MTU MGUMU
KUTAWALIKA
Ni rahisi sana kutazama wengine na sisi
wenyewe tukasahau kujitazama na kujitathmini. Tunaweza tukayajua sana mapungufu
ya wengine na tukasahau wapi tunapungua. Imenenwa, “Unakiona kibanzi kwenye
jicho la nduguyo na unaacha kutazama boriti ndani ya jicho lako”.
Profesa na Mhadhiri wa chuo kikuu cha
Havard cha Nchini Marekani bwana Bill George anaandika hivi katika moja ya
vitabu vyake, “The hardest person you will ever have to lead is yourself”.
Wewe ndio mtu usiye tawalika, wewe ndio
mtu mgumu kwa viongozi wako. Mara nyingi tumezoea kusema ni fulani na kujisahau
kwamba, tunayo mapungufu makubwa. Kwangu mimi mtu mgumu kumtawala ni mimi, na
wewe ni vema ujijue vema.
Miili yetu inaasili ya kutokutawalika.
Ukipanga mpango wa kuacha michepuko unaweza kushuhudia vita dhahiri ambayo
mwili unainua, hali kadhalika unapopanga kufunga. Biblia inasema, “Ifungeni
dhabihu kwa kamba kando ya madhabahu”. Imenenwa pia, “Itoeni miili yenu kama
dhabihu”. Kwa nini sadaka ifungwe kwa kamba? Isipofungwa itagoma au itakimbia.
Isipofungwa haitawaliki. Warumu 12:1-3
Kufungwa ni kulazimisha, kutia adabu,
kufanya tena na tena mpaka maadili mema na utii uwe sehemu ya maisha yetu. Ni
ngumu ni lazima ukaze. Wachichanji wanajua, ili uchinje nguruwe unahitaji
kufanya kazi, ili utoe fungu la kumi unahitaji kujua kuacha matamanio binafsi
na kuwa mtii kwa Bwana.
Tukutane juu.
Chagua
Kuendelea Mbele
Mara nyingi tunapokutana na changamoto
katika kufikia yale tuliyopanga au kutazamia; tunaweza kuchagua mambo mawili
tu, kusonga mbele au kukata tamaa na kutafuta sababu ya kulaumu na kughairi
kuendelea mbele! Kile utakacho kiamua baada ya kukutana na changamoto ndicho
utakachokipata baada ya changamoto hiyo kupita.
"Ukifikiri kama unaweza au hauwezi,
upo sahihi "
Yaani ukifikiri na kuona kama jambo
fulani unaliweza au utaweza basi ujue upo sahihi; na ukiona au kufikiri jambo
fulani hauliwezi au hautaliweza basi ujue upo sahihi pia! Na hii ndio sababu inayofanya wengine
waendelee mbele na wengine kuishia kulalamika na kughairi kuendelea 'utukufu'
ulio mbele yao
" Bwana akamwambia Musa, Mbona
unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele" Kutoka 14 :15
Siri ya kufanikiwa wakati wa changamoto
sio kurudi nyuma au kukata tamaa, siri ya mafanikio ya kweli ipo katika
kuendelea mbele. Thomas Edison, mwanasayasi na mgunduzi amewahi kusema "Our greatest weakness lies in giving up. The
most certain way to succeed is always to try his one more time "
(Udhaifu wetu mkubwa upo katika kukata tamaa; njia ya uhakika kufikia mafanikio
ni kujaribu mara nyingine: Tafsiri isiyo rasmi)
Kumbuka jambo hili, Haukuanza ili uishie
njiani! Ndio, narudia tena haukuanza ili uishie njiani hivyo chagua kuendelea
mbele. Mwenye hekima mmoja amewahi kusema, unapochoka usiache (usikate tama);
jifunze kupumzika (ili upate nguvu ya kuendelea). Don't stop because you're tired, stop when it's done!
There's a place
for you at the top
MHESHIMU
RAIS WAKO
(Ni kwa
Heshima ya aliyemweka katika kiti hicho)
Ukiwa mtawala au
mmiliki wa biashara unaweza kumweka yeyote asimamie biashara hiyo kwa niaba
yako, asimame kama mwakilishi wako. Mwakilishi huyu bila shaka atakuwa na amri (authority
and power) kwa wale utakao waweka chini yake ili awaongoze na kuwasimamia vema.
