utanashati, vyeo na mali za thamani kamwe havitaweza kukata kiu yako.
Mwanamke
Msamaria alisimama katika kisima cha Yakobo, lakini Yesu pia alisimama kama
kisima. Kwa hiyo kuna kisima cha Yakobo na Kisima kingine ni Yesu Kristo. Ndani
ya kisima cha Yakobo mlitoka maji yasiyo kata kiu, ndani ya Yesu Kristo mlitoka
maji yakatayo kiu. Na Yesu anamwalika kila mtu aje anywe maji hayo ya uzima na
asione kiu tena.
Baada
ya Yesu kuzungumza na yule mwanamke mwishowe alikubali na akataka apewa kile
kinacholeta utoshelevu kile kinachoondoa kiu yaani, Roho Mtakatifu ambaye ndiye
maji yaletayo utoshelevu na kuridhika. Natamani sote tumkimbilie Yesu na
kumsihi kwa maneno ya maombi kama alivyofanya mwanamke Msamaria: “Yule
mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa
kuteka. ”Yohana 4:15
Samaki
huwa katika ubora wake na ufanisi wa juu akiwa majini, mashine huwa katika ufanisi
wa juu inapokuwa mpya tena inapowekewa vilainishi [oil] kwa wakati. Vivyo
hivyo binadamu huonesha ufanisi wa hali ya juu awepo uweponi mwa Bwana ambamo
kuna ushirika wa ajabu na Roho Mtakatifu.
Tafuta
kukata kiu yako leo….tukutane chumba cha juu kama wale mia ishirini [120]
0 comments :