UNATUMIA KIUNGO GANI KUTAZAMA MBALI?
UNATUMIA KIUNGO
GANI KUTAZAMA MBALI?
Mwili wa binadamu unaviungo vingi kila
kimoja kikiwa na kazi yake. Ipo pia milango ya fahamu ambayo kwa kuhisi,
kunusa, kuonja na kwa kuona hufanya kazi. Viungo hivi na milango hii ya fahamu si
tu kwamba ipo kwa binadamu bali hata wanyama, ndege na baadhi ya wadudu
wamejaliwa na Mwenyezi kuwa nayo.
Binadamu ndiye mwenye jukumu la kuwatawala
ndege, wanyama, wadudu na hata viumbe wasioonekana (mapepo, majini, malaika).
Kitabu cha Waebrania kimeeleza malaika ni roho wanotuhudumia, pia mzaburi
amenena wazi jinsi Mungu alivyomfanya mwanadamu punde tu kama yeye na amemvika
utukufu na heshima.
Licha ya utukufu huo mwanadamu si kiumbe
mwenye uwezo mkubwa wa kuona. Tai, mwewe na hata ndege wengine huona mbali
zaidi kuliko mwanadamu. Ni watu wachache tu wenye macho makali ya kuona mita
mia tano au zaidi.
Swali, Ni kwa nini macho ya wanadamu ambao
kibiblia ndio watawala wa dunia hii yanazidiwa na hawa ndege? Jibu langu ni
rahisi, Mungu hakutaka mwanadamu aishi kama tai, Hakutaka mwanadamu aone mbali
kwa macho ya nyama bali atumie akili, fikra na imani katika kuona kwake. Kwa
njia hizi ataona mbali zaidi ya tai na hivyo atamtawala mpaka tai.
Mwanadamu anauwezo wa kuona hata miaka 20
ijayo na akanunua shamba leo na kupanda miti. Mwanadamu wa leo anaweza kuona
miaka 100 ijayo. Hayati Rais Kennedy wa Marekani anayetajwa katika simulizi za
kwenda mwezini, aliwaita wanasayansi wake na kuwapa wazo hilo ambalo hawakuwa
wamewahi kulisikia popote. Hebu waza unamka unaitwa na Rais na anakwambia,
naomba uanze kufikria jinsi gani tutakwenda kwenye Mwezi au Jua. Wakati huo
wewe hujawahi hata kuzifuatilia nyota za angani.
Baada ya wanasayansi hao kufanyia kazi wazo
hilo kwa miaka kadhaa walifanikiwa na kwa sasa kwenda mwezini au kutuma vyombo
kwenda huko si jambo la ajabu tena. Tofauti na hayati Rais Kennedy ambaye ni
mtu wa fikra, Rev Martin Luther King Jr ambaye ni mwanaharakati, yeye katika
harakati zake za kumkomboa mtu dhidi ya ubaguzi
wa rangi anaonekana kuona mbali kama nabii, na hii ni kwa sababu ya
Imani yake ambayo mzizi wake ni neno la Mungu.
Alisema Fred Swaniker kwamba, Afrika
inahitaji Moon shoot thinking, akimaanisha tunahitaji kufikiri mbali sana, tunahitaji
kuruka kifikra (kimawazo) na kutua mbali, mahali ambapo kwa uhalisia macho ya
kawaida hayapaoni ila kwa imani na fikra sahihi tunapaona.
Katika ulimwengu huu hata kipofu anaweza
kufanikiwa kama ubongo wake umechangamka kuliko watu mia wenye macho makali
lakini ubongo umelala. Kuna jambo linanishangaza katika taifa langu, vijana
wengi ukiwahoji si watu wa fikra.
Siku 1000 za kwanza katika ukuaji wa mtoto
zijulikanazo kama “mwanzo bora” zina mchango mkubwa katika uwezo wa kufikri wa
mtoto. Utapia mlo ndio huzaa watu wenye mawazo mgando, na mawazo maji, yote ni
matokeo ya mdororo wa chakula. Mfumo wetu wa elimu hauruhusu udadisi hasa kwa
kuwa mwalimu ndio kila kitu, si rahisi mfumo wetu kuzalisha watu wanaofikiri
kimkakati.
Ili tupate vijana wanaofikiri sawasawa basi
ni muhimu tuwajenge kwa neno la Mungu ambalo litaleta imani, tuwape chakula
bora cha akili yaani vitabu sahihi vya kiada na ziada, watoto wapewe mlo kamili
ukijumuisha matunda, vyakula vya wanga, protini na maji mengi.
0 comments :