Kuelekea Uhuru wa Kifedha

12:43:00 PM Unknown 0 Comments

 
KUELEKEA UHURU WA KIFEDHA
(THE BIBLICAL LAWS OF MONEY)
Tafiti mbalimbali zinaeleza kwamba, moja ya changamoto kubwa ulimwenguni hasa bara la Afrika ni umasikini mkubwa wa kipato. Ni ukweli unaosikitisha, na eneo hili ni moja ya maeneo ambayo hayana msisitizo mkubwa ndani ya mwili wa Kristo (kanisa). Eneo la maarifa kuhusu fedha au uchumi ili kumkomboa mtu kiuchumi ni kama limeachwa; Na kwa sehemu kubwa ukiona mahali fedha inatajwa kanisani au kikundi cha sala basi ujue ni sadaka inayozungumziwa. Ni watu wachache sana wanaozungumzia au kuhubiri au kufundisha maarifa kuhusu fedha na uchumi ili kumuwezesha mtu kupiga hatua katika eneo hilo kwenye maisha yake na jamii yake.
Jambo moja ambalo ni halisi na halikwepeki ni kwamba, ili kuishi katika ulimwengu huu wa sasa kila mtu anahitaji fedha za kutosha kumuweza kukidhi mahitaji yake na mahitaji ya wale wanaomzunguka. Kumbuka fedha haina dini, haijali kabila wala rangi yako; haiwezi kuja kwako kwa sababu wewe ni wa dini au dhehebu au rangi au kabila fulani (it is neutral). Na kwa sehemu kubwa, kiwango cha fedha au mafanikio ya kiuchumi ya mtu yanategemea kiwango cha maarifa na ufahamu sahihi alionao juu ya kanuni za fedha (The laws of money).
Nakumbuka siku moja wakati nipo sekondari niliwahi kuhudhuria kikundi cha sala mahali  fulani, na siku hiyo tukafundishwa kuwa ili kufanikiwa kifedha basi ni lazima tutoe sadaka ya kupanda ili makusudi tuvune mara mia kwa kigezo kwamba ukitoa utapokea mara mia ya ulichotoa (bila shaka unakumbuka hilo andiko). Na tena nikakumbuka lile andiko la kila apandacho mtu ndicho atakachovuna, basi nikapiga hesabu zangu pale, kwamba endapo nitatoa elfu moja basi nitarajie kupokea laki moja (bila shaka sijakuacha hata kama ulikimbia hesabu, elfu moja mara mia ni laki moja). Sijui kama unaelewa maana yake nini upo sekondari unatarajia kupokea laki moja ya kwako binafsi (hahahaha). Nikawaza tu nikiipata hiyo laki moja napanda elfu kumi, sasa piga hesabu hapo elfu kumi mara mia, mavuno ni kiasi gani? (tajiri mtoto anayechipukia).
Japo unaweza kucheka, inawezekana umewahi kuwaza hivyo pia. Kanuni moja muhimu sana kuhusu fedha ambayo huwa haifundishwi na leo nataka niigusie ni kanuni ya uzalishaji bidhaa au huduma (The law of production). Pamoja na kwamba sadaka na maombi ni muhimu sana kwa ustawi wa mtu; ni ukweli uliowaza kwamba hakuna aliyefanikiwa kiuchumi kwa mambo hayo TU (bila uzalishaji huduma na bidhaa) isipokuwa aliyepo upande wa kupokea.  Wazo kuu tunalotaka ulipate kwa siku ya leo ni kwamba, ukitaka kufanikiwa kiuchumi hauwezi kukwepa uzalishaji bidhaa au huduma kwa namna moja au nyingine.  Nioneshe anayeuza bidhaa au huduma, nikuoneshe mtu atakayefanikiwa kiuchumi. Zalisha huduma au bidhaa ambayo tunauhitaji nayo, na sisi tutakuwa tayari kukupa fedha kwa kuipata bidhaa/huduma hiyo kwa sababu tunaihitaji na hapo mafanikio ya kiuchumi yatakuwa dhahiri kwako.
Mungu ameahidi mvua ya Baraka, sio mvua ya fedha. Mungu ameahidi kushusha Baraka kwenye kazi ya mikono yako, kapu lako na chombo chako cha kukandia unga, mifugo yako, mazao shambani kwako, hakuna mahali ameahidi kushusha fedha toka juu. [Kumbukumbu la torati 28:4-5, 8]. Kusubiri mavuno ya sadaka uliyopanda tangu mwaka juzi ili utoke kwenye mkwamo wa kiuchumi uliona sasa, ni uvivu wa kufikiri, na ni kukosa uwajibikaji (irresponsibility).
There’s a place for you at the top!

0 comments :