KILA KITU KIPO KWA KUSUDI MAALUMU

8:06:00 PM Unknown 0 Comments

  
KILA KITU KIPO KWA KUSUDI  MAALUMU
Kutambua sababu ya kuwepo kwako ni jambo la msingi kuliko yote unayoweza kufanya, vinginevyo maisha yanakosa maana. Kusudi ndilo linatoa msukumo wa kuwepo au kutengenezwa kitu ili kutimiza malengo maalumu kwa wakati uliowekwa. Kusudi la kuwepo kwako ndilo linaloleta maana na utoshelevu hata kwa vitu vingine.
Kusudi maana yake ni sababu iliyofanya au inayofanya kilichopo kiwepo au kitengenezwe jinsi kilivyo ili kutimiza kazi maalumu katika kufikia malengo yaliyokuwa yamekusudiwa kabla ya kitu hicho kuwepo au kutengenezwa. Kila kitu kipo kwa kusudi maalumu; hakuna kilichoumbwa au kutengenezwa kiwepo kwa sababu ya kuwepo tu. 

Maua yapo kwa kusudi, wadudu wapo kwa kusudi maalumu hata wanyama wapo kwa kusudi maalumu; wanasayansi wamegundua kuwa kuna baadhi ya viumbe endapo vitatoweka, mfumo wa ikolojia (Ikolojia ni mfumo wa ki-biologia unaoonesha kutegemeana kwa viumbe hai, pamoja na mazingira yao katika kuendeleza uhai) utaadhirika na hivyo kuhatarisha uhai wa binadamu. Ikiwa viumbe hivi vipo kwa kusudi maalumu je, si zaidi ya mimi na wewe?
Ile kwamba kila kitu kimeumbwa kwa kusudi maalumu haina maana kwamba kila kitu kinaishi kulingana na kusudi hilo la kuwepo kwake. Dr. Myles Munroe katika kitabu chake cha Understanding purpose and power of men, ameandika “Kusudi la kitu lisipojulikana, matumizi mabaya hayaepukiki”. Usipojua kwanini umeumbwa maisha ya kila siku yanakuwa ni majaribio. Tumepewa muda wa kuishi; hatujapewa muda wa majaribio ya kuishi. Watu wengi wamekutwa na mauti wakati bado wanajaribu kuishi. What a tragedy!
Yeremeia akiwa bado kijana mdogo alijijua kuwa yeye ni nabii wa mataifa, Daudi akiwa bado kijana mdogo alijijua kuwa yeye ni kiongozi wa Israeli, Yesu akiwa bado kijana mdogo alijua jambo gani limempasa kufanya (Luka2:49-50).
Ufanisi katika maisha ya mtu haupimwi kwa kuangalia ameishi kwa muda gani, bali hupimwa kwa kuangalia kwa namna gani mtu ameishi kulingana na kusudi la kuumbwa kwake. Si kwa urefu bali kwa ukamilifu.
Mungu hana upendeleo kwa mtu yeyote; ikiwa Yeremia, Paulo, Musa na watu wengine wakuu tunaowasoma kwenye Biblia na hata nje ya Biblia kama Mother Teresa, Martin Luther King Jr na wengine wengi ambao majina yao na kumbukumbu zao zinaheshimiwa hata sasa, waliumbwa kwa ajili ya kutumikia kusudi maalumu la Mungu; hata wewe unalo kusudi maalumu juu ya kuumbwa kwako wakati huu; lakini  tunaanza na Mungu.
Wewe pia ni jibu
Kila aliyezaliwa na mwanadamu ni jawabu, wala hakuna haja ya kutafuta majibu nje yako; umekuja kuleta majibu juu ya swali au changamoto au upungufu uliopo duniani ambao unahitaji uwepo wako.
Musa alizaliwa akiwa kiongozi, aliyebeba jibu la Israeli juu ya utumwa wao katika nchi ya misri; Gideon alizaliwa akiwa mtetezi wa Israeli aliyebeba jibu la mateso ya Israeli juu wa wamidiani; Samson alizaliwa akiwa kiongozi wa Israeli aliyebeba jibu la mateso ya Israeli juu ya Wafilisti. Yesu Kristo pekee ndiye Aliyebeba jibu juu ya dhambi na uonevu wa shetani kwa wanadamu.
