Jizoeze kufikiri .....

4:20:00 PM Unknown 2 Comments

JIZOEZE KUFIKIRI JUU YA MATOKEO YA MAAMUZI YAKO KABLA YA KUAMUA (Zaburi 119:9)
Jambo kuu linaloleta majuto katika maisha ya watu wengi ni kukosea katika kufanya maamuzi; hasa kwenye mambo muhimu ya maisha yao. Mara kadhaa tumesikia watu wakijilaumu, “Ningejua nisingefanya nilichofanya au nisingeamua jinsi nilivyoamua”; watu hawa wanajutia matokeo ya maamuzi yao. Kama wangetambua matokeo ya maamuzi yao kabla ya kufanya maamuzi au wangepewa nafasi ya kuamua tena bila shaka wangeamua tofauti na walivyoamua hapo awali.
Hakika majuto ni mjukuu kama ulivyo msemo huu ambao umezoeleka katika masikio ya wengi. Ukweli ni kwamba katika maisha hakuna anayependa kukosea katika kufanya maamuzi hasa katika mambo muhimu yanayogusa maisha yake au maisha ya watu wake wa karibu. Mungu amekusudia kila mtu kuishi maisha yenye ufanisi na furaha; si mpango wa Mungu ukosee katika kuamua na kuishia katika majuto.
Njia mojawapo ya kukusaidia kufanya maamuzi vizuri, ni kwa kujizoeza kufikiri juu ya matokeo ya mwisho ya uamuzi wako kabla ya kuamua. Kuwa na picha ya mwisho ya matokeo ya uamuzi huo. Kuangalia kwa makini aina ya matokeo na endapo pia utakuwa tayari kuishi na matokeo ya maamuzi unayotaka kuyafanya.  Mfano; Ikiwa unajua kuwa mchumba wako sio mwaminifu au ana hasira kupita kiasi na unataka kufunga naye ndoa hapo baadaye, usiangalie kwanza kama unampenda au la, kwanza angalia na kufikiri endapo utakuwa tayari kuishi na matokeo ya yeye kutokuwa mwaminifu au kuwa na hasira kupita kiasi; kabla ya kufikiria kwamba atabadilika mkishafunga ndoa; kwa sababu kama hataki kubadilika mkiwa wachumba au marafiki, una uhakika gani atabadilika mkiwa familia?.
Matokeo mengi ya uamuzi na uchaguzi wako ni matokeo ya kudumu (permanent), ndio maana iko haja ya kuwa mwangalifu. Unaweza kuishi maisha yote bila amani, na hii ndio picha ya matokeo ya kudumu. Kama huridhishwi na matokeo ya baadae ni vizuri usiamue kwanza. Unaweza ukafumba macho sasa na ukafanya maamuzi, lakini matokeo yatakapoanza kuonekana hautaweza kufumba macho tena, na mwisho wake ni kuishi maisha yenye majuto na kujilaumu. Biblia inaweka msingi wa kutusaidia hasa inapofika kwenye kuamua, hasa mambo muhimu yanayogusa maisha yetu na maisha ya watu wengine.
Ni muhimu kuongeza umakini katika miamala ya maisha yetu, kwani tunaweza kufanya kila kitu lakini hatuwezi kutengua kila tulichokifanya, [we can do everything but we cannot undo everything]. Kabla ya kuamua kufanya hiyo kazi, fikiri kwanza juu ya matokeo ya mwisho ya uamuzi wako juu ya kazi hiyo. Mara nyingi tumesikia habari za familia zilizokuwa zinaendelea vizuri mpaka pale ambapo baba au mama aliamua kufanya kazi fulani. Mtu huyu anafanikiwa ofisini au kazini lakini kwa gharama ya familia yake au gharama ya roho yake. Au mwingine anafanikiwa katika biashara kwa gharama ya uhusiano wake na watu wake wa karibu. Uamuzi sahihi hauleti majuto wala kujilaumu baada ya kuamua bali hukupa amani, utulivu na ujasiri hata pale unapokutana na changamoto mbalimbali baada ya kuamua.
Biblia inashauri inapofika wakati unataka kufanya maamuzi fulani, usikimbilie katika kuamua bali uketi kwanza uhesabu gharama na kufanya shauri ili matokeo ya maamuzi hayo yawe yenye ufanisi na kukuwezesha kuishi maisha yenye furaha na ujasiri bila majuto wala kujilaumu hapo baadae. Luka 14:28-32.
Kama Adamu na Eva, wangefikiri au wangejua matokeo ya maamuzi yao ya kwenda kinyume na maagizo ya Mungu ya kutokula tunda, naamini wasingekula lile tunda. Maagizo ya kutokula tunda hayakuwekwa ili kuwaonea bali yaliwekwa ili kuwalinda wao dhidi ya mauti na uharibifu katika maisha yao. [It was for their advantage].
