Kwa nini ulianza?

4:03:00 PM Unknown 0 Comments

 
KWA NINI ULIANZA?
Michael Jordan aliwahi kuambiwa na kocha wake akiwa shule, kuwa hana uwezo wa kuwa mchezaji wa “basketball”; leo hii anajulikana kama shujaa katika mpira wa kikapu ulimwenguni. Dr. Myles Munroe aliwahi kuambiwa na mwalimu wake kuwa yeye si binadamu kamili, akili zake ziko nusu, hivyo hawezi kuelewa kama wanafunzi wengine; lakini leo anatajwa kama mwandishi bora aliyewahi kuishi katika nyakati zetu; ambaye  asilimia 80 ya vitabu vyake vimevunja rekodi ya mauzo na kuandikwa katika lugha zaidi ya 60.
Watu hawa walipokutana na hali ya kukatishwa tamaa katika kufikia malengo, ndoto na maono yaliyokuwa ndani yao, hawakurudi nyuma na kujikunyata; ndani yao walijua kwanini walianza safari katika kufikia malengo na ndoto zao. Sababu ya wao kuanza ilikuwa na nguvu, kuliko nguvu ya kukatisha tamaa kutoka katika mazingira yaliyowazunguka. Wewe pia jiulize ni mangapi ungefanya kama tu, ungekuwa na uhakika wa ushindi wakati wa kuanza? Tafakari kwa jinsi ya mshairi huyu anavyouliza. “How many things would you attempt if you know you could not fail” Robert Frost
Watu wakuu hawakuangalia changamoto za fedha au rasilimali zao; hawakuangalia ubaya wa maisha yao ya nyuma; hawakuangalia nani anayewaamini au asiyewaamini; hawakuangalia mazingira magumu waliyokuwa nayo, bali waliutizama uaminifu wa Mungu na uwezo [potentials] uliowekwa ndani yao. Hawakuwa tayari kwa mazingira yao kuamua hatima ya maisha yao.
Na tena, walijua sababu iliyowasukumu kuanza walichoanza. Kumbuka, Unapotambua kwanini ulianza jambo, utapata nguvu na ujasiri wa kusonga mbele [katikati ya changamoto] ili kufikia malengo makuu ulikuwa nayo tangu awali.
Unaposikia hali ya kukata tamaa katika kuelelekea jambo au “project” fulani katika maisha yako; kitu kimoja unaposwa kujiuliza ni je “Kwanini ulianza? Sababu ya kuanza ndiyo sababu ya kuendelea, inakupa nguvu na ujasiri wa kusonga mbele mpaka utakapotimiza ndoto na maono yaliyowekwa ndani yako.
Kumbuka jambo hili, unapokutana na changamoto fulani katika kufikia lengo lilopo mbele yako; endelea kufanya unachotakiwa kufanya, endelea kufanya unachotarajiwa kufanya; hata kama mazingira yanakushawishi kufanya tofauti [1Samweli30:3-4,6,8].
Bwana atanitimilizia mambo yangu…” Zaburi 138:8a


0 comments :

Mabaya hayatakupata wewe

1:17:00 PM Unknown 0 Comments

 
MABAYA HAYATAKUPATA WEWE
(Hata baya litageuka na kuwa jema kwako)

