Unaweza
kuwa na urafiki hai na Yesu na bado ukawa masikini wa mali na fedha wala si
ajabu, unaweza kuugua na bado ukawa na urafiki mzuri na Yesu. Lazaro alikuwa
masikini na alikuwa mgonjwa lakini bado urafiki wake na Yesu ulikuwa hai. Kamwe
vitu na hali ya afya au fedha si jawabu la mwisho la kuonyesha uhusiano wa mtu
na Mungu, Yohana 11:2. Pastor Chris Oyakhilome anaandika katika utenzi wake, “jambo
muhimu kabisa katika maisha haya si umiliki wa mali, bali ni kugundua kusudi la
Mungu na kulitimiza”. Maisha
hayahusu milki za mali, unaweza ukawa unamiliki kila kitu hapa duniani na bado
isikufaidie chochote. Yesu Alishasema, “…maana
uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyonavyo.” Luka 12:15
Unapompokea
Yesu unapokea kwanza mambo ya msingi na ya lazima kama vile: uzima wa milele,
Roho wake mwema, imani ya kweli, uponyaji na unafanyika makao yake. Haupokei
aina mbalimbali za magari Toyota Carina, Vos wagon wala Isuzu, haya hata yakija
huitwa ziada, cha msingi uzima wa milele. Vitu ni vitu na mtu ni mtu. Kamwe uzima wa mtu haumo katika mali au
alama za juu katika tasnia fulani, bali umo ndani ya Kristo Yesu. Hata upewe
ulimwengu mzima ni bure kabisa kama hautaweza kudumu katika kusudi la Mungu.
Nafsi yako haiwezi kununuliwa na jumla ya utajiri wote wa dunia hii. “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata
ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Marko 8:36
Shabaha
ya shetani ni kuwaona watu wakimlaani na kumlaumu Mungu wao, kwani adui anajua
wazi Mungu hapendi kulaumiwa. Mafanikio ya kiroho hayapimwi kwa alama za juu
darasani, nyumba gari au fedha nyingi. Baraka ni muhimu ila si kipimo sahihi.
Kujipima kimwili ni sababu kubwa inayofanya watu wa kiroho wamlaumu Mungu na
kujuta.
Ukikwepa
kusudi la Mungu baadaye utajiona huna faida, hautaacha kulaumu kwa kuwa mazingira
yatakuwa kinyume na wewe. Utaona umekuja duniani kama mtalii tu, wala hakuna
ulichokamilisha. Mtu hana faida nje ya wito na kusudi aliloitiwa na Mungu.
Maneno ya Solomoni kwamba, “mtu ana faida
gani ya kazi yake…” yanafanana na yale ya nabii Malaki, “Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida;”
haya ni maneno ya watu waliosahau kusudi la Mungu, na kujikuta wakipenda dini,
mali, wake zao, serikali, vitu, marafiki au watoto kuliko kusudi la Mungu.
Nilijifunza
mahali fulani kwamba watu wa ki-dunia huutafuta mkono wa Mungu (vitu) lakini
sisi tunautafuta uso wa Mungu (uwepo). Ukiwa mtu wa kiroho jipime kiroho.
Usijipime kwa kuangalia jinsi waovu au wasio mtii Mungu wanavyofanikiwa. Cha
msingi angalie kama unalitendea kazi kusudi la Mungu kukuumba wewe.
Ukipenda
kujilinganisha na watu na vitu matokeo utakayopata ni kuona utumishi wako hauna
faida. Utaona kumtumikia Mungu hakuna faida, na matokeo yake ni kuleta laana
katika maisha yako. Mungu anajua kila amtumikiaye anapata faida ndio maana
hapendi watu wake waseme hakuna faida katika utumishi.
"Maneno yenu yamekuwa magumu juu
yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna
gani? Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa
kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa
majeshi? Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam,
watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.” Malaki
3:13-18
Hatupaswi
kujipima kimwili bali na tujipime kiroho kwa kuzingatia kusudi la kuumbwa
kwetu. Unaweza ukawa na fedha nyingi, cheo kikubwa, mavazi mazuri na mke mzuri,
lakini kama hujatumikia kusudi la Mungu katika hayo basi ulichofanya ni bure
tena ni sawa na kufukuza upepo. "Mhubiri
asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida
gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua?” Mhubiri 1:2-3
0 comments :