Hekima ni uwezo wa kujua matokeo ya maamuzi yako kabla hujaamua. Unapojua matokeo kwanza inakusaidia kujua nini unatakiwa kuamua, nini hutakiwi kuamua, lini unatakiwa kuamua na lini hutakiwi kuamua n.k! Mara nyingi tumesikia watu wakisema, tunajifunza kutokana na makosa; lakini mwenyehekima mmoja ameongeza na kusema ni vyema makosa hayo yakawa ya mtu mwingine, kwa sababu kuna baadhi ya maamuzi yakikosewa hamna nafasi ya kujifunza; Hauwezi kujifunza kama sumu ya panya inaua kwa kuionja, ile kwamba panya wanakufa wakiila hilo ni darasa tosha [1Kor10:5-11].
“Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia”- Mithali 22:3
Amani ya Kristo iamue ndani ya Mioyo yenu 
Kama ndani ya moyo wako hauna amani na utulivu juu ya uamuzi unaotaka kufanya, usifanye maamuzi kwanza. Kukosa amani na utulivu juu ya jambo hilo unalotaka kuamua ni ishara ya Roho Mtakatifu ndani yako kwamba kuna jambo haliko sawa bado; inawezekana muda bado au jambo lenyewe haliko sawa. Inawezekana kuna mtu unataka kuingia naye katika uhusiano fulani mfano Kibiashara na hauna utulivu na amani juu ya mtu huyo au biashara hiyo, usiamue kwanza. Tumia muda wa kutosha katika kuomba Mungu ili akuongoze juu ya uamuzi huo; na kama bado haupati amani juu ya uamuzi huo jipe muda wa kutosha wa kutafakari na Kuomba ili Mungu akuongoze katika lililo bora zaidi. [Wakolosai3:15]
Usikubadili kusukumwa katika maamuzi na watu wengine au mazingira yanayokuzunguka kwa sababu baada ya kufanya hivyo ni wewe peke yako ndiye utakaye kabiliana na matokeo ya uamuzi huo; na haitakuwa na msaada wowote hapo baadae ukisema fulani ndiye aliyesababisha niamue hivyo. Jambo la msingi ambalo tungependa ukumbuke mahali hapa ni kwamba, wewe ni nahodha wa meli ya maisha yako; inategemea unaloazimia (unaamua binafsi) kwenda wapi. Jukumu hili si la mtu mwingine, watu wanaweza kukushauri lakini jukumu la uamuzi au uchaguzi ni lako binafsi.
Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana; Na kwa shauri la akili fanya vita- Mithali 20: 18
Tafuta mashauri ya neno la Mungu kwanza na uyazingatie kabla ya kufanya uamuzi, ushauri wa neno la Mungu juu ya kuwa na mahusiano bora, namna ya kumpata mwenza bora wa maisha, namna ya kuwa na ndoa nzuri, namna ya kulea watoto, ushauri juu ya mambo ya kiuchumi, biashara, namna ya kumtumikia Mungu kwa ubora, mambo ya uongozi, mambo ya kijamii…….n.k!
Hakuna aliyemshauri bora kwako kupita neno la Mungu. Ushauri wa Neno la Mungu ni bora kwa afya yako ya roho na mwili. Mungu hutoa ushauri ulio BORA kwa ajili yetu kwa sababu mwanadamu anaweza kuchagua jambo la kufanya lakini hawezi kuchagua matokeo ya jambo hilo atakalolifanya.
Tafuta watu wenye hekima na hofu ya Mungu ndani yao ili kukushauri juu ya jambo ambalo hujui ufanye nini na wakati huo huo unatakiwa kulifanyia maamuzi; usiamue kwa siri kama hauna utulivu wala amani nalo, usiamue peke yako ikiwa ndani ya moyo wako unajua kabisa kuwa unahitaji msaada.  Vijana wengi hufikiri kwamba kila aliyeko kwenye ndoa, ni mshauri nzuri juu ya mambo ya mahusiano na ndoa, hili halina ukweli sana. Lakini hii haina maana hauwezi kujifunza jambo la kukufaa kutoka kwao la hasha!
Jambo la muhimu ni kwamba, Unapoenda kuomba ushauri kwa mtu juu ya jambo lolote, ni vizuri kujiridhisha kwamba ushauri huo haupingani na kanuni za  neno La Mungu, kinyume na hapo ninakusihi usifanyie kazi ushauri huo bila ya kujali nani ameutoa. Neno la Mungu linashauri kwamba ni shauri la AKILI tu ndio ufanyie kazi. [Mithali 13:20

