Anuani ya Muda
(P.O. BOX 701, MBEYA)
Yesu
aliposali alisema, “Baba yetu uliye mbinguni” hiyo ni anuani ambayo kila mmoja
wetu anapaswa kuitamani baada ya maisha haya. Ni muhimu mara baada ya kifo
tupatikane kwa anuani hiyo ya Mbinguni. Lakini kwa kuwa bado tuko duniani tunajulikana
kwa anuani za makampuni, anuani binafsi, shule na taasisi ambazo tunaishi na
kufanya kazi ndani yake. Na baadhi labda tuko vijiweni na pengine hatupatikani
kabisa [Unreachable].
Inawezekana
uko kwenye taasisi ambayo kwa namna moja au nyingine inakupa mateso,
Inawezekana uko katika mazingira ambayo kwa namna moja au nyingine hayakupi
furaha, jambo moja nataka ujue ni kwamba, uko hapo kwa kitambo tu. Kitambulisho
ulichopewa na taasisi yako, anuani unayojulikana kwayo sasa ni ya muda tu,
kamwe haita dumu milele. Zamani Nelson Mandela alipatikana kwa anuani ya
gereza, waliomtembelea walilazimika kwenda huko; Yusufu pia alipatikana
gerezani na mwishowe ikulu. Leo hii wote [Yusufu na Mandela] wanajulikana
katika hadithi za kutoka jela mpaka ikulu. From prison to palace story.
Maisha
ya shule au chuo yanaweza kuwa magumu hata mtu akakata tamaa na kuzimia moyo,
lakini maisha hayo ni ya kitambo kifupi tu, punde si punde utamaliza na maisha
mapya yataanza. Nakumbuka anuani ya, P.O BOX 701, Mbeya ilikuwa anuani
yangu ya shule ya Sekondari. Maisha ya shule pale hayakuwa mazuri, kidato cha
kwanza wengi walikuwa wanapigwa na kuonenewa bila sababu. Lakini nilijipa moyo
na nikamwomba Bwana anilinde ili nitoke salama katika taasisi ile. Niliomba
sawa sawa na imani yangu kwa wakati ule, na kweli nilitoka salama. Ilikuwa
anuani ya muda tu.
Sijui
kwa sasa wewe uko wapi na una amani kiasi gani, lakini ninachojua ni kwamba
unapita katika eneo hilo na hutokaa milele katika mateso hayo. Wakati mwingine
ni vema kuomba Mungu akupe uvumilivu na namna ya kuishi katika mazingira fulani
ili uishi vizuri katika kipindi cha mpito.
Inawezekana
Bosi wako ni mkali, inawezekana pia wafanyakazi wenzako hawakutendei vizuri,
jipe moyo kwa maana, wewe na wenzako hamta dumu katika taasisi hiyo milele. Cha
msingi ni hekima itumike ili muachane kwa usalama muda ukifika. Biblia
inasema katika mambo yote tujipatie sifa njema, kwa hiyo hata katika maeneo
yetu ya kazi, biashara na huduma ni lazima tujipatie sifa njema.
Na ili
tuishi na watu hatuhitaji watu wabadilike bali tunahitaji kubadilika.
Usimsubiri mkali awe mpole, bali wewe uwe mpole, usimsubiri mkorofi awe
mtaratibu bali wewe uwe mtaratibu. Kwa hiyo haijalishi uko katika taasisi yenye
changamoto namna gani lazima ujue uko hapo kwa muda tu, fanya vizuri na nuia
kuacha alama mahali hapo. Upo hapo kwa kitambo tu. Anuani yao si kitambulisho
chako cha milele.
Inawezekana
sasa unatumia sanduku la posta la kijiji chako lakini ni nani ajuaye kwamba,
mwishowe watu watumia anuani ya Ikulu kukupata? Inawezekana sasa
unajulikana kwa anuani ya kampuni ya mhindi lakini ni nani ajuaye kwamba,
mwisho wa siku utajulikana kwa anuani ya kampuni yako binafsi? Inawezekana
kabisa, pango mipango na kisha anza kuyaendea mafanikio yako.
Nataka
nikutie moyo mpendwa, uko hapo kwa muda tu, siku si nyingi utajulikana
kwa jina jema na kwa anuani bora zaidi. Uko hapo ili kujifunza, kama haupati
pesa za kutosha usijali, jitahidi upate uzoefu wa kutosha. Tunapofanya kazi
tunafanya kwa ajili ya mambo matatu, ama kwa ajili ya Mungu, ama kwa ajili ya
pesa, au kwa ajili ya uzoefu. Leo nasisitiza pata uzoefu wa kutosha na pesa
zitakuja baadaye, uzoefu unavuta pesa. Uzoefu wa kazi ni pamoja na kujua tabia
mbaya za wateja na wafanyakazi wenzako na namna ya kuzikabili changamoto za
kitabia.
Daudi
na Esta ni watu ambao kwa imani, na kwa ustadi wao walijikuta anuani zao
zinabadilika. Walipatikana katika nyumba ya Mfalme ilhali hawakuzaliwa kwa
mfalme. Na ndivyo ilivyo hadithi yako usipokata tamaa. Mungu anaweza kukutoa
jaani na akakuketisha na wakuu. Endelea mbele. Mpaka wiki ijayo, tukutane
katika nyumba ya mfalme, shalom!!!
0 comments :