Mungu ni mwakilishi wetu

 
MUNGU NI MWAKILISHI WETU.
(Anajua kupigana vizuri kuliko sisi)
Tunaishi kwenye ulimwengu wenye changamoto nyingi, watu wanafukuzwa kazi, yatima wanadhulumiwa; wanafunzi wanafeli, wazazi wanagombana, wapenzi wanaachana na vikao vya kazi havimaliziki kwa usalama.
Yote haya yanamfanya mwanadamu ajitahidi kuyakabili bila ya Mungu. Kuna kitu kinamwambia mwanadamu apigane mwenyewe, kuna msukumo usiotaka kumruhusu Mungu apigane.
Kwa nini tunashindwa kumruhusu Mungu aingilie kati? Ni kwa sababu tunadhani tunajua kupigana kuliko Yeye au ni kwa sababu tunafikiri atasahau. Ukweli ni kwamba Mungu anajibu kwa wakati, yuko makini kuliko wahudumu wa chumba cha watu mahututi.
Siku moja usiku baada ya kuona nyumba yangu imezingirwa na mambo yasiyofaa niliamua kumwita BWANA YESU na dakika ile ile shwari ilirejea. Namshangaa Mungu kwa maana amewapa mamlaka kuu wale wanaompigania. Hudson Taylor akijua fika atakwenda nchi ya mbali kwa uinjilishaji, alijifunza kumtegemea Mungu kwa kila jambo. Hata alipotaka pesa hakumwambia mkuu wake wa kazi bali alimwambia Mungu katika maombi. Ananukuliwa, “ni vema nijifunze kumwomba Mungu kwa kila jambo, maana huko China niendeko hakuna mtu wa kumwomba wala kumtegemea”.
Katika biblia tunaona Mungu amekuwa sauti ya wasio na sauti, amewakumbuka matabaka ya walioonewa. Yeye ni Mungu wa vita, anajua kupigana tena ameshinda vita zote. Kuomba ni kumchagua Mungu awe mwakilishi wako katika vita. Ndio maana biblia imeyaita maombi silaha. Waefeso 6:11
Uwezo wa mwanadamu unakikomo, hata akijitahidi hawezi kutuliza yote yanayomsonga. Taarifa ya habari si taarifa yenye habari za kutia tumaini bali ni taarifa yenye habari mbaya; mafuriko, njaa, migomo, ugomvi, kupunguzwa kazini, vifo na magonjwa.
Nakumbuka siku moja nilipopokea taarifa ya kutisha kwamba mpendwa wangu yuko mbioni kufa. Niliogopa sana! Moyo wangu ulizimia kwa hofu. Siku yangu ilikwenda mrama kabisa. Mara ghafla jioni rafiki yangu akanishauri na kutumia Zaburi 46:1-3. Na hapo nikapata nguvu, na hapo nikapata upenyo na hapo nikasimama tena. Na hapa nikajua kama ni vita si mimi nitakaye kufa, bali ni wenzangu ndio watafia nchi zao na falme zao.
“Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.” Zaburi 46:1-3
Nikamkimbilia Mungu kwa sala, tukashinda vita na mpendwa wangu akawa salama! Tishio la kifo, ajali, hukumu ya Mahakama, Waganga, Wachawi halina uwezo wowote kwa yule ajuaye kuliitia jina la BWANA, yule aliyepaka damu ya Yesu ya Pasaka.
Kujiambatanisha na Mungu ni kujiambatanisha na ushindi. Kama wakristo sisi ni washindi, maana tu uzao wa ushindi.
Mkimbilie Mungu ukiwa na cheti cha daktari, mwambie utaishi kwa neno lake wala si kwa chakula, wala si kwa neno la daktari. Ingawa tunaheshimu mchango wa kila taaluma lakini Bwana ndiye atakaya maneno yote, kwa kuwa Yeye ni mwanzo tena mwisho. Hata kama umetenda dhambi usisite kumwendea Mungu wakati wa changamoto yako. Yeye ni kimbilio wakati wa shida, shida zinaturejesha kwake.

