USIWAPELEKE MAHALI USIPOWEZA KUWATOA

10:09:00 PM Unknown 0 Comments

 
USIWAPELEKE MAHALI USIPOWEZA KUWATOA
Hili ni jambo la msingi kwa kiongozi wa ngazi yoyote ile, haijalishi ni ngazi ya familia, kata, kampuni, taasisi binafsi au kiongozi wa siasa. Kuna maeneo ukiwafikisha watu au ukiwapeleka unaowaongoza hautaweza kuwatoa wote kwa usalama. Kiongozi lazima awe na kipimo cha madhara na uathirika unaoweza kujitokeza kabla ya kuchukua uamuzi wake.
Kwenye biblia kuna kisa cha Lutu aliyemuita Ibrahimu mjomba. Huyu baada ya kuipeleka familia yake katika miji ya Sodoma na Gomora alishindwa kuwatoa wote. Huko alimpoteza mkewe.  Alitamani waokoke familia nzima kama walivyoingia lakini hakuweza. Ingawa haijaandikwa lakini nina hakika Lutu alijisikia vibaya kumpleleka mkewe mahali asipoweza kumtoa. Sodoma ilikuwa ni uchaguzi wa Lutu nyakati za kutengana na Ibrahamu, haukuwa uchaguzi wa mkewe Lutu. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.” Mwanzo 19:26
Rais Obama aliyekuwa kinara katika kuangusha Serikali ya hayati Rais Gadafi wa Libya alinukuliwa akijutia kushindwa kuijenga Libya mpya. Obama amewafikisha watu wa Libya mahali ambapo hawezi kuwatoa. Mpaka ameondoka hajaweza kujenga Libya mpya aliyoahidi na badala yake imekuwa pango la magaidi na wapiganaji.
Amesisitiza mwenye hekima mmoja kwamba, “In life you cannot undo every action” akimaanisha, “Katika maisha si kila kitu unaweza kukirejesha tena katika uhalisia wake.” Kuna akili zilizoharibika, kuna familia zilizoharibika, kuna vikundi vilivyoharibika; kuna jamii zilizoharibika, pia kuna kampuni zilizoharibika na si wote watakao weza kufanya urejesho. Kwa kuwa zoezi la urejesho ni gumu na zito basi ni busara kuepuka uovu, tabia hatarishi na mazingira yake. Huwezi kuepuka moshi ikiwa unapika kwa kuni, kwa hiyo katika kubadilisha mwenendo huwezi kupuuza mchango wa mazingira yako. Mazingira hatarishi ya Sodoma na Gomora ndio chanzo cha uharibifu wa mke wa Lutu.
Kama baba wa familia au kiongozi (Lutu) ni lazima uogope maamuzi au maeneo ambayo huna uhakika kwamba, wale unaowaongoza watatoka salama. Yuko rafiki anayeweza kukufundisha tabia mbaya ambayo huwezi kuiacha, yako makundi mabaya ambayo yanaweza kukufundisha tabia hatarishi ambazo huwezi kuzikomesha. Je, unamkumbuka uathirika uliingia lini maishani mwako? Ulevi, ubwiaji wa unga na dawa za kulevya, utazamaji wa picha chafu na uasherati? Ni baada ya kujisamehe sisi wenyewe ndipo tunapoweza kumsogelea Yesu mwanamapinduzi ili atusamehe na kutupa upya.
Watu wengi wamekuwa wanamwogopa Yesu kwa kuwa ni mwanamapinduzi na wanajua wakimsogelea atapindua tabia zao na atapanda tabia njema. Mwanamke Msamaria aliyekutana na Yesu kwenye kisima cha Yakobo alikuwa na uathirika. Alikuwa amekuwa na wanaume watano, that was an addiction! Na kwa muda ule mfupi Yesu alipindua maisha yake.
Muda, afya njema, ufahamu, malezi ya watoto, umoja na mshikamano ni moja ya mambo ya kulinda sana kwa kuwa hayarejeshiki kirahisi na pengine hayarejesheki kabisa baada ya kuharibiwa.
Jilinde!

0 comments :