Mungu ni mwakilishi wetu
MUNGU NI MWAKILISHI WETU.
(Anajua kupigana vizuri kuliko sisi)
Tunaishi kwenye
ulimwengu wenye changamoto nyingi, watu wanafukuzwa kazi, yatima wanadhulumiwa;
wanafunzi wanafeli, wazazi wanagombana, wapenzi wanaachana na vikao vya kazi
havimaliziki kwa usalama.
Yote haya
yanamfanya mwanadamu ajitahidi kuyakabili bila ya Mungu. Kuna kitu kinamwambia
mwanadamu apigane mwenyewe, kuna msukumo usiotaka kumruhusu Mungu apigane.
Kwa nini
tunashindwa kumruhusu Mungu aingilie kati? Ni kwa sababu tunadhani tunajua
kupigana kuliko Yeye au ni kwa sababu tunafikiri atasahau. Ukweli ni kwamba
Mungu anajibu kwa wakati, yuko makini kuliko wahudumu wa chumba cha watu
mahututi.
Siku moja usiku
baada ya kuona nyumba yangu imezingirwa na mambo yasiyofaa niliamua kumwita
BWANA YESU na dakika ile ile shwari ilirejea. Namshangaa Mungu kwa maana
amewapa mamlaka kuu wale wanaompigania. Hudson Taylor akijua fika atakwenda
nchi ya mbali kwa uinjilishaji, alijifunza kumtegemea Mungu kwa kila jambo.
Hata alipotaka pesa hakumwambia mkuu wake wa kazi bali alimwambia Mungu katika
maombi. Ananukuliwa, “ni vema nijifunze kumwomba Mungu kwa kila jambo, maana
huko China niendeko hakuna mtu wa kumwomba wala kumtegemea”.
Katika biblia
tunaona Mungu amekuwa sauti ya wasio na sauti, amewakumbuka matabaka ya
walioonewa. Yeye ni Mungu wa vita, anajua kupigana tena ameshinda vita zote.
Kuomba ni kumchagua Mungu awe mwakilishi wako katika vita. Ndio maana biblia
imeyaita maombi silaha. Waefeso 6:11
Uwezo wa
mwanadamu unakikomo, hata akijitahidi hawezi kutuliza yote yanayomsonga.
Taarifa ya habari si taarifa yenye habari za kutia tumaini bali ni taarifa yenye
habari mbaya; mafuriko, njaa, migomo, ugomvi, kupunguzwa kazini, vifo na
magonjwa.
Nakumbuka siku
moja nilipopokea taarifa ya kutisha kwamba mpendwa wangu yuko mbioni kufa.
Niliogopa sana! Moyo wangu ulizimia kwa hofu. Siku yangu ilikwenda mrama
kabisa. Mara ghafla jioni rafiki yangu akanishauri na kutumia Zaburi 46:1-3. Na
hapo nikapata nguvu, na hapo nikapata upenyo na hapo nikasimama tena. Na hapa
nikajua kama ni vita si mimi nitakaye kufa, bali ni wenzangu ndio watafia nchi zao
na falme zao.
“Mungu kwetu
sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.” Zaburi 46:1-3
Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.” Zaburi 46:1-3
Nikamkimbilia
Mungu kwa sala, tukashinda vita na mpendwa wangu akawa salama! Tishio la kifo,
ajali, hukumu ya Mahakama, Waganga, Wachawi halina uwezo wowote kwa yule ajuaye
kuliitia jina la BWANA, yule aliyepaka damu ya Yesu ya Pasaka.
Kujiambatanisha
na Mungu ni kujiambatanisha na ushindi. Kama wakristo sisi ni washindi, maana
tu uzao wa ushindi.
Mkimbilie Mungu
ukiwa na cheti cha daktari, mwambie utaishi kwa neno lake wala si kwa chakula,
wala si kwa neno la daktari. Ingawa tunaheshimu mchango wa kila taaluma lakini
Bwana ndiye atakaya maneno yote, kwa kuwa Yeye ni mwanzo tena mwisho. Hata kama
umetenda dhambi usisite kumwendea Mungu wakati wa changamoto yako. Yeye ni
kimbilio wakati wa shida, shida zinaturejesha kwake.
0 comments :