Bado hujawa tayari kuoa

 
BADO HUJAWA TAYARI KUOA.
(MANENO YAKO YANAAMUA HATMA YAKO)
Si rahisi kufahamu mtazamo wa mtu kama hajatamka chochote, si rahisi kujua mawazo ya mtu asipoyaweka katika maneno. Maneno yetu huonesha hatma yetu. Your words determine your reach!
Maneno yetu huelezea msimamo na uelekeo wetu juu ya jambo fulani. Kuna baadhi ya maneno mtu akitamka unaweza kujua hali inayojiri moyoni mwake. Yafuatayo ni baadhi tu ya maneno yanayooenesha kwamba mtu hayuko tayari kwa kuolewa au kuoa.
Wanawake wote ni sawa. Kitendo cha kusema wanawake wote ni sawa ni hatua inayo onesha mtazamo mbaya dhidi yao. Kwambo wote ni waovu, au wote hawafai. Mtu mwenye mtazamo huu hafai kwa kuoa. Hata biblia imetanganisha wako iliyowaita mke mwema na kuna wengine imewaita kahaba. Wako wazuri na wema kama Abigaili, na unapaswa kumwomba BWANA ili upewe mke mwema. “Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato. Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake.” Mithali 31:11-12
Mwanamke atanisaidia nini? Mtu anayefikiri anajitosheleza mwenyewe (self centered and self consumed) na asingehitaji msaada wa mwingine hafai kwa kuungana naye. Kama hauoni umuhimu wa nafasi ya mke katika kukusaidia kibiblia na kijamii basi usioe. Ni yule anajua umuhimu wa nafasi fulani ndiye anayeweza kuipigania hata nyakati za changamoto kali. Ni Mungu aliyesema, Si vema mwanaume awe peke yake, wala si mwanadamu aliyenena hayo. Kama haikuwa vema pale Edeni basi ujue si vema hata sasa uwe peke yako. Mwanzo 2:18
Wanawake hawaokoki. Hili nalo si jambo jema. Nimewahi kumsikia rafiki yangu mmoja akilisema na akinukuliwa na rafiki yangu mwingine. Rafiki yangu huyu ameoa mwaka jana,sasa sijui kwa nini kaoa. Katika ndoa mwanamke ni kama udongo ambao mwanaume anapanda maisha yake (Sow your life) na kinyume chake kwa wanawake. Asiyeokoka maana yake asiye zaliwa mara ya pili au asiyeamini, Sasa kwa nini upande maisha yako kwa mtu asiye amini? Ingawa wanaume huwa na msimamo imara sana katika imani na maamuzi lakini bado wokovu si swala la kijinsia bali ni swala la imani. Luka 8:4
Ataniharibia huduma? Naamini uharibifu katika muungano unaweza kufanywa na mtu yeyote aliyesehemu ya muungano huo. Kusema ni upande fulani tu si sawasawa, kwani kwa kufanya hivyo upande mwingine unakuwa ni kama upande wa Malaika. Ni jambo jema kama pande zote zitalenga na kujizatiti kusaidia mafanikio ya kiroho ya upande mwingine kiroho. Mithali 31:11-12
Tunakuwa salama sana pale ambapo fikra zetu zinakuwa sawasawa na neno la BWANA. Pale tunapowaona wengine ni bora kuliko sisi tunaonesha ukomovu wa akili na imani. Tunakuwa wenye hekima sana tunapoacha kuwahukumu watu kwa rangi zao, jinsia zao, kabila lao na nchi zao. Imeandikwa “wote” yaani nchi zote, makabila yote na lugha zote. Warumi 3:23 “Kwa sababu wote, wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu”
Tukutane katika msimu wa tano wa “weekend of purpose” hapo mwezi May jitahidi ufike, yako mengi mazuri yanaandaliwa kwa ajili yako mteule wa BWANA. Barikiwa.