2 comments :

WEWE NDANI YA KUSUDI LA MUNGU

8:12:00 PM Unknown 0 Comments

 
WEWE NDANI YA KUSUDI LA MUNGU
(Samaki ndani ya maji, wewe ndani ya kusudi la Mungu)

Hapo mwanzo kila alichokiumba Mungu aliona kuwa ni chema ‘good’; alionesha kuridhishwa na hali yake. Mungu huvipenda vitu vyote alivyoviumba. Mungu hupenda watu tofauti tofauti, wenye vionjo na tabia tofauti tofauti. He is God of Varieties! Alimpenda Musa mpole, lakini alimtaka Haruni ambaye ni msemaji (mwongeaji) amsaidie Musa. Mungu anakusudi jema na watu wa haiba zote, kasumba mbali mbali au silika yoyote ile. [Mwanzo 1:31]
Kama aliyekuumba amesema wewe ni mwema ‘good’ maana yake uko tayari kwa kazi fulani. Alipoitazama ile kazi na alipokutazama wewe akasema vema, maana yake ameonesha kuridhishwa na uhusiano uliopo baina yako wewe na kusudi uliloitiwa.
Ukiona uko katika eneo ambalo linakuhitaji ujifanyie marekebisho makubwa sana (massive change) ili uwepo wako ufae katika eneo hilo, lazima ujiulize mara mbili; inawezekana si eneo lako.  Ukiona uko na mtu anayetaka ubadilike sana ili umfae yeye, ujiulize mara mbili pia; yawezekana si wa shirika lako. Kusudi la kuumbwa kwako ndiyo bahari pekee unayoweza kuogelea kwa urahisi.  Samaki hafanyi marekebisho yoyote ili afae kukaa majini, wala tai hafanyi marekebisho ili kuruka, anafanana na kusudi lake. Sihitaji kuwa mtu fulani ili niwe mimi.
Tunapoteza muda mwingi tukisubiri kubadilika, ati! ndio tuanze. Ukweli ni huu: “Agent of change never change” yaani, wakala wa mabadiliko habadiliki. Kama umezaliwa kubadilisha ulimwengu maana yake wewe umeshabadilika tangu hujaja duniani. Kama umezaliwa kuwatoa watu utumwani maana yake wewe si mtumwa. Musa hakuwahi kuwa mtumwa japo alikuwapo Misri. Yesu hakuwahi kutenda dhambi japo aliishi duniani. Kama umezaliwa ili kufa, maana yake umeshakufa hata kabla hujazaliwa (mkumbuke Yesu). ...Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia” Ufunuo 13:8
Mungu haleti wanafunzi wa kada fulani hapa duniani, Yeye hushusha watendaji ambao tayari ni imara kabisa.  Huleta askari walio tayari kwa vita na si kwa mafunzo. Ukizaliwa tu, ujue umeshatumwa; si lazima ukae na Yesu miaka mitatu kama mitume; ni hasara kuwa mwanafunzi asiyehitimu. Habari yako ni ya tofauti, umezaliwa ukiwa tayari. Bwana akawatuma (wakazaliwa) Yerubaali, na Baraka, na Yeftha, na Samweli, akawaokoa ninyi na mikono ya adui zenu pande zote, nanyi mkakaa salama.” 1 Samweli 12:11 [Maneno ya kwenye mabano ni msisitizo wa mwandishi].
Shida zako zinakusaidia kujua jambo moja kubwa kwamba, “wewe ni mkimbizi.”  You’re not where you belong! Bora uwe mkimbizi katika nchi jirani kuliko kuwa mkimbizi katika kusudi la Mungu. Unafanya vizuri kazi isiyokupasa kufanya, unakula usichopaswa kula, na una marafiki usiopaswa kuwa nao. Hii ilimpata mwana mpotevu; alikula na nguruwe, badala ya kula na Mungu, si unajua ukifungua moyo Yesu atashinda kwako na kula pamoja na wewe. Usipofungua mlango ndio habari ya kula na nguruwe inakuja. {Ufunuo 2:20}
Mwana mpotevu alipogundua ukweli kwamba, anatawaliwa na mazingira badala ya yeye kuyatawala aliamua kuondoka. Kusudi ndilo linakupa uwezo wa kuyatawala mazingira badala ya mazingira kukutawala wewe. Tukimtosa mtu baharini bila ya kumwokoa au kumpa vifaa vya kumsaidia, bila shaka baada ya kitambo atakufa. Si kifo cha bahati mbaya, mazingira (maji) yamemtawala. Mungu alitaka tuyatawale mazingira yetu kupitia kuishi  kusudi, kila yanapotutawala yanaashiria kifo.
