Ubongo hauna rangi
UBONGO HAUNA RANGI
(Brain has
no colour)
Hakuna utofauti wa akili kati ya bara moja
na lingine, hakuna utofauti katika kuumbwa kwa Mzungu na Mwafrika, sote tu sura
na mfano wa Mungu. Hakuna tofauti kati ya watu wa magharibi na watu wa kusini.
Kila mtu anaweza kuwa atakavyo, na anaweza mambo yote. Kila mwasisi wa Taifa
ana nafasi ya kulifanya taifa lake kuwa nambari moja kwa maendeleo.
Ulipopewa rangi nyeusi ya mwili si kwamba
umepewa ubongo mweusi. Ubongo hauna rangi, mtu mweusi hana ubongo mweusi, wala
mtu mweupe hana ubongo mweupe, ubongo ni ubongo tu. Ukikuta ubongo mweusi basi
ni wewe mwenyewe umeupaka rangi nyeusi. Wakati Wright Brothers wanavumbua
urushaji wa ndege wengine wanarogana. Wakati mmoja anaun’garisha ubongo wake
kwa kusoma kitabu kizuri mwingine anatazama picha za ngono na hivyo anauchafua
zaidi. Sote tumefanya hayo lakini leo makala hii ni simu ya kukuamsha, Brain has no colour!
Ben Carson, Usain Bolt, Hayati Dr Myles
Munroe ni miongoni mwa wachache walioihakikishia dunia kwamba, wana ngozi
nyeusi lakini hawana ubongo mweusi. Hofu, mashaka, kutokujiamini, uchoyo,
ubinafsi, uchafu, uchawi, ulevi, ulafi, uasherati na vingine vingi huchafua
ubongo na kufanya uwe na rangi nyeusi. Ili uhakikishe hili, chunguza na
utagundua jamii nyingi zenye mambo ya kishirikina ziko nyuma kielimu, na
familia za kuhusudu ulevi huwa hazisongi mbele.
Kwa asili mwanadamu anazaliwa akiwa na
ubongo wenye kumpa akili ya kutenda mambo yote, kuweza kila kitu kwa wakati.
Yale yasiyofaa ambayo mwanadamu huona na kusikia huendelea kumharibu na kufanya
awe na hofu, kujidharau, kujiwekea mipaka ya kiutendaji. Wafilipi 4:13
Usimfundishe mwanao kuwatukuza wazungu,
bali mwambie ana ubongo sawa na wao na anaweza kufanya zaidi ya wao. Darasa
moja, mwalimu mmoja na shule moja lakini matokeo ya watoto huwa tofauti kwa
sababu ya vizuizi tunavyowawekea. Mwingine anaambiwa anga ndio kuzuizi chake
mwingine anaambiwa ajira, ukiajiriwa tu inatosha mwanangu! Huna wa kuajiriwa
hawezi jihusisha na tafiti za kurusha vyombo kwenda mwezini au kupasua vichwa
vya watu, hii ni kwa sababu upatikanaji wa ajira ni rahisi na hivyo kufikiri
kwenda mwezini au kuwa daktari bingwa ni kama kupoteza muda.
Tatizo lolote ikiwamo la ajira, kabla
halijawa la Serikali ni la wazazi wa mtoto, baadaye ni la mtoto mwenyewe, na
mwisho ni la nchi. Ubongo wetu unapakwa matope na mafuta machafu ya mawazo
mgando ndio maana tunashindwa kufikiri kimkakati.
Tunashindwa kupenya katika majadiliano yenye
maslahi makubwa. Mawazo mabaya si kuzini na kuua watu tu, bali ni uoga.
Tunaogopa kuanza, tunaogopa kugombea, tunaogopa kuamka mapema, tunaogopa
kusafiri, tunaogopa kukopa, tunaogopa kuacha kazi, tunaogopa kusimamia mawazo
yetu, tunaogopa kweda nchi za mbali. Ukienda uwanja wa Ndege utaona wanaoingia
kwetu ni wengi kuliko wanaotoka, sisi tunaogopa wao wanakuja. Hawajui lugha
yetu, wala hawajui asili yetu ila wanakuja kisha wanafanikiwa na wanaondoka.
Jifunze kwa wachina waliojazana Kariakoo Dar es salaam.
Ubongo hauchakai kwa sababu unautumia sana,
bali unachakaa kwa sababu hautumii akili. Ni kweli hukupata muda wa kwenda
shule sawa, Je, hujapata hata muda wa kufikiri? Tofauti kati ya msomi na mtu
ambaye hakusoma ipo kwenye kufikiri. Ukiweza kufikiri vizuri na kupanga
kimkakati basi wewe ni msomi. Ni vijana wachache ambao hufikiri kimkakati yaani
akapanda au akawekeza katika mradi utakao mlipa baada ya miaka hamsini.
Azimio la Arusha lilikuwa tunda la akili ya
mwalimu Nyerere, Tuzo ya Nobel ni mtoto wa akili ya Mzee Alfered Nobel
aliyesikia sifa zake mbaya na kubadilika. Afrika kusini huru ni mtoto wa akili
wa Hayati Nelson Mandela, Microsoft Cooperation ni mtoto wa Bill Gate, TANU si
ni mtoto wa Mwalimu Nyerere.
Je, akili yako imetuzalia nini cha maana? What is your brain child?
Wanaotumia akili zao vizuri hubuni,
huanzisha na huvumbua. Huasisi mataifa, huanzisha viwanda na makampuni,
huanzisha taasisi zao. Hawafi wakiwa wamelala kitandani, hufa wakiwa katika
mapambano ya kukamilisha azma na wito wao.
0 comments :