Mwakilishi huyu akidharauliwa bila shaka wewe uliyemweka umedharauliwa pia. Serikali haziwekwi na wapiga kura, zinawekwa na Mungu.
Maeneo mengi tumeshuhudia wenye kura nyingi wakikosa Urais. Wanademokrasia
wenye imani wanaelewa hili.
Tunapaswa kuwaheshimu
viongozi si kwa sababu ni wema au ni wabaya bali, ni kwa heshima ya yule
aliyewaweka watuongoze yaani, Mungu Baba. Ameandika Mchungaji Kenneth Copeland,
“Hakukuwa
na Serikali korofi kama ile ya wakati wa Yesu Kristo, lakini bado Yesu alitaka
iheshimiwe na akasema, ‘yaliyo ya Kaisari apewe Kaisari.’” Kwa maneno
mengine Kristo aliwataka watu walipe kodi kwenye Serikali ambayo kimsingi
ilikuwa inawakandamiza, hata wao hawakuamini kama Yesu amesema waheshimiwe kama
Serikali. Serikali yaweza kuwa dhalimu lakini Mungu aliyeiweka kwa majira
husika si dhalimu, na anamakusudi nayo.
Muda mzuri
wa kuiheshimu Serikali ni pale inapofanya vibaya, maana ikifanya vema hata
wapagani huiheshimu (Luka 6:28).
Muda mzuri wa kubariki ni pale watu watakapo kulaani. Katika agano la kale
Serikali ya Farao yule wa wakati wa Musa ilikuwa korofi na yenye kiburi hata
mbele za Mungu, lakini Mungu alisema ni yeye aliyeiweka kwa makusudi yake. Kuna
kusudi kwa serikali yako. Serikali haijiweki madarakani inawekwa. Katika Warumi
9:17 neno nimekusimamisha linaweza kuwa na maana, nimekuweka. “Kwa maana
maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili
nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.” Warumi
9:17
Tunamuheshimu mkuu wa
nchi kwa sababu tunayo hofu ya Mungu
aliyemweka. Si kila Mtawala (Boss) anastahili heshima kutokana na tabia yake,
wengine wanatabia mbaya. Pamoja na hayo kila Mkristo anapaswa kutoa heshima kwa
kila mtawala bila kujali tabia yake.
Angalizo:
Katika kumtii kiongozi
lazima tuhakikishe hatumkosei Mungu, kiongozi asigeuke sanamu moyoni mwetu.
Sauti ya kiongozi ikiwa kinyume na injili ya Kristo na ipuuzwe. Mijadala mambo
ya mapenzi ya jinsia moja, mauji ya holela, utoaji wa mimba unaohalalishwa
kisheria, ndoa za mitala ni mambo ambayo ni kinyume na injili. Yapuuzwe hata
kama msemaji atakuwa ni mkuu wa Nchi.
Mungu anaweza
kubadilisha moyo wa kiongozi ikiwa watu watasimama kuomba. Maombi kwa Mungu
mwenye nguvu yanaweza kuelekeza nchi wapi ielekee ikiwa mwombaji ataomba kwa
bidii. Mungu anaendesha mioyo ya watawala kupitia maombi ya watakatifu.
Endelea
kuombea nchi yako….., Shallom Israel, Shallom Tanzania….
UZURI UNADANGANYA.
(Beauty is
fleeting)
Nimewahi kupewa ushauri kutoka kwa watu
mbalimbali kuhusu masuala ya mahusiano na ndoa. Nimejitahidi pia kusoma walau
vitabu kadhaa. Yote kwa yote kuhusu ndoa na mahusiano sitasahau ushauri huu,
“uzuri/urembo unadanganya.” Kwa nini unadanganya? Kwa sababu si wa kudumu, na
si kitu utakachokihitaji kila siku.
