Ububu wa Zakaria


UBUBU WA ZAKARIA.
(Bora asiyesema, kuliko anenaye yasiyostahili)
Kuzaliwa kwa Yohana mbatizaji kulikuwa kwa muujiza, maana wazazi wake walikuwa wazee sana na wenye kukoma katika kawaida za wanadamu. Zakaria aliposhindwa kuamini aliyoambiwa na BWANA alifanyika bubu. Kumwacha mwenye imani ndogo azungumze kunaweza kuharibu ushuhuda, hivyo ni bora afanyike bubu. Talk Faith! Luka 1:20
Biblia inasema Zakaria alifanywa bubu kwa sababu hakusadiki neno la Mungu (Luka 1:20). Asiye na imani hutamka mashaka wala hakuna uhai na uwezo wa kujenga katika maneno yake. Tumepewa vinywa kwa ajili ya kujibariki na kuwabariki wengine. Tumepewa vinywa kwa ajili ya kumkiri Mwokozi wetu na kuwajenga wanaotusikia. Kwa nini kuongea jambo ambalo ndani yake hamna tumaini, kwa nini kuzungumza jambo ambalo ndani yake imani tena ya nini tutamke lile ambalo si faraja.
Akiwajenga watoto wake mchungaji mmoja alisema, “Talk love, talk faith, talk hope and edify others” yaani, zungumzeni upendo, imani, tumaini na kuwajenga wengine. Ni afadhali ukae kimya kuliko kujilaani au kujiita mdhambi. Tunahesabiwa haki kwa maneno yetu, hatusaidii sana kujiita wenye dhambi, na kujiona watu duni.
Kristo alitimiza amri kumi hivyo kupitia Kristo kila aaminiye ametimiza amri kumi ndani ya Kristo. Hivyo basi si mara zote unapojiita mdhambi unapata rehema, kuna mara nyingine unajihukumu kwa sababu tu hauna imani ya kujiita mwenye haki.
John F Kennedy aliyepata kuwa Rais mwenye upekee wake nchini Marekani alisema, “The only reason to give a speech is to change the world” yaani “sababu pekee ya kutoa hotuba ni ili kuubalisha ulimwengu wetu” yaani kuufanya uwe bora zaidi na uwe mahala salama zaidi.
Hatuongei ili kufanya watu wapigane, hatuongei kuleta uchochozi. Yesu alipotukanwa hakujibu chochote badala yake alijikabidhi kwa Mungu. Aliamini Mungu anaweza kujibu mashambulizi hayo vizuri kuliko yeye. Tatizo wengi wetu hatumwamini tunaona tunaweza kujibu na kulipiza vizuri kuliko Yeye. Tunasahau kisasi ni juu ya BWANA na kwamba BWANA ni hodari wa vita.
Wako wale wasemao jino kwa jino au jicho kwa jicho, lakini sheria hii haiwezi kutekelezeka ikiwa aliyekutendea yu na nguvu kuliko wewe. Waefeso sita imeiita imani yetu silaha, imeiita pia maombi yetu silaha, kwayo tunaweza kushindana vema kuliko kwa matusi, dharau na majigambo.
Mungu akubariki sana!
Usikose msimu wa tano wa Weekend Purpose.

