Kwa Msaada wa Bwana Mungu Tumeweza

9:49:00 AM Unknown 1 Comments

KWA MSAADA WA BWANA MUNGU TUMEWEZA
(Aksante Bwana Yesu) 

Kuna nyakati ambazo unajikuta njia panda na mbele ya macho yako njia zote zinaonekana ni njema au ni sawasawa tu. Na hapo unamuhitaji rafiki atakaye kugusa begani na kukwambia, “tafadhali, tupite upande huu” bila shaka upande atakao uchagua rafiki huyo ni upande salama. Kuna nyakati ambazo unajiona una mabaya mengi na hapo unamhitaji rafiki atakayekwambia, unamazuri mengi pia.

Hayati Dkt William Arthur anasema: “Mungu amekupa zawadi ya sekunde 86,400 leo, Je,umetumia hata moja kumshukuru?”. Kwa zaidi ya wiki hamsini na mbili (52) takribani mwaka mmoja sasa, Mungu ametupa neema ya kukujia kila siku ya Ijumaa kwa njia ya makala zetu. Tumekujia kama marafiki tukikwambia, “tafadhali, tupite upande huu ambao ni salama”. Leo tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu. Kama si Yeye tusingeliweza kabisa kukufikia kwa mwaka Mzima. Utukufu na heshima vimrudie Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo na Yesu Kristo aliyetumwa. Amina

Siku moja nilikuwa katika tamasha moja la kusimumua. Na mahali pale watu walikuwa wakielezea mafanikio yao na kuwatia moyo wengine. Lakini kuna jambo moja lilikuwa likisumbua kichwa changu siku ile nalo ni hili, katika maelezo ya kufanikiwa kwao sikusikia wakimtaja Mungu. Na mimi nikajiuliza: Ni kweli Mungu hakuwasaidia hawa? Je, mitaa yao haipati mvua kutoka juu? Je! Si Mungu aliyewapa afya njema hawa? Si Mungu aliyewavusha hawa? I was like where is my God in their speeches?

Hatumtaji Mungu katika maelezo yetu kama utaratibu au mtindo fulani tu (formality.) La hasha! Tunamtaja kwa sababu Mungu anaishi na tumeona akitusaidia. Kwetu sisi Mungu ni halisi zaidi (japo kwa macho ya nyama hatumwoni) kuliko tuwaonao na tuyaonayo kwa macho ya nyama.  Yuko karibu nasi kuliko nguo tuvaazo.  Yeye ni Mungu ndani yetu. Kama tumefanya vema basi amefanya, maana yu ndani yetu.

Nilipoanza kazi kwa mara ya kwanza nikiwa na maarifa ya darasani tu bila ya kujua kilichopo kazini nilipata funzo kubwa. Mhasibu wa ofisi ile aliacha kazi na Mhasibu pekee niliyebakia ni mimi na nilihitajika kufunga hesabu na kupeleka kwa bodi. Mara nyingi hesabu zilinisumbua hazikuwa sawasawa kwa lugha ya kihasibu, ‘not balanced or not tallies’ Mara nyingi hali hiyo ilipotokea nilifanya jambo ambalo halifundishwi shuleni wala chuoni. Mara kadhaa ilipotokea nilikuwa nikiinama chini au nikifumba macho yangu na kuomba kwa BWANA. Nilimtaka Roho Mtakatifu anisaidie kama mfanyakazi mwenzangu (co-worker) ni ajabu aliniitikia na kunisaidia kujua chanzo cha tofauti ya hesabu zangu. Kwangu mimi Mungu ni halisi hata katika mambo ya Uhasibu. Bila shaka ndio maana Daudi akasema hivi: “Haleluya. Nampenda Bwana kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote.”Zab 116:1-2

Tunapomshukuru Mungu tunaibadili siku ya kawaida kuwa siku kuu. Tunamposhukuru Mungu leo hatufanyi mila ya wazungu, tunapomshukuru leo hatutimizi ratiba bali tumemwona, tunamtambua na tunampenda Mungu wetu. Hakika Yesu yupo ametusaidia nasi tunamshukuru. Ee Mungu wewe uko umetusaidia nasi Ee Bwana tunakushukuru. Waliokombolewa na Bwana na waliomwona BWANA katika makala hizi 53 waseme. Amina.

