ULIMWENGU MKAMILIFU
“Imagine a world without a loser, a
world without a purposeless person”
Dunia
kamilifu inategemea sana ukamilifu wa mwanadamu. Kwa asili mwanadamu ni
mkamilifu na mwenyehaki. Hebu jaribu kufikiri kwamba ulimwengu ungekuwa mkamilifu
ungependeza namna gani; hata hivyo ukamilifu wake unategemea wanadamu. “Basi ninyi
mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”Mathayo
5:48
Katika
ulimwengu mkamilifu hakuna askari polisi wala askari magereza, katika ulimwengu
mkamilifu hakuna chuki wala mapigano watu hukaa kwa amani. Amani yao huja kwa
sababu kila mtu anafanya anachopenda na alichotumwa na Mungu kukifanya hapa
duniani. Kama Yohana mbatizaji alivyotoka kwa Mungu na kuja duniani, ndivyo
kila mmoja wetu pia alivyotoka mbinguni ili kuja kutekeleza wajibu wake hapa
duniani. “Palitokea mtu,
ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa
yeye.”Yohana 1:6-7
“Tukiwa na watu wakamilifu yaani, watendao kwa ukamilifu tunaweza kuwa na ulimwengu mkamilifu ”
Kwa
kupitia msalaba wa Yesu Kristo ukamilifu umewezekana. Lengo la Mungu ni sisi
sote turejee Mwanzo sura ya kwanza ambapo mwanadamu ameonekana katika ukamilifu
wake. Ni muhimu kuwa na picha ya
ulimwengu wa watu wakamilifu hata kama ulimwengu huo utahusisha watu watatu tu. Mungu ametuumba wanadamu tukiwa
wakamilifu, ni katika mwanzo sura ya tatu ndipo Adamu na Eva walipopoteza
ukamilifu wao. Ni wakati huo ndipo Chuki, usaliti, uchoyo na mauti vilipata
nafasi katika maisha ya mwanadamu na ukamilifu ukapotea. Kwa upendo Mungu
aliendelea kumtafuta mwanadamu tena ili kumrejesha katika ukamilifu aliokuwa
nao mwanzoni.
Tukiwa na watu wakamilifu yaani,
watendao kwa ukamilifu tunaweza kuwa na ulimwengu mkamilifu. Ni
rahisi mtu kutenda kwa ukamilifu na kwa upendo ikiwa tu mtu atafanya
anachopenda kufanya. Kama kila mtu atafanya kazi aipendayo (aliyoitwa na Mungu
kuifanya), tena kama kila mmoja wetu atamruhusu Mungu atende ndani yake basi
tutashuhudia ulimwengu mkamilifu. Mwanadamu huweza hutenda kwa ukamilifu kwa
sababu ni Mungu ambaye hutenda ndani yake. “
“Ukijenge maisha yako katika eneo ambalo Mungu atatenda kazi ndani yako basi utakuwa mtu mkamilifu”
Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu
Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema,
mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake,
kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina.”
Waebrania 13:20-21
Ukijenge
maisha yako katika eneo ambalo Mungu atatenda kazi ndani yako basi utakuwa mtu
mkamilifu. Inawezekana ni katika kuwalisha masikini, huenda ni katika siasa, au
katika kufundisha, lakini liko eneo ambalo Mungu atatenda pamoja nawe. Na
huenda hata sasa anatenda kazi pamoja nawe pasipo wewe kujua. Uzuri wa kusudi
ni kwamba si wewe utendaye, bali ni Mungu ndani yako. “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka
kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.”Filipi
2:13
Palipo
na furaha ya kweli pana ukamilifu wote, ndio maana imenenwa “furahini katika
BWANA.” Kuna furaha ya ajabu katika kutii mapenzi ya Mungu, kila mtoto wa Mungu
mtiifu anajua jambo hili. Lazima
ujiulize ni wakati gani katika kutenda kwako umekuwa mwenye furaha sana.
Ukipata jawabu basi jenga maisha yako kuzunguka jambo hilo. Binafsi napenda
kuhubiri habari za Mungu na ninakaza mwendo ili kujenga maisha yangu katika
jambo hili moja; napenda mtu wa jambo moja.
