Kuanzia viongozi .......

9:15:00 AM Unknown 0 Comments

KUANZIA VIONGOZI HADI WAFUASI WAO
(Sote tunamuhitaji Yesu)
Sote tunamuhitaji Yesu kuanzia viongozi wa dini kama Papa Francis mpaka Viongozi wa siasa kama Barack Obama sote kwa ujumla tunamuhitaji mwokozi. Hakuna wokovu kwa mtu awaye yote ila kwa Yesu Kristo tu. Nukuu za Alexender The Great ni simulizi zenye mafunzo tele. Kuna nyakati alinukuliwa akisema, “Nitakapokufa nataka jeneza langu libebwe na madaktari bingwa, waweke mikono yao juu ya jeneza langu ili watu wajue wazi kwamba kuna nyakati, hata madaktari wazuri hawataweza kuokoa maisha.”
Madaktari bingwa wanaposhindwa wanamfanya mwanadamu akumbuke kwamba, hakuna uzima kwa mtu awaye yote isipokuwa kwa Yesu Kristo. Bill Graham anasema, “Hata wanasayansi wasiomjua Mungu wala kumkiri wakishaugua saratani (cancer) huanza kukiri na kusema Mungu nisaidie”. Biblia inamfananisha mwandamu na ua ambalo leo lipo na kesho halipo tena. Hakuna la kudumu ndani ya mwanadamu.
Nje ya Yesu Kristo mwanadamu ni kama kivuli punde hayupo tena. Mwandamu anapata uzima ndani ya Kristo na si uzima tu unaokomeshwa na kifo bali uzima ulio juu ya kifo. Kifo hakiwezi kukomesha maisha ya mtu amwaminiye Kristo Yesu. Iko wazi katika 1Kor 15:55-56 Yesu Kristo alishinda kifo kwa ajili yetu hata ikaandikwa, Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako? 56 Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati.
Mauti imeshindwa, mauti imechoka na uzima wa Yesu Kristo umetawala tena. Mauti ilipata nguvu kupitia dhambi naye Yesu Kristo alipokwisha kutusamehe dhambi zetu basi aliivunja ile nguvu ya mauti. Ndio maana watu wengi waliokuwa karibu na kufa alipowaambia wamesamehewa dhambi waliponywa, maana nguvu ya mauti ni dhambi, dhambi ikiondolewa mauti hukosa nguvu. Wamwaminio hawaogopi kifo.
Je, unahisi kufa? Je, unaogopa kifo? Nguvu ya uhai inakuja kupitia msamaha. Wale wenye hakika kwamba, Mungu amewasamehe dhambi zao kamwe hawaogopi kifo. Biblia inasema, “anaraha aliyesamehewa dhambi”, kwa lugha nyingine anafuraha aliyesamehewa dhambi. Waliosamehewa dhambi wamebarikiwa tena biblia inasema wanayo heri. Zaburi 32:1-2
Yesu aliishinda mauti kwa kupitia kuishinda dhambi. Na hakuna mwandamu awaye yote aliyeishinda dhambi na kuiharibu pale msalabani isipokuwa Yesu Kristo peke yake. Madaktari, walimu, viongozi wa siasa, viongozi wa dini hawakuweza na hawataweza ni Yesu peke yake. Mhimili (mzizi) wa kifo ni dhambi, unapotubu unafukuza mauti na hofu zake.
Tumaini la uhai na uzima wetu ni Kristo peke yake. Kama tungelikuwa na uzima Yesu asingelikuja. Kama tungelikuwa wema asingekuja pia. Kwa hiyo amekuja kwa sababu tulikuwa wafu kwa dhambi, watupu kwa uovu wetu na wachafu kwa matendo yetu.
Mwimbaji mmoja anasema, “All I need is you” ni kweli tunamuhitaji Yesu peke yake. Tunamuhitaji kila saa na kila wakati. Ni vema tusogelee mahali anapokaa. Twende kitini pake kwa toba. Imeandikwa, “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. ” Waebrania 4:16
Yesu anapatikana katika kiti cha rehema na biblia inasema, “wakati wa mahitaji”. Je! ni wakati gani huo tunaohitaji neema na rehema? Ni kila saa na kila dakika. Mara kadhaa asubuhi nimekuwa nikipiga magoti na kuomba neema ya siku husika, kwa kuwa najua ninahitaji neema kila siku. Najua namuhitaji Yesu kwa uhai wangu.
Siku ukitenda dhambi unahitaji neema, na siku usipotenda dhambi unahitaji neema pia. Na kama tunahitaji neema kila siku na kila saa basi moja kwa moja tunamuhitaji Yesu kila siku na kila saa. Yeye ndiye mtoaji wa neema hizo. Pata muda wa kuomba sote tunahitaji neema...tukutane wiki ijayo mpendwa. Barikiwa

0 comments :

Rafiki yako ni nani?