Ili kufikia malengo yako

 
ILI KUFIKIA MALENGO YAKO
Kila mwaka mpya unapoanza watu wengi huwa na kawaida ya kujiwekea malengo katika mwaka husika. Karibu kila mtu au mahali huzungumia mipango au malengo anayotamani na kujipangia; Lengo ni kupata taswira ya mahali ambapo mtu anataka kwenda au kufanikisha katika mwaka huo. Hili ni jambo zuri kwa kuwa linaleta hamasa, nguvu na matumaini ya kusonga mbele katika maisha ya kila siku; kwa kuwa kama mtu hajui anapotaka kwenda (hana malengo au mipango) njia yoyote itamfikisha.
Changamoto moja ambayo hutokea ni kwamba watu wengi huwa na hamasa kubwa juu ya kuweka na kutamani kutimiza malengo yao mwanzoni mwa mwaka; lakini kadiri muda unavyozidi kwenda hamasa na nguvu ya kuyaendea malengo waliojiwekea hupungua au hutoweka kabisa. Na hivyo wanapofika mwisho wa mwaka wanagundua kuwa hawana kitu cha kuonesha au wanakitu kidogo tu ukilinganisha na malengo waliokuwa nayo wakati wanaanza mwaka.
Jambo hili tunaweza kuliona hata kwa wanaisraeli walipokuwa wanatolewa katika utumwa na kupelekwa katika nchi yao ya ahadi. Wakati wanatoka walikuwa na hamasa kubwa na nguvu na matumaini ya kufikia nchi ya ahadi; lakini kwa kadiri walivyokuwa wanaendelea na safari hamasa, matumaini na nguvu ya kufikia ahadi iliyokuwa mbele yao ilikuwa ikipungua kwa baadhi yao. Ukitizama safari yao utagundua kuwa kilichofanya hamasa na matumaini yao kupungua kadiri walivyosonga mbele, ni kitendo cha wao kuacha kuangalia (Paying attention) Ahadi na kuanza kuangalia changamoto walizokuwa wanakutana nazo njiani.
Je unapokutana changamoto katika mipango uliojiwekea katika mwaka huu, unachagua kuangalia nini? Unaangalia changamoto au unaangalia malengo yako? Ukitumia muda mwingi kutafakari changamoto uwe na uhakika hamasa na nguvu hupungua na hatimaye huweza kutoweka kabisa. Lakini ukitumia muda wako kutafakari malengo yako na kutafuta namna ya kufanikisha (Mfano; Kutafuta maarifa zaidi kwa kusoma vitabu au kurudi shule tena, kutenga muda mwingi zaidi wa kufanyia kazi jambo hilo, kutafuta ushauri, kujifunza kwa waliokutangulia/ waliofanikiwa, kurudia tena uliposhindwa mara ya kwanza n.k) uwe na uhakika mwisho wa mwaka au muda uliojiwekea  utakuwa na kitu cha kuonesha na sio maneno matupu ya kwanini ulishindwa.
Katika kufikia malengo au mipango uliojiwekea mwanzoni mwa mwaka au mwezi au kipindi chochote kile changamoto hutokea au naweza kusema haziepukiki kwa namna moja au nyingine. Changamoto ndizo zinatufanya tushangilie na kuwa na moyo wa shukrani pale ambapo tumefikia malengo hayo. Kumbuka jambo hili: Kama ni rahisi (hakuna changamoto) kila mtu angefanya. Changamoto haziji ili kufisha ahadi yako, bali zinakupa fursa ya kuona Ukuu na Utukufu wa Mungu kwa namna ambayo hujawahi kuona. Ni changamoto ya wanaisraeli ndio iliyofanya tutambue Mungu anaweza kufanya njia mahali pasipo na njia. Mtu hapewi tuzo kwa kusimulia namna changamoto zilivyomkwamisha; hupewa tuzo kwa kuonesha namna gani ameweza kufikia malengo yake katikati ya changamoto.
There’s a place for you at the top!