Kama namna ya kumshukuru Mungu pamoja nasi waunganishe rafiki zako angalau watano kwa kututumia anuani ya barua pepe zao (email) ili nao pia wafikiwe na neno la Mungu. Pia unaweza kujiunga (kusubscribe) kwa kupitia kwenye blog yetu kwa kuandika email yako na kutuma, utakuwa ukipokea article zetu kila ijumaa. Usisahau kuichagua page yetu ya facebook pia kama njia moja wapo ya kukufikia. Leo tunategemea kupokea  anuani tano za marafiki zako unaowapenda na ungependa wapate makala hizi. Tafadhali tutumie tunasubiri.  Mungu akupe kukaa salama.

1 comments :

Katika nchi hii, ni nani jasiri kama mimi?

11:52:00 AM Unknown 0 Comments

 
KATIKA NCHI HII NI NANI JASIRI KAMA MIMI?
(Neno Lake ndio ujasiri wetu)
Kichwa cha makala hii ni nukuu ya  maneno ya mwanasiasa aliyekuwa na haiba ya aina yake hapa Nchini Tanzania hayati Mchungaji Mtikila. Katika moja ya mazungumzo yake alihoji, “katika taifa hili ni nani mtu jasiri kama mimi?” Tunahitaji watu wenye ujasiri kama wa Mchungaji Mtikila lakini msingi wa ujasiri wao na uwe ni neno la Mungu. Tunahitaji watu wenye uhakika na maisha  yao (life is predictable) na msingi wao uwe ni ukweli wa neno la Mungu.
Wasiwasi ni yale mawazo yanayompata mtu anaposahau neno la Mungu. Kwa nini leo watu wengi wanahuzuni? Kwa nini leo watu wengi wamekata tamaa?  Kwa nini leo watu hawapati usingizi? Kwa nini leo wengi wanahofu na kesho yao? Ni kwa sababu wamesahau Yesu alivyosema.
Mwenye hekima mmoja anasema, hekima ni uwezo wa kulitumia neno la Mungu katika hali na maeneo tofauti tofauti. Tutalitumiaje neno ambalo tumelisahau? Tutalitumiaje neno ambalo hatulijui? Mpaka tumejua namna ya kulitumia neno la Mungu katika uchumi, katika kuachwa, katika dhiki, katika kushinda, katika kazi, katika masomo na biashara ndipo tunaweza kujiita wenye hekima.
Nyakati nyingine katika shida na mateso neno pekee ambalo Mungu aliwatumia watu wake ni kwamba, yuko pamoja nao. Ile tu kujua kwamba katika shida yako uko pamoja na BWANA inakutia nguvu. Siku moja nafsi yangu ilikuwa imeugua na nilikuwa najua sijatenda vema mbele za Bwana. Katika hali ya kukata tamaa ndipo nilipoona maono kwamba, Mungu yuko pamoja nami pamoja na mapangufu yangu, na nikajawa na furaha sana. Utajiri wa Mungu si tu wa fedha na Dhahabu bali ni pamoja na utajiri wa rehema, neema, msamaha, upendo na amani.  Wanaoujua utajiri wa Mungu wanajisamehe na kuwasamehe wengine haraka.
Je, Unamashaka kwa sababu umekaa kitambo kirefu bila mchumba? Je, bado haujapata kazi na unatafuta? Kumbuka alivyosema, Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. ” Mhubiri 3:1
Je, unaogopa itakuwaje? Kumbuka neno, Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai. ” Zaburi 27:13
Mitume wa Yesu walifika kaburini na kushangaa kuona BWANA hayumo kaburini waliogopa na kudhani mwili wake umeibwa. Na malaika wawili walijua mitume hawa wanamaradhi na tiba yake ni kuwakumbusha neno la Kristo mwenyewe na hapa Malaika akawaambia: “Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya” Luka 24:6
Wasingeliambiwa kumbukeni kama wangelikuwa wanakumbuka. Pamoja na Yesu kusema sana habari za ufufuko wake mitume walisahau. Ndio maana ni Muhimu kusoma neno la Mungu mara kwa mara, kusahau kupo!  Kukumbuka alichosema BWANA wetu Yesu ni ufunguo wa upatikanaji wa mahitaji yetu. Kumbukeni alivyosema, andikeni malengo yenu na maombi yafanyike, yapelekwe mbele zake BWANA. Usisahau kumpa utukufu MUNGU wetu  atakapo kujibu nina hakika atajibu tu.
Tukutane kileleni mahali wanapopatikana washindi.