Baba anaweza kukukataa, hata mama anaweza pia. Ni sehemu moja tu unayoweza kupokelewa bila ya kuambiwa ondoa hiki na kile kwanza, nayo ni katika kusudi lako. Your purpose will adopt you as a lovely son/daughter
Kama nimezaliwa kucheza mpira si lazima nicheze kwenye kiwanja cha mtu asiyenitaka, pia si lazima nicheze katika timu isiyonikubali. Ndio maana kuna viwanja vingi na timu nyingi. Kamwe usibadili uamuzi wako wa kucheza mpira bali badilisha timu na viwanja.  Nimewahi soma nukuu hii: “Change direction but don’t change your decision.”
Ni sehemu moja tu ambapo hisia zako zote hupokelewa, ni mahali pale tu ndipo kimo chako huleta maana, ni katika kusudi uliloitiwa na Mungu ndipo haiba yako; utanashati wako, kujisahau kwako, ukimya wako, mihemko yako, haraka zako, udadisi wako, ujasiri wako, hekima yako na upole wako hupokelewa kwa moyo wote. Ni katika kusudi la Mungu ndipo Musa mpole na Haruni msemaji wote huwa na  maana. {Kutoka 4:14}
Sijui unapata taswira gani unapomuona kaka mtanashati, sijajua unawaza nini unapomuona dada mrembo, binafsi ninajua jambo moja, “mwili ni kwa BWANA.” Kama alivyoagiza Yesu mitume wamfungue yule punda na atakayeuliza ajibiwe hivi: “BWANA anahaja naye.” Ndivyo ilivyo kwako, BWANA anahaja nawe na namna ulivyo. ... Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili.” 1Wakorintho 6:13
Mungu ni Roho, roho haili nyama ya mtu wala ya punda. Ukisikia maandiko yanasema BWANA anahaja nawe ujue kinachotajwa hapo ni utumishi au kusudi la kuumbwa kwako wala si ,’lunch’. Biblia inasema “mwili si kwa zinaa bali ni kwa ajili ya BWANA.” Mwili wako unaakisi kusudi lako. UKiliendea kusudi lako litakupokea bila ya kukuambia jikarabati kwanza. Kwani  tayari unafanana na kusudi lako, hakuna haja ya ukarabati.
Biblia inatafsiri, mwili ni nyumba ya roho. Si kila nyumba ni kwa ajili ya kulala, nyingine ni ofisi. Nadhani kwa mtazamo wa biblia, mwili ni ofisi. Ofisi huakisi kazi za taasisi husika. Kwa mamantilie jiko ni ofisi, kwa fundi makenika Gereji ni ofisi. Jiulize nini kinafanyika katika mwili wako kama ofisi.  Muonekana mzuri na tabasamu bashasha usio sadifu matendo unatupa nafasi ya kujua kwamba hauishi kusudi lako. Kaka mzuri unavuta sigara, balaa gani kama hii! Dada mzuri lakini kahaba, ni msiba gani kama huu! Jengo linaashiria kusudi jema lakini kinachotendeka ndani ya ofisi (mwili) ni ubatili.
Hadi biblia ikasema, “mwili si kwa ajili ya zinaa” maana yake watu hudhani mwili ni kwa ajili ya zinaa. Mtazamo huo mbovu umepelekea kusudi la Mungu kusahaulika.Tujifunze kwa Yesu, alipata mwili ili autumie katika mateso na kuleta ukombozi. Alikuwa na sababu za kiofisi za kuvaa mwili. Bila mdomo asingelikunywa siki, bila mabega asingelibeba msalaba.  Mwili ni kwa ajili ya utimilifu wa kusudi. Mwili wake ulikuwa ofisi ya kutimizia kusudi. Alionekana kama kusudi lake, wewe pia umefanana na kazi fulani au wito fulani na Mungu amekushakupa ofisi yaani, mwili.
Kama una mwili lazima ujue lipo kusudi kwa ajili yako. Unamsubiri Mungu? Alishasema imekwisha, tena akasema kila alichokiumba ni chema; Anakusubiri wewe. Badilisha mtazamo wako, anza hiyo safari, anza sasa hiyo biashara, ondoka huo mkoa uende anapokupeleka Mungu. Labda ulikimbia shule rudi masomoni, anza kulifanyia kazi hilo wazo, chukua fomu na ugombanie hiyo nafasi, anza kuamka mapema, anza kuishi hilo kusudi, anza kuwasaidia yatima, labada ni mhudumu anza sasa kuhudumu, tekeleza azma ya moyo wako na kuyatawala mazingira yako. Badala ya kuishia kujivika nguo nzuri (pamba kali) za kisasa wewe tinga kusudi la Mungu na kisha utoke, wakati ni sasa! Ogelea.