4:04:00 PM Unknown 0 Comments

RAFIKI YAKO NI NANI?
[Aina ya marafiki ni dalili ya hatima yako] 
Rafiki ni mtu ambaye mna vitu au mwelekeo unaofanana. Rafiki ni Yule ambaye mna mwelekeo wa pamoja katika imani, biashara au kazi. Rafiki ni yule umpendaye na ungependa kuwa na muda mwingi pamoja naye.
Unaweza kufanya urafiki na mtu, na cheo chake, na kitu au vitu. Urafiki na Kaizari ni urafiki na cheo ili upate manufaa  fulani, urafiki wa Yesu na Lazaro ni mfano wa urafiki kati ya watu na upendo kati ya Yuda Iskariote na pesa ni mfano wa watu ambao wako tayari kuwa peke yao ilmradi wawe na pesa.
Kuna nyimbo rafiki tunazozipenda ambazo mara nyingi tunazisikiliza, halikadhalika kuna video rafiki, kipindi cha televisheni rafiki na hata kaseti ya redio rafiki. Tuna kitabu rafiki tena kuna majarida na magazeti rafiki. Ukifanya urafiki na mpumbavu lazima uumie, nyimbo za kipumbavu zinaumiza mioyo, zinaondoa usafi wa moyo kwakuleta mawazo machafu. Biblia inasema, “Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.” Mithali 13:20
Kuna nyimbo za kipumbavu ambazo ukifanyo nazo urafiki lazima uumie, kuna video za kipumbavu, kuna vipindi vya redio vya kipumbavu halikadhalika kuna majarida na vitabu vya kipumbavu. Kuna magazeti ya kipumbavu [udaku] rafiki wa hayo lazima aumie. Moyo wake hautakuwa safi, utawaza uchafu wa picha ya mbele ya magazeti hayo. Msisitizo wangu uko hapa: Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.” Mithali 13:20b
Nimejikataza kuendelea kuitazama vitu kwenye “you tube” kwani picha za matangazo na picha chafu zinazowekwa makusudi zimekuwa kama mtego kwangu. Kuliko kumkosea Mungu kila siku ni bora nisiingie kabisa. Kila mtu ana eneo lake analojaribiwa kwalo, wengine ni urafiki na magazeti, wengine mitandaoni, wengine mavazi na wengine mazungumzo mabaya. Wengine hujaribiwa kwa kutaka kuvutia au kupendwa na watu, hawa huweka picha za mtego wakitegemea aonaye awape, “like” au awakubali.
Rafiki ni yule anayezungumza nawe, magazeti, vitabu, majarida na picha huzungumza nasi. Lengo la mwandishi ni kuona msomajia ua mtazamaji anapata ujumbe kusudiwa. Mara nyingi huwa sitazami wala kusikia nyimbo za kidunia [kipumbavu] lakini huwa inanilazimu nikiwa safarini. Nyimbo hizo hupigwa ndani ya basi na madhara yake ni hasi. Huwa nasafiri nikiwa na vitabu na majarida mazuri ya kusoma lakini bado kwa masaa kumi na nne au kumi ya safari nyimbo za kipumbavu huleta kero na uchafuzi wa moyo. Kama watu watapata ajali huku wakitazama nyimbo chafu basi mioyo yao itakuwa katika hali mbaya.
Tunaweza kujaribiwa kwa kuwa na makundi yenye mazungumzo mabaya lakini kwa kuwa na tabia ya kuchagua vitu vinachochea tamaa mbaya. Ni muda mzuri leo wa kuamua kuacha kabisa urafiki na kipindi kichafu cha redio au televisheni, ni muda mzuri wa kuvunja urafiki mbaya. Rafiki mpumbavu atafanya uangamie, napenda tafsiri hii: “The companion of fools will suffer harm
Mfano mzuri wa madhara yanayompata rafiki wa mpumbavu ni yale ya nchi ya Japani iliyoyapata kutoka Marekani kufuatia urafiki wao na Hiltrer wa Ujerumani. Japani walifanya urafiki na Ujerumani kwa kusaini mkataba wa ulinzi na usalama wa mwaka 1940 matokeo yake mbeleni walivamia kisiwa kimoja nchini marekani na kuambulia kupigwa mabomu ambayo mpaka sasa wanayaonja madhara yake. Yote hayo ni kwa sababu ya rafiki mpumbavu. Nakushauri achana naye na kesho yako itakuwa njema.