0 comments :

Napendekeza usikope IV

10:44:00 AM Unknown 0 Comments

NAPENDEKEZA USIKOPE
(Makala ya Nne)  
Wiki hii ninamalizia kwa kutaja kanuni nyingine zenye uwezo wa kutupatia uhuru wa kifedha ikiwa tutaziangalia na kuzitenda. Waswahili wanasema “huwezi kuvuka mto kwa kuuangalia” kwa hiyo ili upate matokeo bora ni lazima uzifanyie kazi kanuni hizi. Lazima uzitende kwa bidii vinginevyo hauwezi kupata matokeo tarajiwa. Ili kutoka katika hali ya mikopo fanya yafuatayo:
  1. Weka akiba: Wawekezaji wengi wanasifa ya kutumia kidogo na kuweka akiba kubwa. Hatuwezi kuweka akiba kama tunatumia kila tulichokizalisha au tunakula kila tunacholipwa. Warren Buffet tajiri mkubwa duniani anatoa kanuni mbili za kukusaidia kukuza uchumi wako anaitaja ya kwanza ni, “usipoteze pesa na ya pili inasema, usisahau kanauni ya kwanza, usipoteze pesa.” Katika kila ngazi ya mshahara wako, haijalishi ni kubwa au ndogo hakikisha unaweka akiba. Pasipo akiba huwezi kuwekeza. Ukilipwa laki tano weka akiba, ukilipwa milioni tano weka akiba. Usipoweka akiba katika ngazi ndogo ya mshahara hautaweza hata utakapo kuwa na ngazi kubwa. Akiba ni uamuzi ambao msingi wake ni nidhamu. Mataifa yenye akiba kubwa (35%) ni yale yenye nidhamu katika pesa. Kama ambavyo benki hukata pesa yao ya mkopo moja kwa moja ndivyo ambavyo mtu anapaswa kujifunza kuweka akiba moja kwa moja. Serikali hukata kodi yake (PAYE) bila majadiliano, mtu hupokea mshahara ambao tayari umeshakatwa kiasi cha kodi ya serikali na hivyo mtu haoni maumivu kwa kuwa hajizipeleka kwa mkono wake katika taasisi ya kodi. Vivyo hivyo unapaswa kuhakikisha akiba yako haiguswi bali inaingia moja kwa moja katika akaunti yako ya akiba au ile ya malengo.
  2. Jilipe kwanza; Mshahara wako ni ile hela unayobaki nayo baada ya kutoa matumizi yako yote ya mwezi. Kama ukitoa matumizi yako yote ya mwezi hubakiwi na kitu basi ujue huna mshahara bali una posho. UKigundua huna mshahara anza kufikiri namna ya kupata mshahara. Hela unayopeleka dukani na shuleni kulipa ada ni mshahara kwa hao unaowapelekea na si yako. Hakikisha unajilipa kwanza na kama hamna hakikisha unaishi kwa namna ambavyo unapata kipato cha ziada. Pesa inayokwenda katika chakula, maji, ada na mavazi ni pesa ya kujikimu na hii haitoi jibu la uhuru wa kifedha. Uhuru wa kifedha unaletwa na pesa inakwenda kwenye miradi. Kama hautuweki akiba na kujipanga kuwekeza maana yake tunaishi ili kujikimu tu.
  3. Wekeza katika mali zisizo hamishika: Ukifanikiwa kuwa na akiba kubwa wekeza katika mali zisizo hamishika. Unaweza kumiliki mali isiyohamishika kama kiwanja kwa kuamuru (issue standing instruction) kampuni au taasisi inayohusika na utoaji viwanja kukata sehemu ndogo ya mshahara wako kila mwezi mpaka itakapotosha kununua kiwanja. Kwa mazingira ya sasa na mishahara ya kitanzania si rahisi kununua kiwanja kwa kulipia mara moja lakini kwa njia hii ninayopendekeza ni rahisi kabisa. Inawezekana kabisa mpaka muda ambao unamaliza kulipia kiwanja hicho tayari kikawa na thamani kubwa kuliko jumla ya makato yako yote. Mali zisizo hamishika ndizo humtambulisha sana mtu mwenye utajiri. Hakikisha utajiri wako unajumuisha pia mali zisizo hamishika kama vile; viwanja, mashamba, nyumba na miti. Ukiwekeza katika ardhi leo, ambapo huenda unazaidi ya miaka ishirini kuelekea kustaafu inawezekana ardhi yako ikakupatia karibu robo tatu ya pesa ambayo utalipwa wakati wa kustaafu (miaka 60).
  4. Jifunge kwa kujiwekea masharti: Mkopo usio na masharti ni mkopo mbaya. Kama benki hawajakupa masharti hakikisha wewe binafsi unajiwekea. Mikopo mikubwa huhitaji mchanganuo wa biashara ambao kwa kiasi fulani unasaidia katika kuleta matokeo chanya ya matumizi ya pesa. Mikopo binafsi ambayo watu wa kati wanachukua ni hatari kwa kuwa haihitaji hata mtu aeleze anapeleka wapi. Unaweza kuzitumia katika sherehe ya ndoa, katika kununulia vinywaji au chochote unachotaka.
Nakushukuru kwa kusoma makala hii. Naaomba kuhitimisha na ninapendekeza usikope kwa vigezo nilivyovitaja katika makala zote nne. Na ukiweza kukopa basi hakikisha unavigezo nilivovitaja katika makala zote nne. Mpaka wiki ijayo, Shalomu!!!