Jambo muhimu katika maisha - II

 
  JAMBO MUHIMU KATIKA MAISHA - II
Juma lililopita tuliangazia umuhimu wa kujijengea tabia ya kujitathimi mara kwa mara ili kupata fursa ya kuangalia au kuona kama aina au kiwango cha maisha anayoishi mtu; au muelekeo wa jambo fulani (kibiashara, kiroho au kikazi) ni sawa na matarajio (inavyotakiwa kuwa) yake au la! Mwenyehekima mmoja anasema, “Kama tutajitathimini juu ya aina au kiwango au uelekeo wa jambo lolote katika maisha yetu; lakini tusichukue hatua katika kile tulichojitathimini, muda utapita lakini kesho tutakuwa pale pale tulipokuwa jana na hivyo tutakuwa tumepoteza muda bure”.
Lengo la kujitathimini sio kujisikia vibaya au kuwa na hatia au aibu kwa mahali tulipo, bali kupata fursa ya kupiga hatua ili kesho tusiwepo mahali tulipokuwa jana au tulipo leo. Kama mwana mpotevu angejitathimini bila ya kuchukua hatua ya kutoka mahali alipokuwa kama matokeo ya kujitathimini kwake, basi kujitathimini kwake kusingeleta badiliko lolote katika maisha yake. Kumbuka, hakuna jambo hubadilika lenyewe. Mpaka umechukua hatua dhabiti, kutamani kuwa na mbadiliko pekee hakutabailisha kitu.
Mambo mawili nataka nikuhimize katika mapumziko ya mwisho wa wiki hii:
i. Chukua hatua kwa kuanza kujitathimini kwanza, kusoma ujumbe huu pekee hakutoshi; tunatamani kuona badiliko la kweli katika maisha yako, tunatamani kuona unafikia malengo yako na kilele cha mafaniko yako. Ndio maana tunakuhimiza chukua hatua, tafuta muda wa kujitathimini, zima redio, weka simu mbali, zima TV, acha ‘kuchat’ na ujitathimini. Kumbuka TV, Internet na Redio hufanyakazi masaa 24, hakuna siku watazima ili kukupa fursa ya kujitathimini; kila siku utasikia “mpenzi mtamaji/msikilizaji endelea kuangalia/kusikiliza kipindi kinachofuata”, hata kama ni saa nane usiku bado watasema endelea tu.
ii. Chukua hatua kwa kufanyia kazi matokeo ya tathimini yako kwa kuzingatia maswali muhimu ya kujiuliza yaliyopo kwenye toleo lililopita. Swali moja wapo lilisema: je, kwa sasa nikichukua maamuzi/hatua (actions) gani yatakuwa ni mwanzo wa mabadiliko katika maisha yangu? Mfano: kutoka katika mahusiano, kuomba msamaha, kutafuta kazi nyingine, kutafuta mshauri mwenye hofu ya Mungu anishauri, kujiunga na shule/kozi n.k!
Mwenyehekima mmoja anasema, “Watu hawafanikiwi kwa sababu wana mawazo mazuri; bali kwa sababu wanayafanyia kazi kwa wakati” Kufanya tathimini pekee hakutoshi, chukua hatua na kuyafanyia kazi kwa wakati ili kupata matokeo yaliyo bora zaidi.
There’s a place for you at the top

Jambo muhimu katika maisha

  JAMBO MUHIMU KATIKA MAISHA
Mafanikio katika jambo lolote kwenye maisha ya mtu si jambo la bahati nasibu; mafanikio huja kama matokeo ya kufuata au kutekeleza kanuni muhimu katika maisha ya mtu. Jambo moja wapo muhimu (kanuni) katika maisha ya mtu ili kufikia kilele cha mafanikio yake ni kujijengea tabia ya kujitathimini mara kwa mara ili kupata fursa ya kuona kama kile unachokifanya au kiwango cha maisha unayoishi ni sawa na kile ulichopanga au kutarajia.
Mwenyehekima mmoja amewahi kusema, maisha yasiyokuwa na kujitathimini ni maisha matupu (void). Si watu wengi wamejijengea tabia hii ambayo ni kanuni muhimu sana ili kufikia mafanikio halisi katika jambo lolote. Nioneshe mtu anayejitathimini mara kwa mara, nikuoneshe mtu anayefanikiwa katika njia zake.  Mfano mzuri wa kanuni hii muhimu katika maisha ni habari ya mwana mpotevu, ambaye aliishi maisha nje ya kile alichokusudiwa mpaka pale alipoamua kufanya jambo muhimu la kutathimini aina na kiwango cha maisha aliyokuwa anaisha. Kumbuka kila kitu huwa sawa mpaka pale umesimama na kujitathimini. (Luka 15)
Kujitathimni kunatoa fursa muhimu sana katika maisha katika maisha ya mtu. Kujitathimini kunaweza kufanyika wakati wowote ule, mwanzo wa mwaka au mwisho wa mwaka au katika ya mwaka au kila mwezi kulingana na malengo uliyojiwekea na mazingira uliyonayo. Kujitathimini kuna faida nyingi ikiwemo faida saba (7)zifuatazo:
i. Kujitathimini kunakupa fursa na kuamsha (renew or rejuvenate) hamasa (passion) na kukupa nguvu katika kile ulichokuwa unafanya au kuchukua hatua katika kile unachotakiwa kukifanya ili kufikia kilele cha mafanikio katika jambo husika.
ii. Kujitathimini kunakupa fursa na nafasi ya kuangalia malengo na vipaumbele vyako ili kuona kama vinaendana au vitakufikisha katika mafanikio unayoyatazamia.
iii. Wakati mwingine kujitathimini kunakupa fursa ya kujitambua zaidi na kuanza upya ili kujinasua mahali ulipokuwa umekwama.
iv. Kujitathimini kunakupa nafasi ya kuona rasilimali na fursa (opportunities) zinazokuzunguka ili upate  kuzitumia na kukufikisha katika malengo makuu.
v. Kujitathimini kunakupa nafasi ya kuziona fursa badala ya vikwazo katika changamoto au mazingira uliyonayo.
vi. Kujitathimini kunakupa fursa ya kutambua ni maeneo gani unayohitaji msaada (assistance) na mahali pa kupata msaada huo ili kukuwezesha kufikia malengo yako.
vii. Kupata fursa ya kuona kama kile unachokifanya au kiwango cha maisha unayoishi ni sawa na kile ulichopanga au kutarajia
Njia thabiti ya kujitathimini katika jambo lolote ni kwa kujiuliza maswali muhimu. Hii itakupa fursa ya kuona aina na kiwango ulichopo au mwenendo wa jambo husika; yafuatayo ni baadhi ya maswali muhimu unapojitathimini hasa katika kuangali aina na kiwango cha maisha uliyonayo sasa (Kiroho, kibiashara, kifamilia,kiuchumi,  kiofisi n.k):
i. Hivi ni kwanini naishi maisha ya namna hii kwa sasa? Je ningependa kuendelea na maisha haya hadi nitakapozeeka ama nataka kubadilika? (kutoka kitabu cha Timiza Malengo yako, Joel Nanauka)
ii. Je hivi aina na kiwango cha maisha ninayoishi ni sawa na kile nilichopanga au kutarajia (plan)
iii. Je hiki ninachokifanya kinachangia katika kufikia malengo yangu ya kimaisha?
iv. Je ni jambo gani naweza kufanya ili kuongeza ufanisi na ubora katika kile ninachokifanya? Kitu gani naweza kuboresha zaidi ili kutoa huduma au bidhaa bora zaidi ya sasa?
v. je, kwa sasa nikichukua maamuzi gani yatakuwa ni mwanzo wa mabadiliko  katika maisha yangu? Mfano: kutoka katika mahusiano, kuomba msamaha, kutafuta kazi nyingine, kujiunga na shule/kozi n.k (kutoka kitabu cha Timiza Malengo yako, Joel Nanauka)
“There’s a place for you at the top”