Mungu haleti mabaya; hata kama yakitokea  huyageuza mabaya kuwa mazuri. Kwa wenye tumaini hata wanapoona jambo lenye sura ya kutisha bado wanaamini halitakuwa la kuwadhuru. Wana wa Israeli wakiwa utumwani Babeli, walipatwa na machungu mengi;  hawakuwa na makazi,  tena walitengana na ndugu zao. Katika kizazi chetu cha sasa hatujaonja hali ya utumwa wa kitaifa. Kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli, zamani watu walichukuliwa toka Afrika kama watumwa na kupelekwa Ulaya kufanyishwa kazi nzito. Si rahisi mtumwa kuamini kama bado Mungu ni mwema kwake.
Wana wa Israeli hawakujua mabaya hayo yangekuwa mpaka lini. Hawakujua ukomo wa utumwa wao. Katikati ya shida yao (utumwa) Mungu ananena kwa kinywa cha nabii Yeremia kwamba anawawazia mema. Anapanga mizuri kwa ajili yao kwa hiyo wasiogope. Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” Yeremia 29:11
Si rahisi kwa mtu aliyekatika shida kuamini kwamba Mungu anampango mzuri na maisha yake. Katikati ya ombwe la kukosa ajira lazima uamini Mungu anampango mzuri na wewe. Katika hali ya kuugua lazima ujipe moyo kwamba Mungu anampango mzuri. Katikati ya kutengwa na kuachwa bado lazima utambue Mungu ana kusudi jema. Katika hali ya utumwa Mungu anasema na Israeli kwamba mambo yatakuwa mazuri.
Njia za Mungu ni juu sana. Pale ambapo adui anapanga mabaya na kuleta utumwa Mungu hugeuza mabaya hayo na kuwa mazuri. Wakipanga kukwamisha watajikuta wanakufungulia njia bila wao kujua.
Tyndale Mwingereza ambaye ni mmoja kati ya watafsiri wa awali walioandika Biblia katika lugha ya kiingereza anahusishwa na simulizi zenye mafunzo mengi. Tyndale alifanya kazi kama mtafsiri katika nyakati ambazo Biblia ilikuwa katika lugha ya kilatini na haikuruhusiwa kutafsiri kwenda lugha nyingine. Kwa nia ya kumkwamisha, Askofu mmoja wa Durham alinunua nakala zote za Biblia toka kwa mwuza vitabu kwa nia ya kwenda kuziharibu, akidhania kwamba jambo hilo lingekwamisha kazi ya Tyndale. Badala yake pesa hiyo ilitumika kununua malighafi zilizoandaa toleo jipya na bora zaidi. Tyndale alipohojiwa akiwa gerezani alitakiwa amtaje aliyemfadhili katika uandishi wa toleo bora la Biblia alisema ni Askofu Durham. Nadhani umeona walipanga kumkwamisha kwa kununua Bibla zote na kuzichoma wasijue ya kwamba, pesa yao inaweza kusaidia kuandaa toleo bora zaidi.
Tangu kale mpaka sasa Mungu ni mwema. Kila mahali wanasema Mungu ni mwema wala huna haja ya kuogopa. Yesu Kristo ni mfalme na alikuja kutuokoa, lakini njia aliyoitumia kutuokoa haikueleweka mioyoni mwa wengi. Wengi walidhani mfalme atatuokoa kwa kutumia vita wala si kwa njia ya msalaba. Wengi waliona msalaba kama njia dhaifu, walitegemea kuona farasi wa moto, mabomu na mikuki, kwao kufa msalabani haikuwa njia sahihi ya kutuletea wokovu.
Oh! ilionekana ni njia dhaifu kumbe ni njia sahihi na kamilifu. Endelea kumtumaini Mungu, mwombe akuletee wokovu lakini usichague njia. Hata kama hatuoni wala kuzielewa njia za Mungu bado twaweza kuziamini. Don Moen mwimbaji wa nyimbo za injili mwenye alama amerekodi maneno haya kwa uchache nanukuu: “He (God) works in ways we cannot see” (Mungu hufanya kazi kwa namna tusiyoweza kuona)
Hata shetani hakujua kwamba kwa njia ya msalaba watu watakombolewa. Angelijua asingelimchinja Yesu Kristo. Hawakujua kwa njia ile dhaifu BWANA anatupatia ushindi. Mwenye hekima mmoja anasema: “When the devil killed Jesus, Jesus Killed the devil.” Yaani, “Pale shetani alipomuua Yesu, Ndipo Yesu alipomuua shetani.” Endelea kumwamini Mungu.

0 comments :

Kifo ni hatua muhimu kuelekea mafanikio

2:11:00 PM Unknown 0 Comments

 
KIFO NI HATUA MUHIMU KUELEKEA MAFANIKIO
(DIE TO SELF AND LIVE ALL TO HIM)

Kifo hakina maana moja tu; Kifo ni zaidi ya kupoteza pumzi. Tunapoacha kila jambo tulipendalo kwa ajili ya Bwana tunakuwa wafu katika hali yetu ya ubinafsi na tunakuwa hai kwa BWANA. Tunapopenda mambo yetu binafsi na kuyakataa ya BWANA MUNGU tunakuwa hai kwetu na tunakuwa wafu kwa BWANA. Jambo la msingi ni kuwa hai kwa BWANA. Biblia inatutaka tujitoe kama dhabihu hai. “…Itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai...” Warumi 12:1
Watu wengi wakuu wamepitia kifo, na katika kipindi hicho cha kifo agenda zao binafsi zilikufa na agenda za Mungu zikahuishwa na kutukuka katika maisha yao. Miaka 27 jela ilimfanya Nelson Mandela awe kama mfu katika ubinafsi wake, miaka 40 ambayo Musa alikaa Midiani ilimfanya awe mfu kwa agenda binafsi na awe hai kwa agenda za Mungu. Charles Spurgeon amewahi kusisitiza kwamba ufunguo wa mafanikio yote ni mmoja nao ni: “Die to self and live all to Jesus” yaani, “Ufe katika ubinafsi wako na umwishie (uwe hai) Kristo”
Hudson Taylor Mmisionari aliyeacha alama ya aina yake kule China amekuwa msaada kwangu kila nisomapo habari zake. Naye kama mtu mwingine yeyote alilazimika kufa ili mapenzi ya Mungu yachukue mkondo katika maisha yake. Hii ni moja ya kauli zake kabla ya kuliacha jiji zuri la London na kuelekea China kama Mmisionari. Alisema, “Kwa ajili ya kusudi la kwenda China niko tayari kutoa kila kitu, kila sanamu, hata kama ninaipenda.”  Yaani  “For this I could give up everything, every idol, however dear”
Kwa kuwa Mtume Paulo alipenda sana sheria kuachana na sheria kwake ilikuwa ni sawa na kifo. Kwake kuacha sheria na kuiona kama mavi ni kuachana na jambo alilolipenda mno. Kwa ajili ya utukufu wa Mungu aliachana nayo. Maandiko yamemnukuu akisema amepata hasara ya mambo yote kwa ajili ya Kristo. Ni kauli ya ndani, ni kionjo cha moyo. Nimepata hasara ya mambo yote! Paulo alikufa katika ubinafsi wake ili Mungu atukuzwe. “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.”Wafilipi 3:7
Kila mtu mkuu ninaye mtazama kwa asilimia fulani naona jinsi alivyokufa katika mambo binafsi ili ajenda za Ki-Mungu na Ki-utu zipate nafasi. Nyerere alijikatalia wizi ili usawa utawale nchini mwetu Tanzania. Tangu akiwa sekondari Tabora  hakuwapenda wanafunzi waliokuwa wanachukua chakula kingi bila ya kujali wenzao. Bill Winston aliacha kazi ili kutii wito wa Mungu wa uinjilishaji. Reinhard Bonnke alijikatalia kukaa Ujerumani baada ya kuona maono ya bara la Afrika likioshwa kwa damu ya Yesu, akaamua kuja Afrika. Leo hii hawa wote ni watu wakuu na waliofanikiwa kuandika historia nzuri.
Je, uko tayari kuacha ubinafsi na kufa ili Mungu aishi ndani yako? Je, unadhani ni kitu gani Mungu anataka utoe kwa ajili ya utukufu wake? Umewahi kuwaza uzuri wa mafanikio yako ikiwa utatii na kujitoa kwa Mungu?
Nasikia moyoni mwangu ule wimbo wa tenzi “Yote kwa Yesu” ukiimbwa hebu utafakari na ukiweza imba. Moja ya beti inasema, “Nimeacha na anasa kwako Yesu nipokee.”   Oh! jitahidi ujitoe kwa Yesu, na kuachana na anasa za kidunia. Yes All to Jesus I surrender…Endelea kuimba na hakikisha unajitoa na unayaua mapenzi yako ili Yesu atukuke.  Mpaka wiko ijayo, Shallomu!