0 comments :

Napendekeza usikope III

3:00:00 PM Unknown 0 Comments

NAPENDEKEZA USIKOPE
(Makala ya Tatu)
Leo nitaanza kutaja njia za kuondokana na madeni. Wengine husema mbona kwenye biblia kuna mfano wa kabaila aliyetoa talanta. Ni kweli upo, lakini waliochukua talanta walikuwa na lengo la kuzalisha na walifanya hivyo. Vipi wewe tangu uanze kuchukua mikopo umezalisha kiasi gani? Tunakopa ili kutengeneza njia ya kutokukopa tena, lengo lingine kinyume na hili ni batili. Walichukua wakazalisha zaidi na nina amini baadaye walirudisha pesa za kabaila na wakapata mitaji yao na kuendelea na maisha yao bila kudaiwa na mtu yeyote.
Matendo yetu hayana nguvu ukilinganisha na kanuni zilizotusukuma katika kutenda matendo hayo. Kama kanuni iliyomsukuma mtu { kukopa} haina msaada basi hata atende kwa umakini wa kiwango cha juu sana bado matokeo yatakuwa mabaya. Kanuni lazima ifafanue sababu. Kwa nini unakopa? Utakopa mpaka lini?
Ile kwamba benki wana hela haina maana lazima twende tukakope, kabla ya kukopa ni lazima nijiulize na kupima ufanisi na uzoefu wangu katika kujitawala na kutumia mkopo. Kinachotokea katika maisha ya sasa ni mkopo unazaa mkopo badala ya mkopo kuzaa uhuru wa kifedha. Wako ambao wamekopa hadi hawakopesheki tena, Hii ni hatari!
Usitegemee mfanyakazi katika taasisi inayotoa mikopo akwambie kwamba, mikopo ni mibaya. Udhaifu wa wateja ndio utajiri na  ujazo tele wa mshahara wake. Inahitaji mtu huru kama mwandishi wa makala haya kuweza kulisema jambo hili. Ili utoke kwenye madeni fanya yafuatayo:
  1. Andika Malengo yako ya kifedha: Ni rahisi kufanya kazi au biashara kuliko kuandika malengo, ndio maana watu wengi wanafanya biashara na kazi bila kuandika malengo yao. Kama ni rahisi wangeandika. Malengo yako lazima yawe na ukomo kama asemavyo Napoleon Hill: “Goal is a dream with deadline
Unahitaji shilingi ngapi katika muda gani? Unahitaji pesa hizo kwa ajili ya nini? Malengo yako lazima yafafanua mambo haya.Kuna kitu cha ajabu kinatokea unapopanga na kukabidhi malengo yako kwa Mungu. Nimeona Mungu akinisaidia katika malengo yangu na mipango yangu ya mwaka huu. Kupanga ni kutumia masaa machache kuishi mwaka mzima, ni kutumia siku moja kuishi mwaka mmoja.
Malengo yako ya kiuchumi yanapaswa kuwa ni zaidi ya kujikimu yaani, zaidi ya kumudu gharama za maisha (maji, nauli, umeme, chakula, ada, pango na maradhi). Ni vyema uandike malengo na mipango ya kukuza uchumi wako. Wanaondika malengo yao hupata kipato maradufu ukilinganisha na wale wasio andika. Asilimia 5% ya watu ambao huandika malengo yao tafiti zilizofanyika huko Marekani zinaonesha ni wenye kipato kizuri kuliko asilimia 95% isiyo weka malengo kwa maandishi. Meneja wa Tigo wa Kanda ya nyanda za juu kusini alisema, “nikishapanga malengo yangu na kuyaandika huyawasilisha kwa mke wangu na mke wangu husaini kama ameridhia au lah!”. Dr Myles Munroe anasema, “Mungu ni Alpha na Omega kwa sababu, Yeye hupanga mwanzo na mwisho wa kila jambo”. Tujifunze kwa Mungu kwa kuanza kupanga na kuandika malengo yetu ya, kiuchumi, kijamii na kitaaluma.