Kwa mara ya mwisho

 
KWA MARA YA MWISHO
[USIPOZUIA LEO HUWEZI KUZUIA KESHO]

Inaweza ikawa ni ahadi ya uongo, kujiahidi kupita uwezo wetu wa utendaji. Ngoja nile kwa mara ya mwisho, ngoja ninywe kwa mara ya mwisho, ngoja niende kwa mara ya mwisho, ngoja nikakae naye kwa mara ya mwisho. Tunaweza kushinda jaribu la kesho leo, kamwe huwezi kushinda jaribu la kesho bila ya kushinda leo.
Inawezekana unajitahidi kupunguza ulaji wa sukari, inawezekana unajitahidi kuacha kilema fulani au unahitaji kupunguza kiasi cha unywaji wa soda. Unaweza tu kwa kuondoa urasimu wa mpaka kesho, mpaka mwezi ujao au mpaka juma lijalo. Usianguke leo ili usimame kesho, badala yake simama leo ili kesho usimama imara zaidi. Mwenye hekima mmoja anaandika: “Giving in even once weakens our ability to resist next time”
Hujachelewa bado, wala haujaharibika kabisa, you are not beyond repair! Usijikatie tamaa mabadiliko yanawezekana. Siku 365 za mwaka ni fursa 365 za kubadilika. Neema ipo kila asubuhi kwa hiyo unaweza kubadilika bila shaka. 
Kuna nyakati huwa najiona niko chini (very down) kwa sababu ya dhambi, makwazo, majaribu na pengine kiburi changu dhidi ya neno la Mungu. Lakini huwa najitia moyo nikiwa na hakika kwamba, Mungu hakuniumba ili anihukumu bali ili aniokoe na kunipa uzima wa milele katika YESU KRISTO. Nikikumbuka neno hili huwa nafarijika sana, Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo;” 1Wathesalonike5:9
Kuna mwingine anaweza akasema Mungu anajua tutakwenda jehanamu, kwa hiyo hakuna haja ya kufanya jitihada. Wazo hilo si la kweli, Mungu anajua utakwenda mbinguni kwa hiyo fanya jitihadi za kumtafuta.  1Watheselonike 4:9 inaweka wazi kwamba Mungu hakutuumba kwa ajili ya hukumu.
Yesu aliposema, haombi kwa Baba atutoe ulimwenguni bali atulinde na yule mwovu alimaanisha, Changamoto zipo, na hakuna aliyekingiwa changamoto (no one is immune to challenges) sote tunapaswa kupambana na kushinda. Unapotatua changamoto moja unatengeneza kinga ya kukusaidia kupambana na changamoto nyingine, ndivyo wasemavyo wenzetu kwamba; “bahari shwari haitoi wanamaji shupavu.” Utapitia mengi katika bahari ya maisha; ila uwe na hakika Mungu anakuwazia mema na mwisho wake utatoka katika bahari ya maisha ukiwa shupavu na hodari. Yako mateso na ziko changamoto, yote hayo yapo ili kufanya uwe bora zaidi na uwe shujaa zaidi.
Bila jangwa huwezi kuwa na Musa mpole na mtaratibu, bila ubaguzi wa rangi huwezi kuwa na Nelson Mandela mwenye kusamehe na mwenye heshima; bila ya kufeli au kuishia njiani ki-masomo tusingelipata watu bora kama Bill Gates ambao laiti wangefaulu masomo yao vizuri na kuhitimu wangekuwa waajiriwa wala wasingeliweza kujiajiri na kuajiri maelfu kama walivyo sasa.
Endelea mbele Yesu Kristo yu hai kwa ajili yako. Shallom……