Kipaji chako ni hiki hapa

 
KIPAJI CHAKO NI HIKI HAPA
(Katika taabu ni rahisi kujua kipaji chako halisi)
Nani ni nani Tanzania, Kuna watu wanafuatana na utambulisho wao, Mchango wao na karama zao zimewatambulisha. Who is who in Tanzania? Sheikh Shaaban Robert amejulikana kwa mashairi, Askofu Moses Kulola amejulikana kwa injili, Rose Mhando amejulikana kwa nyimbo za injili. Wewe unautambulisho gani?
What is your Identity? Tunaposhindwa kujua utambulisho wetu kupitia karama na makusudi ya kuumbwa kwetu tunapoteza maana ya kuishi. Na hapa siku tukiimba vizuri tutafikiri sisi ni waimbaji na siku tukifundisha vizuri tutafikiri sisi ni walimu. Tatizo hili limewasumbua wengi na limekuwa likijulikana kama, The Crisis of Identity, ni hali ya kutokujua utambulisho wetu na mchango wetu kwa jamii.
Ukitaka kukosa mshindi katika mchezo wa mpira wa miguu usimpige refa bali ondoa magoli na hivyo kutakuwa hakuna sehemu ya kufunga na tayari mpira utapoteza ladha. Kingine unachoweza kufanya ni kuweka nguzo nyingi za magoli (yaani badala ya mbili weka nne). Malengo mengi maishani ni usumbufu. Kuwa na malengo mengi hakukupi nafasi ya kuwa mshindi ndio maana kila timu hufunga katika goli moja tu. Maisha bila ya kuwa na lengo kuu la kufanikisha hayana ladha. Ndio maana ni muhimu kujua kusudi lako na kipaji chako. 
Kipaji halisi hujidhihirisha wakati wa taabu, wakati ambao uko peke yako bila ya ulio wazoea. Unachopenda kufanya gizani bila ya kuhimizwa na mtu kinaweza kuwa kipaji chako nuruni. Kipaji cha ubondia hugunduliwa nje ya ulingo na ulingoni ni sehemu ya udhihirisho tu.
Yusufu alitabiri Gerezani, Paulo na Sila waliimba na kumsifu Bwana wakiwa gerezani mpaka milango ya Gereza ikafunguka. Je! kipaji chako kinadhihirika wakati wa shida? Kipaji halisi hakinyamazishwi na mazingira magumu.
Kipaji au karama ya Mungu huonekana hata katika taabu, Yesu aliendelea kuhubiri, kuponya na kuokoa hata akiwa msalabani. Don’t be silenced by problems
Nimeona Mungu akiponya kwa uponyaji mkuu katika mazingira ambayo sikuwa hata na utayari. Siku chache zilizopita tumeshuhudia Boss mkubwa aliyeachishwa kazi TANESCO akiendelea na kuhubiri injili. Kawaida ya kipaji halisi ni nyenzo inayotumika hata katika taabu, kamwe hainyamazi. Umri haunyamazishi kipaji chako, ana miaka 82 ya kuzaliwa bado Jimmy Swaggart anaimba, kupiga kinanda vizuri na kufundisha.
Wako wakimbizi waliotumia vipaji vyao ugenini, wako watumwa waliotawala utumwani. Wako wafanyakazi wa ndani walioishia kuwa wafalme. Ni baada ya kugundua vipaji vyao na kuvitumia hata katika mazingira magumu. Endelea kutumia kipaji chako usikate tamaa.
Mazingira magumu yanapaswa kukuhamasisha kutumia kipaji chako na si kukitelekeza kipaji chako. Kwa tafsiri yangu Paulo alimaanisha hivi, “…chochea kipaji ulichopewa na Mungu kilicho ndani yako.” 2 Tim1:6
Kileleni ndipo tunapopatikana

