Mungu Anakutazama
MUNGU ANAKUTAZAMA
(Maovu na mema yote hutendeka mbele
ya macho ya Mungu)
Katika
tasnia ya michezo, wengi wetu tumezoea kucheza vizuri mahali ambapo mashabiki
au watazamaji ni wengi. Si wachezaji wengi wanaweza kujituma na kucheza kwa
bidii sirini. Wengi hupenda kucheza vizuri wakiwa wanatazamwa na maelfu ya
mashabiki jukwaani. Si ajabu ndio maana viwanja kama Old Trafford na Stanford
Bridge (viwanja vya soka) huchukua mashabiki wengi, na wachezaji hujiona
wabarikiwa wakisakata katika nyasi hizo.
Lakini
ni lazima tujue wazi kwamba, Mungu ni mkuu kuliko watazamaji, anaona ndani ya
mioyo yetu na hata nafsini mwetu. Ufanisi wake katika kuyatazama maisha yetu ni
mkubwa kuliko mamilioni ya mashabiki wasioweza kutazama mpaka moyoni. Mwenye
hekima mmoja anasema, “You’re for an audience
of one: GOD ” akimaanisha, “Tunaishi kwa ajili ya kusanyiko la mtazamaji
mmoja; MUNGU.” Tunapaswa kulenga kumpendeza yeye na kumtukuza yeye peke yake
ambaye kwa nyakati zote hutuona.
Ikiwa
kusanyiko unalolenga kulipendeza ni la watu, basi uwe na hakika mwenendo wako
utakuwa mbaya katika nyakati ambazo hawakuoni, na ikiwa unalenga kumpendeza
Mungu mwenendo wako utakuwa safi nyakati zote. Mungu akiwa ndio kusanyiko lako,
basi utaishi vema maana yeye anapatikana mahali kote, si uwanjani wala ukumbini
tu; bali yuko nasi gizani na nuruni, asubuhi, mchana jioni hata usiku.
Kitendo
cha Adam na Eva (kabla ya anguko) kuishi bila nguo, tena bila ya kuona aibu
kilikuwa ni alama ya uaminifu na hali ya kuwa bila hatia mbele za Mungu.
Hawakuwa na kitu cha kuficha mbele za Mungu, hawakusongwa na jambo lolote
ambalo lingewafanya waone aibu mbele za Mungu. Mwanzo 2:25
Kundi
kubwa leo tumekuwa na sura tatu, ile ambayo jamii inaijua, ile ambayo sisi na
Mungu tunaijua, na ile ambayo Mungu peke yake huijua. Ni muhimu kuwa na sura
moja isiyobadilika, ni vema kutokuwa vuguvugu tena ni muhimu kukataa unafiki
ambao tafrisiri yake rahisi ni kuwa na sura nyingi (many faces).
Mtu
mmoja alisifika sana ofisini ilhali nyumbani kwake hawakuwa na furaha naye
kabisa, alikuwa mwema kwa watu wasio wake na aliwatesa walio wake. Sura yake ya
nyumbani ilikuwa tofauti na u-malaika aliouonesha ofisini. Ni msemo wa kutisha
na usiotakiwa, “saint at abroad and devil
at home.” Yaani, “Mtakatifu akiwa mbali, shetani nyumbani.” Ni muhimu
kutafuta sura moja, nyumbani na ugenini, usiku na mchana, chumbani na nje ya
chumba.
Dhambi
zote hutendeka mbele ya macho ya Mungu. Tafakari hili neno, mbele ya macho
yake. Kila dhambi tutendayo tunamkosea Mungu peke yake. Maumivu ya dhambi
humwelekea Mungu ndio maana kuna nyakati hushindwa kuvumilia. Usije fikiri hata
mara moja kwamba, unajikosea au unamkosea jirani, mara nyingi tunapokosa
tunamkosea Mungu. Unapomtendea jirani yako uovu unamtendea Mungu. Inatisha
kwani mabaya yote hutendeka mbele ya macho yake.
Tafakari na kuchukua hatua, Mungu yuko tayari kusamehe nyakati zote.
0 comments :