Acha Kujipima Kimwili

8:28:00 PM Unknown 0 Comments


ACHA KUJIPIMA KIMWILI

Unaweza kuwa na urafiki hai na Yesu na bado ukawa masikini wa mali na fedha wala si ajabu, unaweza kuugua na bado ukawa na urafiki mzuri na Yesu. Lazaro alikuwa masikini na alikuwa mgonjwa lakini bado urafiki wake na Yesu ulikuwa hai. Kamwe vitu na hali ya afya au fedha si jawabu la mwisho la kuonyesha uhusiano wa mtu na Mungu, Yohana 11:2. Pastor Chris Oyakhilome anaandika katika utenzi wake, “jambo muhimu kabisa katika maisha haya si umiliki wa mali, bali ni kugundua kusudi la Mungu na kulitimiza”.  Maisha hayahusu milki za mali, unaweza ukawa unamiliki kila kitu hapa duniani na bado isikufaidie chochote. Yesu Alishasema, “…maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyonavyo.” Luka 12:15
Unapompokea Yesu unapokea kwanza mambo ya msingi na ya lazima kama vile: uzima wa milele, Roho wake mwema, imani ya kweli, uponyaji na unafanyika makao yake. Haupokei aina mbalimbali za magari Toyota Carina, Vos wagon wala Isuzu, haya hata yakija huitwa ziada, cha msingi uzima wa milele. Vitu ni vitu na mtu ni mtu. Kamwe uzima wa mtu haumo katika mali au alama za juu katika tasnia fulani, bali umo ndani ya Kristo Yesu. Hata upewe ulimwengu mzima ni bure kabisa kama hautaweza kudumu katika kusudi la Mungu. Nafsi yako haiwezi kununuliwa na jumla ya utajiri wote wa dunia hii. “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Marko 8:36

Shabaha ya shetani ni kuwaona watu wakimlaani na kumlaumu Mungu wao, kwani adui anajua wazi Mungu hapendi kulaumiwa. Mafanikio ya kiroho hayapimwi kwa alama za juu darasani, nyumba gari au fedha nyingi. Baraka ni muhimu ila si kipimo sahihi. Kujipima kimwili ni sababu kubwa inayofanya watu wa kiroho wamlaumu Mungu na kujuta.

Ukikwepa kusudi la Mungu baadaye utajiona huna faida, hautaacha kulaumu kwa kuwa mazingira yatakuwa kinyume na wewe. Utaona umekuja duniani kama mtalii tu, wala hakuna ulichokamilisha. Mtu hana faida nje ya wito na kusudi aliloitiwa na Mungu. Maneno ya Solomoni kwamba, “mtu ana faida gani ya kazi yake…” yanafanana na yale ya nabii Malaki, “Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida;” haya ni maneno ya watu waliosahau kusudi la Mungu, na kujikuta wakipenda dini, mali, wake zao, serikali, vitu, marafiki au watoto kuliko kusudi la Mungu.

Nilijifunza mahali fulani kwamba watu wa ki-dunia huutafuta mkono wa Mungu (vitu) lakini sisi tunautafuta uso wa Mungu (uwepo). Ukiwa mtu wa kiroho jipime kiroho. Usijipime kwa kuangalia jinsi waovu au wasio mtii Mungu wanavyofanikiwa. Cha msingi angalie kama unalitendea kazi kusudi la Mungu kukuumba wewe.

Ukipenda kujilinganisha na watu na vitu matokeo utakayopata ni kuona utumishi wako hauna faida. Utaona kumtumikia Mungu hakuna faida, na matokeo yake ni kuleta laana katika maisha yako. Mungu anajua kila amtumikiaye anapata faida ndio maana hapendi watu wake waseme hakuna faida katika utumishi.

"Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani? Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi? Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.” Malaki 3:13-18

Hatupaswi kujipima kimwili bali na tujipime kiroho kwa kuzingatia kusudi la kuumbwa kwetu. Unaweza ukawa na fedha nyingi, cheo kikubwa, mavazi mazuri na mke mzuri, lakini kama hujatumikia kusudi la Mungu katika hayo basi ulichofanya ni bure tena ni sawa na kufukuza upepo. "Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua?” Mhubiri 1:2-3



0 comments :