0 comments :

Kanunu ya Mazingira

3:53:00 PM Unknown 0 Comments


KANUNI YA MAZINGIRA
(Vigezo lazima vikamilike)

Ili mbegu iweze kuota ni lazima vigezo vinavyohusika vikamilike. Uoteshaji wa mbegu hauhitaji maombi tena haufanyiki kwa mafungo bali kwa kutimiza vigezo vinavyotakiwa katika kanuni ya mazingira. Ili mbegu ikue inahitaji yafuatayo: maji, mwanga, joto na hewa. Mambo haya yakitimia hata kama mkulima ni mweusi mbegu itaota na hata kama ni mweupe mbegu itaota. Ukitii na kutimiza vigezo mafanikio ni lazima.

Kuna watu ili wafanikiwe wanahitaji mazingira ya kanisani, wengine mazingira ya biashara wengine mazingira ya shuleni na wengine viwandani. Yule wa kanisani hawezi kuwika sokoni halikadhalika wa sokoni hawezi kuwika kanisani. Ni muhimu kila mtu ajue mazingira yanayobeba kipaji chake. Mito na bahari ndiyo inayobeba kipaji cha samaki cha kuogelea.

Unadhani mazingira gani yanaweza kubeba kipaji chako? Je, ni katika mazingira gani watu wanauona uwepo wako?  Je, ni katika tasnia gani unapata utoshelevu wa mahitaji yako? Ni katika mazingira gani Mungu anatukuzwa kwa ajili yako na wewe unatakaswa?

Nimewahi kusoma makala moja isemayo, tasnia ya filamu imeajiri watu wengi nchini Nigeria kuliko mafuta. Ingawa Nigeria wanasifika kwa kutoa mafuta lakini ni mazingira ya filamu ndiyo yamewaajiri watu wengi zaidi. Ni bora kupingwa na watu wengi katika mazingira sahihi kuliko kukubaliwa na watu wote katika mazingira ambayo si sahihi kwa ukuaji na ustawi wako.

Bora upinzani wa jinamizi la usiku kuliko ule wa mazingira yaani, unaamka mapema kwenda kufanya kitu usichopenda. Unawahi kuamka kwende katika mazingira usiyoyataka. Kama umeitwa katika mazingira ya michezo basi siasa haikufai. Ni raha sana mtu anapokuwa katika mazingira sahihi, Christiano Ronaldo anasema yuko tayari kucheza soka hata bila ya kulipwa. Anaupenda mpira wa miguu, yuko radhi kucheza bure mpira ni maisha yake. Usain Bolt angeendelea kung’ang’ana na mpira wa miguu huenda asingekuwa chochote, lakini utii wake kwa kanuni ya mazingira ulimpeleka kwenye riadha ambapo anashikilia rekodi ya dunia.

Mwenye hekima mmoja amewahi kusema: “There are no bad people there are misplaced people”.  Hakuna watu wabaya ila kuna watu ambao wapo katika mazingira ambayo si sahihi kwao. Mazingira mabaya si yale yasiyo na pesa bali ni yale ambayo hayakusaidii kufikia ndoto zako na kuwa unachotaka kuwa. Mazingira yanapaswa kukubeba kwa sababu kwa asili mtu hawezi kubeba mazingira. Kuyabeba mazingira ni kazi ngumu. Ndio maana

Rai yangu kwako leo ni kukusihi utii kanuni ya mazingira na kwenda kwenye eneo lako husika. Wahubiri wengi wamekuwa na simulizi za kuacha kazi na kwenda kwenye wito wao, jambo hilo si mtindo bali ni kanunu ya msingi ya mazingira.

Nenda shule, nenda kwenye biashara, nenda kanisani, nenda kwenye huduma, nenda kwa watoto, nenda kwa yatima nenda kwa watu ambao umeitiwa. Wengine wameitwa katika mazingira ya ujasiliamali wengine wameitwa katika mazingira ya uongozi. Sote tunapaswa kuyatafuta mazingira yetu na kuyatii. Petro alicha mazingira ya baharini [uvuvi] na akaenda katika mazingira yenye watu wengi [kwenye uinjilishaji na utumishi] huko akafanikiwa sana.