Kutokujua kusudi au sababu ya kuwepo kwa kitu, haifanyi kitu hicho kukosa sababu ya kuwepo kwake. Ile kwamba hujajua bado kusudi la kuwepo kwako haina maana hamna kusudi la kuwepo kwako. Kusudi la kuwepo kwako ndilo lililofanya uwepo wako uwe muhimu.
Mungu aliliweka kusudi lako kabla ya wewe haujazaliwa; Mungu aliamuru idadi ya siku zako kabla hazijaanza kuhesabiwa hapa duniani.
“Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; chuoni mwako ziliandikwa zote pia, siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado Zaburi 139:16-17!
[Msisitizo umeongezwa]
Mungu hutangaza mwisho wa jambo mwanzoni; Huuweka mwisho wa jambo kabla ya kuanza jambo lenyewe. Ukiona Mungu ameanza jambo, basi ujue mwisho wake upo tayari. Mungu haanzi jambo lolote bila ya kuhakikisha kuwa kila kitu kitakachohitajika ili kutimiza kusudi hilo kipo tayari. Hii ni kanuni ya Ki-Mungu isiyobadilika; Na inakupa uhakika kuwa lipo kusudi maalumu juu ya kuumbwa kwako. [Isaya46:10-11]
Siku Moja Yesu aliwafundisha  wanafunzi wake kanuni hii muhimu inayokupa uhakika wa kufanikiwa katika maisha ya kila siku. Aliwafundisha kwa mtindo wa swali akisema,
Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.” Luka 14:28-30
Ile kwamba umezaliwa na bado unaishi hadi muda huu unaposoma ujumbe huu, ni udhibitisho tosha kwamba Mungu analo kusudi maalumu kwa ajili yako litakalo kuwezesha kuishi maisha yenye ufanisi na mafanikio ya kweli; Na kwamba, kile Alichokianza katika maisha yako Anao uwezo wa kumaliza.
Tunaanzia hapa!
Maisha ya mwanadamu ni kama kitabu, kwa jinsi anavyokaa na Mungu ndivyo kinavyozidi kufunguka kurasa hadi kurasa. Hayati Dk. Myles Munroe anaandika katika kitabu chake cha Understanding your potential, kwamba “Hatuwezi kujua sisi ni nani kwa kuhusiana na viumbe, bali tunaweza kujitambua kwa kupitia kuhusiana na Muumba”
Huwezi kujitambua wewe ni nani na kuitambua kazi uliyoitiwa na Mungu hata ukatembea katika kusudi la kuumbwa kwako kabla ya kukutana na Mungu, na kuwa na uhusiano naye binafsi
Musa alijua kusudi lake alipokutana na Mungu nyikani; Sauli (Paulo) alijua kusudi lake alipokutana na Yesu njiani, Petro na Yohana pia kule ziwani. Ni ajabu wengine wanaweza kukutwa na mauti kabla hata ya kugundua kazi maalumu na sababu ya kuumbwa kwao.
Kabla ya Mungu kukufunulia kusudi lake kwa maisha yako, Hujifunua kwako kwanza; Hukukutanisha na U-Mungu wake kwa kuwa umetoka kwake na wewe ni sura na mfano Wake [Mwanzo1:26]. Ndio maana kumpokea Yesu ni Muhimu si tu kwa ajili ya kwenda Mbinguni lakini pia inakupa fursa ya kutambua kusudi la Mungu kwako kwa hapa duniani na kukuwezesha kuishi maisha yenye ufanisi na mafanikio huku ukimaliza “mwendo” bila majuto. Hautamaliza bila kuanza sasa;

“Ni lazima kuishi katika kusudi hata kama halituvutii sana.”

0 comments :