Siachi

 
SIACHI
(Dhambi ni kutelekeza kipaji chako)
“If you can’t walk then crawl. But whatever you do you have to keep moving Forward'” Martin Luther King Jr.
Katika siku za karibuni tumeshuhudia migomo ya watu wenye taaluma na vipaji mbalimbali. Kumekuwa na migomo ya walimu, madereva, madaktari na watu wa kada na tasnia nyingine tofauti tofauti. Migomo hii hulenga kuifanya jamii na serikali itambue mahitaji ya makundi haya kipekee, hususani tafsiri ya uwiano wa mchango wao kwa jamii na mishahara wanayolipwa.
Katika migomo yote, mgomo wa madaktari hutikisa zaidi, madhara yake ni dhahiri machoni pa wote. Watu hupoteza maisha, wagonjwa huteseka na ndugu zao hupoteza matumaini. Kama ilivyo kwa madaktari, yako madhara kwa kila mwenye kipaji ambaye ataacha kukitumia. Waathirika ni wale ambao Mungu alitaka wanufaike kwa kipaji chako. Ni wazi hakuna mto unaokunywa maji yake wenyewe. Yako madhara kama viongozi watajiuzulu bila msingi, yako madhara kama wahubiri watasimama na kuacha kuhubiri. Yesu alisema, atazamaye nyuma hafai kwa ufalme wake.
Dereva mwenye hekima akikimbia nafasi yake atafanya madereva walevi wapate ajira na kisha kuua watu kwa ajali isiyo na sababu. Kwa sababu ya wenye hekima kuogopa siasa, nchi zimeongozwa na mabaradhuli. Mchungaji akiacha kuombea kondoo shetani anawatafuna. Kuacha wajibu wetu ni dhambi, Samweli akasema, siachi…… 1Sam 12:23
Wizi, uzinzi, ulevi na uasherati si dhambi kubwa ukilinganisha na mhandisi kuacha kazi aliyoitiwa na Mungu. Dhambi kubwa ni mwimbaji wa kusifu na kuabudi kuacha huduma yake, mhubiri kuacha kuhubiri, kiongozi kuacha kuongoza.
Wewe kama ni ndege jielekeze katika kuruka na si kuogelea. Ni kwa faida yako, ukitaka kujua madhara ya kutokutumia kipaji chako jifunze katika vipaji ambavyo madhara yake yako nje kama vile udaktari au udereva, ambapo kosa moja hugharimu pumzi za watu.
Paulo alisema, “Ole wangu nisipo ihubiri injili”. Usipofanyia kazi kipaji ulichopewa na Mungu unafanya dunia iwe kama kibogoyo, maana pengo lako halitazibika. Uzuri wa dunia ni pamoja na mchango wa kipaji chako.
Jaribu kufikiri familia yenu bila ya wewe, kanisa lenu bila ya wewe, kazini kwako bila ya wewe kuwepo  kama hakuna pengo lolote katika kutokuwepo kwako ujue wazi hautumii kipaji chako. Imagine the World without Jesus Christ!
Mimi siachi kuhubiri, siachi kuimba, siachi siasa safi, siachi ufundi, siachi sanaa, siachi nasema siacha ubunifu wangu. Usiache karama yako ya maombi (1Sam 12:23); usiache biashara yako wala usidharau mwanzo wako mdogo, wala usipuuze wazo lako la ushindi. Kuendelea mbele inapaswa kuwa kama wimbo wako. Mungu Baba na akuimarishe katika kipaji na wito wako ulioitiwa, ukawe hodari; kama jua lisivyo acha kuangaza na wewe kwa kupitia kipaji chako ukaangaze milele kwa jina la Yesu Kristo. Amen
Kileleni ndipo tunapopatikana.

