WEWE NDANI YA KUSUDI LA MUNGU
WEWE NDANI YA KUSUDI LA MUNGU
(Samaki
ndani ya maji, wewe ndani ya kusudi la Mungu)
Hapo
mwanzo kila alichokiumba Mungu aliona kuwa ni chema ‘good’; alionesha kuridhishwa na hali yake. Mungu huvipenda vitu
vyote alivyoviumba. Mungu hupenda watu tofauti tofauti, wenye vionjo na tabia
tofauti tofauti. He is God of Varieties!
Alimpenda Musa mpole, lakini alimtaka Haruni ambaye ni msemaji (mwongeaji)
amsaidie Musa. Mungu anakusudi jema na watu wa haiba zote, kasumba mbali mbali
au silika yoyote ile. [Mwanzo 1:31]
Kama
aliyekuumba amesema wewe ni mwema ‘good’ maana yake uko tayari kwa kazi fulani.
Alipoitazama ile kazi na alipokutazama wewe akasema vema, maana yake ameonesha
kuridhishwa na uhusiano uliopo baina yako wewe na kusudi uliloitiwa.
Ukiona
uko katika eneo ambalo linakuhitaji ujifanyie marekebisho makubwa sana (massive
change) ili uwepo wako ufae katika eneo hilo, lazima ujiulize mara mbili;
inawezekana si eneo lako. Ukiona uko na
mtu anayetaka ubadilike sana ili umfae yeye, ujiulize mara mbili pia;
yawezekana si wa shirika lako. Kusudi la kuumbwa kwako ndiyo bahari pekee unayoweza
kuogelea kwa urahisi. Samaki hafanyi
marekebisho yoyote ili afae kukaa majini, wala tai hafanyi marekebisho ili
kuruka, anafanana na kusudi lake. Sihitaji
kuwa mtu fulani ili niwe mimi.
Tunapoteza
muda mwingi tukisubiri kubadilika, ati! ndio tuanze. Ukweli ni huu: “Agent of
change never change” yaani, wakala wa mabadiliko habadiliki. Kama umezaliwa
kubadilisha ulimwengu maana yake wewe umeshabadilika tangu hujaja duniani. Kama
umezaliwa kuwatoa watu utumwani maana yake wewe si mtumwa. Musa hakuwahi kuwa
mtumwa japo alikuwapo Misri. Yesu hakuwahi kutenda dhambi japo aliishi duniani.
Kama umezaliwa ili kufa, maana yake umeshakufa hata kabla hujazaliwa (mkumbuke
Yesu). “...Mwana-Kondoo,
aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia” Ufunuo 13:8
Mungu
haleti wanafunzi wa kada fulani hapa duniani, Yeye hushusha watendaji ambao
tayari ni imara kabisa. Huleta askari
walio tayari kwa vita na si kwa mafunzo. Ukizaliwa tu, ujue umeshatumwa; si
lazima ukae na Yesu miaka mitatu kama mitume; ni hasara kuwa mwanafunzi
asiyehitimu. Habari yako ni ya tofauti, umezaliwa ukiwa tayari. “Bwana akawatuma (wakazaliwa) Yerubaali,
na Baraka, na Yeftha, na Samweli, akawaokoa ninyi na mikono ya adui zenu pande
zote, nanyi mkakaa salama.” 1 Samweli 12:11 [Maneno ya kwenye mabano
ni msisitizo wa mwandishi].
Shida
zako zinakusaidia kujua jambo moja kubwa kwamba, “wewe ni mkimbizi.” You’re
not where you belong! Bora uwe mkimbizi katika nchi jirani kuliko kuwa
mkimbizi katika kusudi la Mungu. Unafanya vizuri kazi isiyokupasa kufanya,
unakula usichopaswa kula, na una marafiki usiopaswa kuwa nao. Hii ilimpata
mwana mpotevu; alikula na nguruwe, badala ya kula na Mungu, si unajua ukifungua
moyo Yesu atashinda kwako na kula pamoja na wewe. Usipofungua mlango ndio
habari ya kula na nguruwe inakuja. {Ufunuo 2:20}
Mwana
mpotevu alipogundua ukweli kwamba, anatawaliwa na mazingira badala ya yeye
kuyatawala aliamua kuondoka. Kusudi ndilo linakupa uwezo wa kuyatawala
mazingira badala ya mazingira kukutawala wewe. Tukimtosa mtu baharini bila ya
kumwokoa au kumpa vifaa vya kumsaidia, bila shaka baada ya kitambo atakufa. Si
kifo cha bahati mbaya, mazingira (maji) yamemtawala. Mungu alitaka tuyatawale
mazingira yetu kupitia kuishi kusudi,
kila yanapotutawala yanaashiria kifo.