Si vema kumpuuza mtu mwenye hekima
anapofumbua kinywa chake kusema kitu. Solomon mtu mwenye hekima sana ndiye
aliyesema katika Mithali 31:30, “uzuri si wa kudumu” Yaani sura, mpangilio wa
meno, rangi na umbo zuri havisemi kweli maana baada ya muda mtu huzeeka na
ngozi hukunjamana, na mara urembo wote hutoweka. Maana yake uonavyo leo sivyo
itakavyokuwa milele. Kwa lugha nyingi si mambo utakayoyahitaji baadaye. Baada
ya muda kupita utagundua haukuhitaji sura bali ulihitaji, upendo, ushirika,
amani na uaminifu. Kwa nyakati tofauti wachungaji na wenye hekima wameonya
kwamba,kufanya uamuzi kwa kujali mwonekano wa nje ni hatari.
Amesema mwenye hekima huyu, “Mwanamke
aliye na umbo zuri na sura nzuri pasina maarifa kichwani afaa kwa usiku mmoja,
lakini yule mwenye ufahamu na maarifa afaa kwa maisha yote.” Ndoa ni agano la
maisha si la usiku mmoja. Mwonekano wa nje hautoshi kutoa taswira ya ndani ya
utu, uchapakazi, uaminifu na upendo.
Urembo ukisimama peke yake hautoshi,
utanashati peke yake hausaidii. Haipasi kuwa urembo na utanashati, badala yake
inafaa kuwa urembo na akili, urembo na uchapakazi, urembo na ibada, urembo na
upendo, urembo na uaminifu.
Ili urembo usikudanganye basi ni lazima
uwe umeujua ukweli. Tafuta watu wanaoheshimika utagundua si kwa rangi zao wali
si kwa urembo na utanishati wao bali ni kwa kujitoa sadaka, kuishi maisha ya
heshima, uaminifu na utu wema.
Wewe si Mr. Tanzania unaanzaje kuoa Miss
Tanzania? Urembo unadanganya.
Tukutane kileleni………
NYUMA YA MAFANIKIO YA KILA MTU
(THE SPIRIT BEHIND YOUR SUCCESS)
Ulimwengu usioonekana umekuwa ukitegemeza
ulimwengu unao onekana. Ulimwengu wa roho unategemeza ulimwengu wa mwili,
Ulimwengu wa roho unaamuru ‘dictate’ ulimwengu wa nyama. Tumezoea kusema nyuma
ya mafanikio ya kila mwanaume kuna
mwanamke, hii si sahihi saana.
Ukweli ni kwamba nyuma ya kila mwanaume
kuna roho, na si mwanaume tu bali ni nyuma ya kila mwanadamu kuna roho. Nyuma
ya mafanikio ya Yusufu kulikuwa na Roho bora, Nyuma ya ustadi wa Daudi kulikuwa
na Roho Mtakatifu.
Kila mwanadamu unayemwona, ni ama
anapelekwa na Roho wa Bwana au roho wa shetani. Nyuma ya kazi yako kuna roho,
nyuma ya Uhasibu wangu kuna roho pia. Kama alivyowahi kusema Mtumishi wa Mungu
Nabii Makandiwa, “Hakuna dakika wala sekunde ambapo mwanadamu anaweza kwenda
sehemu yoyote bila uongozi wa Roho wa Mungu au roho wa shetani”. Ni ama uko
chini ya uongozi wa Roho wa Mungu au roho wa shetani. Warumi 8:14
Umewaona watu sokoni, kanisani, shuleni,
au safarini? Ni ama wanaongozwa na Roho wa Mungu au roho ya shetani. Kila siku
na kila saa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, kinyume na hali hii ni uongozi
wa Roho wa shetani.
Nyuma ya kila kiongozi kuna roho, matendo
ya viongozi hudhihirisha roho wanazozitumikia, Namna pekee ya kujua roho/Roho
unayemtumikia ni kwa kuchunguza matunda unayozaa. Matunda ya chuki, uasi, wizi,
mgawanyiko, majanga, ukame, njaa, na vita hudhihirisha utawala fulani kiroho.
Zamani Mungu alisema na watu wake kwa mvua, njaa, ukame na magonjwa, hata sasa
mambo haya huzungumza kitu kutoka ulimwengu wa Roho.
Zingatia haya;
- Nyuma ya
mafaniko ya kila mwanadamu kuna roho.
- Ulimwengu wa roho
unatawala ulimwengu tunaoishi na kutembea ndani yake.
- Mwanadamu hawezi
kuishi bila nguvu ya rohoni.
Tukutane ijumaa, shalom.