Bado hujawa tayari kuoa

 
BADO HUJAWA TAYARI KUOA.
(MANENO YAKO YANAAMUA HATMA YAKO)
Si rahisi kufahamu mtazamo wa mtu kama hajatamka chochote, si rahisi kujua mawazo ya mtu asipoyaweka katika maneno. Maneno yetu huonesha hatma yetu. Your words determine your reach!
Maneno yetu huelezea msimamo na uelekeo wetu juu ya jambo fulani. Kuna baadhi ya maneno mtu akitamka unaweza kujua hali inayojiri moyoni mwake. Yafuatayo ni baadhi tu ya maneno yanayooenesha kwamba mtu hayuko tayari kwa kuolewa au kuoa.
Wanawake wote ni sawa. Kitendo cha kusema wanawake wote ni sawa ni hatua inayo onesha mtazamo mbaya dhidi yao. Kwambo wote ni waovu, au wote hawafai. Mtu mwenye mtazamo huu hafai kwa kuoa. Hata biblia imetanganisha wako iliyowaita mke mwema na kuna wengine imewaita kahaba. Wako wazuri na wema kama Abigaili, na unapaswa kumwomba BWANA ili upewe mke mwema. “Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato. Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake.” Mithali 31:11-12
Mwanamke atanisaidia nini? Mtu anayefikiri anajitosheleza mwenyewe (self centered and self consumed) na asingehitaji msaada wa mwingine hafai kwa kuungana naye. Kama hauoni umuhimu wa nafasi ya mke katika kukusaidia kibiblia na kijamii basi usioe. Ni yule anajua umuhimu wa nafasi fulani ndiye anayeweza kuipigania hata nyakati za changamoto kali. Ni Mungu aliyesema, Si vema mwanaume awe peke yake, wala si mwanadamu aliyenena hayo. Kama haikuwa vema pale Edeni basi ujue si vema hata sasa uwe peke yako. Mwanzo 2:18
Wanawake hawaokoki. Hili nalo si jambo jema. Nimewahi kumsikia rafiki yangu mmoja akilisema na akinukuliwa na rafiki yangu mwingine. Rafiki yangu huyu ameoa mwaka jana,sasa sijui kwa nini kaoa. Katika ndoa mwanamke ni kama udongo ambao mwanaume anapanda maisha yake (Sow your life) na kinyume chake kwa wanawake. Asiyeokoka maana yake asiye zaliwa mara ya pili au asiyeamini, Sasa kwa nini upande maisha yako kwa mtu asiye amini? Ingawa wanaume huwa na msimamo imara sana katika imani na maamuzi lakini bado wokovu si swala la kijinsia bali ni swala la imani. Luka 8:4
Ataniharibia huduma? Naamini uharibifu katika muungano unaweza kufanywa na mtu yeyote aliyesehemu ya muungano huo. Kusema ni upande fulani tu si sawasawa, kwani kwa kufanya hivyo upande mwingine unakuwa ni kama upande wa Malaika. Ni jambo jema kama pande zote zitalenga na kujizatiti kusaidia mafanikio ya kiroho ya upande mwingine kiroho. Mithali 31:11-12
Tunakuwa salama sana pale ambapo fikra zetu zinakuwa sawasawa na neno la BWANA. Pale tunapowaona wengine ni bora kuliko sisi tunaonesha ukomovu wa akili na imani. Tunakuwa wenye hekima sana tunapoacha kuwahukumu watu kwa rangi zao, jinsia zao, kabila lao na nchi zao. Imeandikwa “wote” yaani nchi zote, makabila yote na lugha zote. Warumi 3:23 “Kwa sababu wote, wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu”
Tukutane katika msimu wa tano wa “weekend of purpose” hapo mwezi May jitahidi ufike, yako mengi mazuri yanaandaliwa kwa ajili yako mteule wa BWANA. Barikiwa.