Baba
anaweza kukukataa, hata mama anaweza pia. Ni sehemu moja tu unayoweza
kupokelewa bila ya kuambiwa ondoa hiki na kile kwanza, nayo ni katika kusudi
lako. Your purpose will adopt you as a
lovely son/daughter.
Kama
nimezaliwa kucheza mpira si lazima nicheze kwenye kiwanja cha mtu asiyenitaka,
pia si lazima nicheze katika timu isiyonikubali. Ndio maana kuna viwanja vingi
na timu nyingi. Kamwe usibadili uamuzi wako wa kucheza mpira bali badilisha
timu na viwanja. Nimewahi soma nukuu
hii: “Change direction but don’t change
your decision.”
Ni
sehemu moja tu ambapo hisia zako zote hupokelewa, ni mahali pale tu ndipo kimo
chako huleta maana, ni katika kusudi uliloitiwa na Mungu ndipo haiba yako;
utanashati wako, kujisahau kwako, ukimya wako, mihemko yako, haraka zako,
udadisi wako, ujasiri wako, hekima yako na upole wako hupokelewa kwa moyo wote.
Ni katika kusudi la Mungu ndipo Musa mpole na Haruni msemaji wote huwa na maana. {Kutoka 4:14}
Sijui
unapata taswira gani unapomuona kaka mtanashati, sijajua unawaza nini
unapomuona dada mrembo, binafsi ninajua jambo moja, “mwili ni kwa BWANA.” Kama
alivyoagiza Yesu mitume wamfungue yule punda na atakayeuliza ajibiwe hivi:
“BWANA anahaja naye.” Ndivyo ilivyo kwako, BWANA anahaja nawe na namna ulivyo. “... Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni
kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili.” 1Wakorintho 6:13
Mungu
ni Roho, roho haili nyama ya mtu wala ya punda. Ukisikia maandiko yanasema
BWANA anahaja nawe ujue kinachotajwa hapo ni utumishi au kusudi la kuumbwa
kwako wala si ,’lunch’. Biblia inasema “mwili si kwa zinaa bali ni kwa ajili ya
BWANA.” Mwili wako unaakisi kusudi lako. UKiliendea kusudi lako litakupokea
bila ya kukuambia jikarabati kwanza. Kwani
tayari unafanana na kusudi lako, hakuna haja ya ukarabati.
Biblia
inatafsiri, mwili ni nyumba ya roho. Si kila nyumba ni kwa ajili ya kulala,
nyingine ni ofisi. Nadhani kwa mtazamo wa biblia, mwili ni ofisi. Ofisi huakisi
kazi za taasisi husika. Kwa mamantilie jiko ni ofisi, kwa fundi makenika Gereji
ni ofisi. Jiulize nini kinafanyika katika mwili wako kama ofisi. Muonekana mzuri na tabasamu bashasha usio
sadifu matendo unatupa nafasi ya kujua kwamba hauishi kusudi lako. Kaka mzuri
unavuta sigara, balaa gani kama hii! Dada mzuri lakini kahaba, ni msiba gani
kama huu! Jengo linaashiria kusudi jema lakini kinachotendeka ndani ya ofisi
(mwili) ni ubatili.
Hadi
biblia ikasema, “mwili si kwa ajili ya zinaa” maana yake watu hudhani mwili ni
kwa ajili ya zinaa. Mtazamo huo mbovu umepelekea kusudi la Mungu
kusahaulika.Tujifunze kwa Yesu, alipata mwili ili autumie katika mateso na
kuleta ukombozi. Alikuwa na sababu za kiofisi za kuvaa mwili. Bila mdomo
asingelikunywa siki, bila mabega asingelibeba msalaba. Mwili ni kwa ajili ya utimilifu wa kusudi.
Mwili wake ulikuwa ofisi ya kutimizia kusudi. Alionekana kama kusudi lake, wewe
pia umefanana na kazi fulani au wito fulani na Mungu amekushakupa ofisi yaani,
mwili.
Kama
una mwili lazima ujue lipo kusudi kwa ajili yako. Unamsubiri Mungu? Alishasema
imekwisha, tena akasema kila alichokiumba ni chema; Anakusubiri wewe. Badilisha
mtazamo wako, anza hiyo safari, anza sasa hiyo biashara, ondoka huo mkoa uende
anapokupeleka Mungu. Labda ulikimbia shule rudi masomoni, anza kulifanyia kazi
hilo wazo, chukua fomu na ugombanie hiyo nafasi, anza kuamka mapema, anza
kuishi hilo kusudi, anza kuwasaidia yatima, labada ni mhudumu anza sasa
kuhudumu, tekeleza azma ya moyo wako na kuyatawala mazingira yako. Badala ya
kuishia kujivika nguo nzuri (pamba kali) za kisasa wewe tinga kusudi la Mungu
na kisha utoke, wakati ni sasa! Ogelea.
0 comments :