Ukamilifu
huenda pamoja na uaminifu. Hizi mbili hazitofautiani kamwe. Hakuna mtu mkamilifu asiye mwaminifu. Nimewahi kumtazama mwezeshaji
mmoja akiwahoji watu kuhusu uaminifu wao katika saa za kazi. Aliwauliza, “Katika
saa kumi na mbili za kazi ni saa ngapi wanakuwepo ofisini kimwili, kiakili na
kimawazo?” Aliyesema saa nyingi ni tatu yaani katika saa 12 ni kwa muda wa saa
tatu tu ndio akili yake huwa pale kwa asilimia 100%. Wengine walisema saa moja
kati ya 12 na wengine saa mbili kati ya 12. Hakuna ambaye anakuwepo pale
kiakili kwa muda wote wa saa 12, lakini kimwili wanakuwepo. Huu pia si
uaminifu. Hii ni shida itokanayo na kufanya kazi usiyoipenda.
Ukamilifu
unachagizwa sana na mwanadamu ambaye anafanya apendacho alichoumbwa kukifanya.
Unamkumbuka Yona aliyekuwa na mawazo ya Ninawi ilhali anaelekea Tarshishi ili
kujiepusha na uso wa Mungu. Wako maaskari ambao wameshika bunduki badala ya
Biblia Takatifu, wanaenda lindo ilhali walipaswa kwenda katika mkesha.
Wanafanya wasichokipenda na hivyo hawapati furaha ya kweli. Wako vijana
wanaoishi nje ya kusudi la kuumbwa kwao, wako wahandisi hata waashi ambao
wamepishana na wito wao.
Ni
muhimu kila mtu ajue alichoitiwa, akipokee na kukiheshimu. Ni lazima kila mtu
atambue upekee wake katika sayari hii. Ni sayari ambayo kila mtu ni halisi wala
si nakala ya mwingine. Dunia yetu ingekuwa nzuri mno kama kila mtu angekitumia
kipawa au kipaji chake kwa upendo. Kila mtu angefanya kazi kwa utulivu na amani
angestawi.
Hakuna
amani katika nchi ya watu wasiotimiza waliyoitiwa na Mungu. Ni hatari kukaa na
mtu asiyeenda katika kazi aliyoagizwa na Mungu. Watu waliosafiri na Yona
walitaka kufa kwa sababu Yona alikataa kwenda katika maagizo ya Mungu. Watu
waliosafiri na Paulo waliokoka kwa sababu Paulo amekwenda katika maagizo ya
Mungu.
Kama
hatuendi katika makusudi ya kuumbwa kwetu basi kufa kabla ya wakati “pre mature
death” si ajali. Hatua muhimu katika kuibadili hatima yako ni kubadilisha
kwanza mwelekeo wako. Yona alibadilisha mwelekeo wake kwa kutubu akiwa ndani ya
tumbo la samaki na baadaye akaenda Ninawi kama alivyoagizwa.
Inawezekana
haukitendei haki kipaji chako, hauishi kusudi la Mungu wala haunendi kwa kadiri
ya wito wako ni muda mzuri leo wa kufanya mabadiliko. Chukua uamuzi anza kuishi
sawasawa na kusudi la Mungu katika maisha yako leo. Ama uteseke kwa kuanza
upya, au ufe katika eneo ambalo Mungu hakutaka kabisa udumu hapo. Nje ya wito
hakuna ukamilifu, ni sawasawa na samaki nje ya maji.
“Mtu anayefikiri kuhusu sababu, kwanini hawezi kufikia malengo makuu katika maisha yake, hutumia nguvu ile ile katika kufikiri, sawa na mtu anayefikiri kuhusu namna [njia] ya kufikia malengo hayo; yamkini huyu wa pili hutumia nguvu kidogo”
Kila
mtu huwa na sababu nyingi sana za kumzuia kwenda katika kusudi la Mungu.
Uchungu wa kutokwenda ni majuto na maisha ya yasiyo na furaha ya kweli, uchungu
wa kwenda ni changamoto. Kila mtu anayo sababu yake inayomdanganya ili asifikie
malengo makuu, mwingine atasema
umasikini, mwingine ugonjwa, mwingine ulemavu, mwingine familia aliyotokea,
mwingine elimu ndogo.
Kumbuka,
Sababu 1000 za kutokwenda au kutokufanya kusudi la Mungu hazina mashiko
ukilinganisha na ile moja itokayo kwa Mungu inayokuhimiza kuyatendea kazi makusudi
ya kuumbwa kwako. Mtu anayefikiri kuhusu sababu, kwanini hawezi kufikia malengo
makuu katika maisha yake, hutumia nguvu ile ile katika kufikiri, sawa na mtu
anayefikiri kuhusu namna [njia] ya kufikia malengo hayo; yamkini huyu wa pili
hutumia nguvu kidogo.
“If you really want to do something you’ll find a way. If you don’t.
You’ll find an excuse” Jim Rohn
0 comments :