0 comments :

Utamaduni wa Yesu

11:35:00 AM Unknown 0 Comments


 
UTAMADUNI WA YESU
(JESUS CULTURE OF WORSHIP)
Utamaduni wa Yesu Kristo ni kuabudu. Katika siku zake hapa Duniani Yesu alijijengea kasumba ya kuabudu mara kwa mara. Wanaoabudu sanamu wanafanana na sanamu, na wanao mwabudu Mungu hufanana na Mungu. Kwa jinsi tunavyomwabudu Mungu zaidi ndivyo tunavyofanana naye zaidi.  Si ajabu ndio maana Yesu alifanana na Baba yake wa mbinguni. Nawaonea huruma wanaoabudu sanamu; fedha, muda, watu au vinyago kwa kuwa mwisho wa siku watafanana na sanamu zao, “Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia.”  Zaburi 115:8
Ni saa kumi na mbili jioni namaliza kutafakari. Mawingu ni ya bluu kidogo na hali ya hewa ni tulivu. Jua linaanza kuzama na mwangaza wake unafifia. Japokuwa kule kwetu Mpanda ni joto, lakini wakati jioni hali huwa ni rafiki. Na mara namwita kwa sauti mpwa wangu, “Benjamini, Benjamin, twende.” Tabiri, tunataka kwenda wapi na Benjamini? Tunakwenda mlimani mahali ambapo watu ni wachache, huko tutamwabudu Mungu na kumshukuru. Tunadumisha utamaduni wa Yesu ambao ni kuabudu. It was His dominant culture to worship God.
Zamani za kuhani Eli, Elkana wa Rama alikuwa akienda kuabudu kila mwaka. Alikwenda kila mwaka kwa kuwa zama zile watu walikwea kwenda mbali sana kuabudu. Walikuwa wakiabudu milimani tu ama Yerusalemu tu na hivyo ililazimu safari ndefu. Lakini sasa tunamwabudu Mungu katika roho na kweli, tunamwabudu mahali popote na muda wowote.Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko.”  1Samweli 1:3
Leo hii hatuendi mlimani wala Yerusalemu. Tunamwabudu Mungu barabarani, chumbani, kanisani, ofisini hata vitandani mwetu. Tunapofanya kwa utukufu wake maana yake tunamwabudu Mungu. Unaweza kumwabudu Mungu wakati wowote iwe ni katika kusoma au wakati unakula chakula. [1Kor 10:31]
Je, unataka kufanana na Mungu? Hakikisha unamwabudu na unamshukuru. Je, unatabia ya kuabudu? Unaweza kuamua kujijengea tabia ya kuabudu; na ni rahisi, tabia ni mazoea, mazoea hujengwa kwa kutenda jambo kwa kurudia rudia. Unamshukuru Mungu asubuhi, mchana jioni hata usiku.
Kwa kuwa Mungu ni mkuu ni vema ukapiga magoti na kumwangukia, ukijua wazi kwa njia hiyo unafanana naye. Ametutaka tumwabudu akijua kwa njia hiyo atatuinua.  Tafadhali mwabudu leo.  Amani ikae na waabuduo halisi na watu wote waseme Amina!


0 comments :