Tii mazingira yako, ipende kanuni ya mazingira….

0 comments :

Ishi Maisha Yako

9:35:00 AM Unknown 0 Comments

ISHI MAISHA YAKO
(Shughuli hii inakuhusu wewe sisi tumekuja kukusaidia) 
Ziko namna mbalimbali za kuishi, lakini namna bora ya kuishi ni ile itokayo kwa Mungu na inayoelezwa katika neno lake yaani, katika biblia. Ukiishi nje ya maisha yanayopendekezwa na Biblia maana yake unaishi nje ya mpango wa Mungu.
Mtu anaweza kufa kwa niaba yako lakini hawezi kuzaliwa kwa niaba yako. Mungu hawezi kuruhusu ofisi yako ya maisha ikaimishwe ndio maana hawezi mtu kuzaliwa kwa niaba ya mwingine. Ni lazima uishi maisha yako. Ngoma ya maisha inakuhusu wewe ni lazima uicheze. Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende.”Ezra 10:4
Maneno, “inuka”  “wewe”  “ukaitende” yanaonesha waziwazi kwamba, hakuna kukwepa. Watu watalia kwa sababu mhusika unalia, watu watufurahi kwa sababu mhusika unatabasamu bashasha. Ndivyo anavyonena Robert Frost mshairi mwenye alama ya aina yake: “No tears in the Writer, No tears in the reader. No surprise in the writer, No surprise in the reader”.
Kila unayemwona kwenye maisha yako yupo ili kukusaidia na si kufanya kwa niaba yako. Yupo kutoa msaada ili wewe ufanye. Marafiki hawataweza kufanya sehemu yako hata ukiwaita watalala, watalala kwa sababa kazi inakuhusu wewe. Yesu alishuhudia wanafunzi wake wakilala licha ya kuwataka waamke kuomba. Ni kwa sababu sherehe ya wokovu ilimhusu Yesu Kristo.
Mambo yanaweza kufanyika bila pesa lakini si bila ya wewe. Mhusika mkuu wa maisha yako ni wewe. Wazazi, marafiki na jamaa hawana ruhusa ya kukubadili badala yake wanatakiwa kukusaidia wewe kuwa wewe halisi. Mariamu mama yake Yesu hakuwa kikwazo kwa huduma ya ukombozi badala yake aliacha Yesu Kristo awe Yesu Kristo kweli kweli.
Familia inaweza kuwa kitalu kizuri cha kukuzia maono na ndoto zako lakini pia inaweza ikawa kamba nzuri ya kunyongea ndoto zako. Ninaposema familia sina maana ya ndugu wa damu tu, bali ninawahusisha wote wanakuzunguka na unaoshirikiana nao. Watu ambao unatumia muda mwingi pamoja nao. Uwe mwangalifu uwapo katikati yao!
Je, ukiondoa shinikizo la wazazi, ungependa kuwa nani? UKiondoa mambo ya umasikini ungesomea nini? Je, ukiondoa shinikizo la mgandamizo wa uchumi ungependa kufanya kazi gani? Je, ukiondoa hofu zako ungependa kuanzisha nini? Hayo ambayo ungeyafanya isipokuwa umezuiliwa kwa sababu ya ukosefu wa pesa, shinikizo la wazazi na umasikini hakikisha unayafanya.
Mgombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi wa sasa nchini Marekani Donald Trump ameandika hivi katika moja ya vitabu vyake, “Its crucial to be true to yourself true to your own choices” yaani, “Ni muhimu sana kuwa muwazi na mkweli kwako binafsi na katika chaguzi zako.” Trump anataka tuwe wazi kwa nafsi zetu, tusiidanganye mioyo yetu. Uwe muwazi, fanya upendacho ili uwe unachotaka. Mimi ninapenda kuhubiri habari za Yesu, tazama! hata sasa ninamhubiri.
 Zawadi ya kwanza ambayo tunaipata toka kwa Mungu ni zawadi ya uhai. Ni zawadi ambayo ni ya pekee sana ambayo ni zawadi binafsi. Mungu ametupa uhai ili tuishi kwa ajili yake, tufanye aliyotupangia hata kama wengine hawatayakubali. Mimi pia nimekuja kukusaidia, kwa heri mpaka wiki ijayo, Shallom….

0 comments :