Kwa kila ambaye....... I
KWA KILA AMBAYE HAJAOA AU KUOLEWA - I
(Amua kuwa na familia ya aina hii)
Ni rahisi sana mtu kuwa na ndoto za kumilika gari, nyumba
nzuri, kufika mbali kitaalamu na hata kiuchumi. Ni nadra sana kwa vijana wa leo
kuwaza kuwa na familia takatifu, ukimpata anayewaza hivyo ni kwa wale wachache
wa mazingira ya kanisani. Wengi wanatamani kuwa na familia za kitajiri.
Hakuna shirika la kupima viwango au ubora wa familia,
lakini naamini neno la Mungu linaweka kiwango. Kwa dunia ya leo familia bora
inapimwa kwa msingi wa kipato, ambao kiuhalisia si msingi imara. Biblia
inapozungumza kuhusu mwanamke mpumbavu au mwanaume mpumbavu inaoensha umuhimu
wa hekima na maarifa ya kimungu kama msingi imara katika familia. Baba hapaswi
tu kuwa na uwezo wa kutafuta na kupeleka mkate nyumbani (breadwinner) bali awe
pia na uwezo wa kumpeleka Yesu nyumbani.
Katika maandiko yako maeneo mengi ambayo familia
zimetajwa. Lakini kwa kusudi la soma hili naomba tujifunze kwa familia ya
Kornelio Yule wa kwenye kitabu cha matendo ya mitume. Huyu ndiye kielezo cha
familia bora. Ambayo kwa mtazamo wangu mimi, familia bora ni ile inayokula
mkate wa kimwili na wa kiroho (neno) pia ni ile inayoshiriki katika kuwapa watu
wengine mkate wa kimwili na wa kiroho. Kila kijana awe na ndoto (dream family) ya
kuwa na familia ya namna hii: “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio,
akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye
na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na
kumwomba Mungu daima.” Matendo ya Mitume 10:1-2
Si Kornelio peke yake, bali hata watoto na mke wake
walikuwa watoaji, watauwa na wachaji wa Mungu, ndio maana ikaandikwa yeye na
nyumba yake yote. Huyu mtu na familia yake wanafaa kuigwa. Maandiko yamemweka
makusudi ili tujifunze kitu.
Hakuna familia ambayo yenyewe peke yake imekamilika.
Usiwaze kuishi kwa mfumo wa kujifungia na familia yako (closed system). Mungu
anajua baba na mama hawatoshi, ndio maana akaleta kitu kinachoitwa kanisa.
Lengo ni kwamba, yale mazuri yasiyopatikana nyumbani basi yakapatikana katika
mwili wa Kristo yaani kanisani. Katika kanisa kuna mitume, manabii, walimu,
wachungaji na wainjilisti. Usipange kukosa hekima zao. Wako ili kuwakamilisha
watakatifu.
Mtandao umefanya kanisa kwa maana ya mwili wa Kristo kuwa
pana zaidi. Vitabu na majarida vinarahisisha mawasiliano katika mwili wa
Kristo. Leo hii unawaza ukawa na baba au kaka wa kiroho ambaye hamjawahi
kuonana naye ana kwa ana. Mwili wa Kristo ni mpana, hakuna sababu ya kumchukia
mtu wa kanisa lingine au wa dhehebu lingine sote tuko pamoja katika mwili
mmoja.
Jaribu kufikiri ni mangapi ungekosa kama ungejifunza
katika familia yako tu? Je, ni mangapi mazuri ungeyakosa kama ungejifungia
kanisani kwenu tu? Leo ninakuletea familia ya Kornelio na naomba ujifunze toka
kwao. Kwa Yule rafiki ambaye hajaolewa basi unanafasi bado, jipange na fikiria
kuwa na familia nzuri kama ya kornelio. Familia ya sala siku zote, maombi siku
zote, sadaka siku zote.
Wiki ijayo nitaendelea kuzungumzia mambo ya kuzingatia
katika hutua za awali kuelekea kuoa au kuolewa.
Maisha ya Kornelio ni alama (legacy) na wewe unayo nafasi ya kuacha
alama anza sasa kunuia kuacha alama katika familia na jamii yako.
0 comments :