0 comments :

KILA KITU KIPO KWA KUSUDI MAALUMU

8:06:00 PM Unknown 0 Comments

  
KILA KITU KIPO KWA KUSUDI  MAALUMU
Kutambua sababu ya kuwepo kwako ni jambo la msingi kuliko yote unayoweza kufanya, vinginevyo maisha yanakosa maana. Kusudi ndilo linatoa msukumo wa kuwepo au kutengenezwa kitu ili kutimiza malengo maalumu kwa wakati uliowekwa. Kusudi la kuwepo kwako ndilo linaloleta maana na utoshelevu hata kwa vitu vingine.
Kusudi maana yake ni sababu iliyofanya au inayofanya kilichopo kiwepo au kitengenezwe jinsi kilivyo ili kutimiza kazi maalumu katika kufikia malengo yaliyokuwa yamekusudiwa kabla ya kitu hicho kuwepo au kutengenezwa. Kila kitu kipo kwa kusudi maalumu; hakuna kilichoumbwa au kutengenezwa kiwepo kwa sababu ya kuwepo tu. 

Maua yapo kwa kusudi, wadudu wapo kwa kusudi maalumu hata wanyama wapo kwa kusudi maalumu; wanasayansi wamegundua kuwa kuna baadhi ya viumbe endapo vitatoweka, mfumo wa ikolojia (Ikolojia ni mfumo wa ki-biologia unaoonesha kutegemeana kwa viumbe hai, pamoja na mazingira yao katika kuendeleza uhai) utaadhirika na hivyo kuhatarisha uhai wa binadamu. Ikiwa viumbe hivi vipo kwa kusudi maalumu je, si zaidi ya mimi na wewe?
Ile kwamba kila kitu kimeumbwa kwa kusudi maalumu haina maana kwamba kila kitu kinaishi kulingana na kusudi hilo la kuwepo kwake. Dr. Myles Munroe katika kitabu chake cha Understanding purpose and power of men, ameandika “Kusudi la kitu lisipojulikana, matumizi mabaya hayaepukiki”. Usipojua kwanini umeumbwa maisha ya kila siku yanakuwa ni majaribio. Tumepewa muda wa kuishi; hatujapewa muda wa majaribio ya kuishi. Watu wengi wamekutwa na mauti wakati bado wanajaribu kuishi. What a tragedy!
Yeremeia akiwa bado kijana mdogo alijijua kuwa yeye ni nabii wa mataifa, Daudi akiwa bado kijana mdogo alijijua kuwa yeye ni kiongozi wa Israeli, Yesu akiwa bado kijana mdogo alijua jambo gani limempasa kufanya (Luka2:49-50).
Ufanisi katika maisha ya mtu haupimwi kwa kuangalia ameishi kwa muda gani, bali hupimwa kwa kuangalia kwa namna gani mtu ameishi kulingana na kusudi la kuumbwa kwake. Si kwa urefu bali kwa ukamilifu.
Mungu hana upendeleo kwa mtu yeyote; ikiwa Yeremia, Paulo, Musa na watu wengine wakuu tunaowasoma kwenye Biblia na hata nje ya Biblia kama Mother Teresa, Martin Luther King Jr na wengine wengi ambao majina yao na kumbukumbu zao zinaheshimiwa hata sasa, waliumbwa kwa ajili ya kutumikia kusudi maalumu la Mungu; hata wewe unalo kusudi maalumu juu ya kuumbwa kwako wakati huu; lakini  tunaanza na Mungu.
Wewe pia ni jibu
Kila aliyezaliwa na mwanadamu ni jawabu, wala hakuna haja ya kutafuta majibu nje yako; umekuja kuleta majibu juu ya swali au changamoto au upungufu uliopo duniani ambao unahitaji uwepo wako.
Musa alizaliwa akiwa kiongozi, aliyebeba jibu la Israeli juu ya utumwa wao katika nchi ya misri; Gideon alizaliwa akiwa mtetezi wa Israeli aliyebeba jibu la mateso ya Israeli juu wa wamidiani; Samson alizaliwa akiwa kiongozi wa Israeli aliyebeba jibu la mateso ya Israeli juu ya Wafilisti. Yesu Kristo pekee ndiye Aliyebeba jibu juu ya dhambi na uonevu wa shetani kwa wanadamu.