Unataka kufanikiwa katika nini - III

 
UNATAKA KUFANIKIWA KATIKA NINI - III
 “Success is predictable, so is the failure”
Unatumiaje muda wako wa ziada?
Moja ya jambo kuu linalotofautisha kati ya mtu aliyefanikiwa na watu wengine, ni namna wanavyotumia muda wao wa ziada. Mwenye hekima mmoja amewahi kusema, namna unavyotumia muda wako leo ndio uamua hatima yako ya kesho. Nioneshe unavyotumia muda wako wa siku, nikueleze hatima yako. Wote tuna masaa 24, wote tunamahitaji ya msingi yanayohitaji muda mfano. Kulala, kula, kusoma (darasani kwa mwanafunzi), kufanya kazi n.k, lakini swali langu la msingi kwako ni je unatumaije muda wako wa ziada?
Muda ni kitu cha ajabu sana, ukichagua kuutumia vizuri au kutoutumia kabisa, bado muda utapita. Ukiamua kulala siku nzima, muda hautasimama, chochote utakachoamua kufanya bado muda utapita; ukiamua kukaa tu bila kufanya chochote bado muda utapita; hata ukiamua kuvunja saa bado muda utapita. Hivyo ni muhimu kuzingatia namna tunavyotumia muda wetu. Kumbuka hauwezi kuhifadhi muda kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Leo nitagusia aina mbili za watu linapokuja swala la muda; kuna watu wanaopoteza muda na kuna watu wanaowekeza muda. Hivyo kila muda unaopita katika maisha yako, unakuwa umewekezwa au umepotezwa. Kitu kinachoamua kama umepoteza au umewekeza muda wako ni namna unavyoutumia muda huo. Katika mahojiano yake na jarida maarufu la nchini Marekani, Dr. David Oyedepo aliulizwa, unatumiaje muda wako wa ziada, akajibu “I use my time to read and think” yaani natumia muda wangu kusoma na kutafakari (personal development). Wewe na mimi tunatumiaje muda wa ziada?
Mfano; Ukisafiri umbali mrefu unafanya nini, unalala muda wote mpaka unafika? Unaangalia filamu na muziki wanaokuwekea mpaka unafika?!!!! Kwanini usibebe kitabu uwe unasoma wakati wengine wamelala? Kwanini usiweke mafundisho ya sauti kwenye simu yako ukiwa na spika za masikioni (earphones) wakati wengine wanasikiliza bolingo? Nina uhakika mpaka unafika mwisho wa safari yako utakuwa umemaliza sura mbili hadi nne za kitabu; na hapo tunasema umewekeza muda wako.
Au ukiwa kwenye foleni za mjini na umepata kiti cha kukaa, unafanya nini? Unalalamika kuhusu foleni mpaka unafika? Unachati mpaka unafika? Unalala? Au unatumia muda huo kujifunza ili uwe bora zaidi katika eneo unalotaka ufanikiwe? Embu tufikiri pamoja, mtu anayekaa kwenye foleni saa moja au mawili au zaidi kwa siku na kuishia kulalamikia foleni na serikali au kuchati, na mtu mwingine anatumia muda huo kujifunza (kitabu au mafundisho ya sauti kwenye CD kwa gari binafsi) namna ya kuwekeza katika biashara au ujasilimali au uwekezaji jambo lolote hata familia, huduma au kazini; unafikiri baada ya mwezi mmoja watu hawa watakuwa sawa kifikra? Baada ya miezi sita watakuwa sawa kimaisha? Au ukiwa nyumbani unatumiaje muda wako?  Kumbuka: Nioneshe unavyotumia muda wako, nikuoneshe hatima yako…. Wito wangu kwako leo ni kwamba, Anza kuangalia namna unavyotumia muda wako; tumia muda wako kuwekeza katika kuongeza ubora kwako binafsi (personal development) au kuongeza ubora katika eneo unalotaka kuona mabadiliko na mafanikio.
There’s a place at the top