  1. Punguza matumizi: Mikopo si suluhisho la kudumu la matatizo ya kifedha bali ni suluhisho la haraka. Nadhani tunapaswa kwenda katika uhuru wa kifedha wa kudumu badala ya jawabu la msisimko (lasting financial freedom rather than momentary and romantic answer). Kanuni zinaeleza wazi tukitaka uhuru wa kifedha ni muhimu kuzalisha kuliko matumizi yetu ili tupate ziada. Kanuni nyingine ni ile ya kupunguza matumizi yetu ili tunachopata kitoshe na pengine kitupatie ziada. Hatupunguzi matumizi haya milele bali kwa muda tu wakati tunatoka kwenye madeni na tunapandisha juu kipato chetu na mwishowe baada ya kufanikiwa tutarejea katika mitindo ya kisasa na mahitaji tutakayo.
Huwezi kuchangia kila harusi na kila sherehe. Anasa na tafrija zinachukua sehemu kubwa ya kipato usipokuwa makini inawezekana ndiyo kikawa kikwazo cha uchumi wako. Muda huu ninapoandika makala hii nina kadi tatu za harusi, Fikiri!  Ili kupunguza matumizi lazima uweze kusema ‘hapana’ au kusema ‘sina pesa’ hata matajiri wakubwa kunavitu hawana uwezo navyo, ndiyo! There are some stuff even millionaires cannot afford. Nyuma ya matumizi ziko tabia, mihemko na hisia. Kupenda sana mavazi, ulevi, uvutaji wa sigara, kuhonga wanawake, na ulafi. Haya ni mambo ambayo yanaongeza matumizi na nyuma yake kuna kasumba mbaya ambazo zinahitaji tiba. Matumizi haya yanaweza kupungua kama tabia hizo sitapatiwa tiba kwa kuamua kupunguza hatimaye kuacha au kutubu na kugeuka.
Njia rahisi za kupunguza matumizi ni kama: Kununua vitu kwa jumla kwani rejareja ni ghali zaidi (buy in bulk), Kuwa na mtindo rahisi wa kusuka au kujipamba ili kuondoa gharama za saluni, kubeba chakula kutoka nyumbani badala ya kununua katika migahawa iliyoko ofisini, epuka kupita katika maduka ili usijitamanishe (avoid window shopping), kutengeneza vitu vya nyumbani kama juisi za matunda badala ya kununua zilizoandaliwa tayari.
  1. Fanya kazi: Kazi si laana bali ni Baraka. Wito wa kuilima na kuitunza bustani ya Edeni [wito wa kazi] ulikuja kabla hata Adam na Eva hawajakosa kwa hiyo kazi si sehemu ya laana bali ni baraka. Unapoamka asubuhi kwenda kazini basi ujue unakwenda sehemu ya baraka [Mwanzo 2:15].
Mafanikio ya kiuchumi yanapaswa kuwa ni matokeo ya kazi. Ndio maana huwezi kutajirika kwa hela ya kuokota au kwa kucheza michezo ya kubeti. Ndoto au mipango ya kifedha bila kufanya kazi kwa umakini na kwa bidii ni bure. Kupanga mipango tu haitoshi ni muhimu upange na ushambulie [Dream and Fire]. Kuwa na malengo tu haitoshi ni lazima ulenge na kufyatua.
Ni vizuri kutumia muda wa ziada kutafuta kipato cha ziada kwa kuwa ni ziada ndiyo iletayo uhuru wa kifedha. Omba (apply) kazi yenye maslahi bora au fanya kazi katika taasisi mbili kwa wakati mmoja japo hii inachosha sana. Mungu alibariki ardhi na mifugo, ukilima usisahau kufuga na mifugo. Jitahidi kufanya kazi na ziada kidogo. Work and a little bit more
Wiki Ijayo nitahitimisha makala yangu kwa kutaja njia nyingine nne Barikiwa…..

0 comments :