Kutokujua kusudi au sababu ya kuwepo kwa kitu, haifanyi kitu hicho kukosa sababu ya kuwepo kwake. Ile kwamba hujajua bado kusudi la kuwepo kwako haina maana hamna kusudi la kuwepo kwako. Kusudi la kuwepo kwako ndilo lililofanya uwepo wako uwe muhimu.
Mungu aliliweka kusudi lako kabla ya wewe haujazaliwa; Mungu aliamuru idadi ya siku zako kabla hazijaanza kuhesabiwa hapa duniani.
“Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; chuoni mwako ziliandikwa zote pia, siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado Zaburi 139:16-17!
[Msisitizo umeongezwa]
Mungu hutangaza mwisho wa jambo mwanzoni; Huuweka mwisho wa jambo kabla ya kuanza jambo lenyewe. Ukiona Mungu ameanza jambo, basi ujue mwisho wake upo tayari. Mungu haanzi jambo lolote bila ya kuhakikisha kuwa kila kitu kitakachohitajika ili kutimiza kusudi hilo kipo tayari. Hii ni kanuni ya Ki-Mungu isiyobadilika; Na inakupa uhakika kuwa lipo kusudi maalumu juu ya kuumbwa kwako. [Isaya46:10-11]
Siku Moja Yesu aliwafundisha  wanafunzi wake kanuni hii muhimu inayokupa uhakika wa kufanikiwa katika maisha ya kila siku. Aliwafundisha kwa mtindo wa swali akisema,
Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.” Luka 14:28-30
Ile kwamba umezaliwa na bado unaishi hadi muda huu unaposoma ujumbe huu, ni udhibitisho tosha kwamba Mungu analo kusudi maalumu kwa ajili yako litakalo kuwezesha kuishi maisha yenye ufanisi na mafanikio ya kweli; Na kwamba, kile Alichokianza katika maisha yako Anao uwezo wa kumaliza.
Tunaanzia hapa!
Maisha ya mwanadamu ni kama kitabu, kwa jinsi anavyokaa na Mungu ndivyo kinavyozidi kufunguka kurasa hadi kurasa. Hayati Dk. Myles Munroe anaandika katika kitabu chake cha Understanding your potential, kwamba “Hatuwezi kujua sisi ni nani kwa kuhusiana na viumbe, bali tunaweza kujitambua kwa kupitia kuhusiana na Muumba”
Huwezi kujitambua wewe ni nani na kuitambua kazi uliyoitiwa na Mungu hata ukatembea katika kusudi la kuumbwa kwako kabla ya kukutana na Mungu, na kuwa na uhusiano naye binafsi
Musa alijua kusudi lake alipokutana na Mungu nyikani; Sauli (Paulo) alijua kusudi lake alipokutana na Yesu njiani, Petro na Yohana pia kule ziwani. Ni ajabu wengine wanaweza kukutwa na mauti kabla hata ya kugundua kazi maalumu na sababu ya kuumbwa kwao.
Kabla ya Mungu kukufunulia kusudi lake kwa maisha yako, Hujifunua kwako kwanza; Hukukutanisha na U-Mungu wake kwa kuwa umetoka kwake na wewe ni sura na mfano Wake [Mwanzo1:26]. Ndio maana kumpokea Yesu ni Muhimu si tu kwa ajili ya kwenda Mbinguni lakini pia inakupa fursa ya kutambua kusudi la Mungu kwako kwa hapa duniani na kukuwezesha kuishi maisha yenye ufanisi na mafanikio huku ukimaliza “mwendo” bila majuto. Hautamaliza bila kuanza sasa;

“Ni lazima kuishi katika kusudi hata kama halituvutii sana.”

0 comments :