Mimi ni mchezaji wa timu ile

 
MIMI NI MCHEZAJI WA TIMU ILE.
(I belong to a winning team) 
Kwa mfano huu jifunzeni. Lauden alikuwa mchezaji mahiri wa timu yake ya kidato cha tano, alijituma sana na kujizuia ili kufanikisha ushindi. Siku moja kabla ya fainali Lauden alilala mapema ili kupata muda mwingi wa kupumzika na kujiandaa na fainali. Baadhi ya wanatimu walikwenda disko kucheza muziki na hivyo walichelewa kulala, wengine walikwenda mitaani katika mambo ya uasherati na ulevi. Licha ya bidii na juhudi za Laudeni katika kujikatalia anasa na kulala mapema bado timu yao haikufua dafu. Juhudi za Laudeni hazikufua dafu, timu yake ilishindwa mbele ya mahasimu wao. Ingawa Laudeni alionekana kuwa mchezaji wa kipekee katika mchezo, bado hakuweza kuisaidia timu yake kushinda.
Wapinzani wao hawakuwa na vipaji vikubwa, ila walikuwa na umoja. Wapinzani wao walizingatia maelekezo na kufanya inavyowapasa kwa pamoja kama timu. Wapinzani wao walielezea kuwa siri ya mafanikio yao ni umoja na ushirika katika mazoezi na mtazamo.
Timu nyingi hazifungwi kwa sababu ni mbaya, bali ni kwa sababu ya utengano. Tunaweza kuwa na umoja ndani ya uwanja na utengano nje ya uwanja hii nayo haifai. Utengano katika mtazamo, maneno na matendo ndio chanzo cha kushindwa. Umoja ni muhimu uwanjani na nje ya uwanja. Mhubiri mzuri haonekani jukwaani bali nyumbani. Ni nje ya uwanja ndipo hutoa jibu la kinachoonekana uwanjani.  Kwa wanafunzi muda wa likizo ndio unaoamua ushindi, ni muda ule ambao mwalimu hajakupangia jambo la kufanya.
Timu ikishinda ushindi ni wa kila mtu, na ikifungwa basi ni wote wameshindwa wala si mlinda mlango peke yake. Ushindi ni jambo la pamoja. Si sahihi kwa mwanatimu kufikiri anaweza peke yake wala si sahihi kwa mwanatimu kufikiri kwamba hana mchango wowote. Tamko la timu ni bora kuliko tamko binafsi
John Maxwell ambaye ni mwalimu mzuri wa uongozi anasema, “moja ni namba ndogo sana kufanya mambo makubwa.” waswahili nao wanasema, “kidole kimoja hakivunji chawa.” Wote wanasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja na kwa umoja kama timu. Biblia inasema, wawili ni bora kuliko mmoja, tena inasisitiza kwamba, Si vema mtu awe peke yake ndio maana akamfanyia msaidizi.
Utengano hutokea pale mmoja anapoacha kutimiza wajibu wake. Timu haifungwi kwa sababu nafasi zote zimeyumba la hasha! Bali ni kwa sababu nafasi fulani imeyumba. Inawezekana ikawa ni nafasi ndogo lakini ndio chanzo cha kuyumba kwa timu. Kila mchezaji ni muhimu katika timu. Oral Robert katika moja ya vitabu vyake anaelezea umuhimu wa mgawanyo wa kazi kwa kuzingatia karama na talanta za mwanatimu. Oral anamnukuu rafiki yake Bob De Weese aliyemwambia maneno haya; “Oral, you be there to preach and pray, and your team will do the rest.
Kwa nini tunapungukiwa baadhi ya mambo maishani mwetu? Moja ya sababu ni ili tujue kwamba mwanadamu ni kiumbe wa mahusiano. Katika kuhusiana na wanatimu, wanajumuiya na wanajamii wengine anakamilika. Timu ni muhimu, mizizi ya timu huenda mbali kuliko juhudi za mtu mmoja, bila ya timu tunaweza kukamilisha kazi kidogo. Yesu alikuwa na wanafunzi wake, Paulo alikuwa na Timotheo na Tito, Sauli alikuwa na Daudi na nabii Nathani. Vipi uko na nani? Bill Gates na Hayati Steve Jobs walikuwa na timu zao za ushindi. Nina amini hata Dangote na yule Strive wa Kwese Tv wana timu zao za ushindi.
Si rahisi mtu asiye na timu na ushirika na watu wengine akawa na ushirika na Mungu. Kuna nyakati ambazo kuwaacha watu maana yake ni kumwacha Mungu. Si kila asiye na kikundi ni wa kiroho. Mwezi uliopita tuliandika andiko fulani, tuliowaandikia walituuliza kama tunafanya kazi kama timu au lah! Tunamshukuru Mungu tunafanya kazi kama timu ya, Life Minus Regret Team, tazama wasifu wa timu yetu (team profile) katika: www.lifeminusreget.blogspot.com
Jisikie furaha kuwa sehemu ya timu fulani, usharika fulani, jumuiya fulani au kanisa fulani. Televisheni si kanisa, lengo lake ni kuwaleta watu kanisani na si kuwaacha sebuleni na rimoti zao. Unahitaji kukutana na watu waaminio kwa ajili ya ibada, kumega mkate na kuwajua wahitaji wanao hitaji msaada wako.
Endelea kuifurahia timu yako ya ushindi. Barikiwa!!!

Malezi ni mkataba mrefu

 
MALEZI NI MKATABA MREFU.
(Ni zaidi ya miaka 18)
Mwanadamu ni kiumbe anayekaa katika utegemezi kwa muda kuliko watoto wa viumbe wengine. Viumbe wengine hulea watoto wao kwa miezi sita au mwaka mmoja na kisha huwaacha wakaendelee na maisha yao.
Ndege hukaa na makinda yao kwa miezi mitatu, wako wanyama wengine hukaa na watoto wao kwa kipindi ambacho ni chini ya mwaka mmoja. Lakini sivyo ilivyo kwa binadamu. Malezi ya mtoto ili mtu awe mtu kamili yanachukua zaidi ya miaka 18. Fikra za kupata mtoto lazima ziende mbele angalau kwa miongo miwili (miaka 20). Mtoto wa binadamu anakaa nyumbani kwa zaidi ya miaka 18 akiwa bado ni tegemezi. Wako wenye miaka zaidi ya 30 na wanalishwa na kutunzwa na wazazi wao. Malezi ni zaidi ya chakula na dawa. Ni kuadabisha na kufundisha utu wema. Mith 21:6
Mkataba wa kupata mtoto hautakiwi kuwa wa usiku mmoja, mkataba wa kupata mtoto unapaswa kuwa mkataba unahusishwa elimu, utu, makuzi, na hatma ya mtoto kwa mioungo isiyopungua miwili. Uamuzi wa kupata mtoto ni lazima uwe ni mkataba wa milele, au uwe mkataba wa zaidi ya miaka 18. Wenye utayari wa kupata mtoto lazima wawe na utayari wa malezi ya pamoja kwa zaidi ya miaka kumi na nane. Kifo ndio sababu rasmi sana ya kibiblia ya kumfanya mtu alelewe na mzazi mmoja, japo kijamii ziko sababu nyingi.
Pamoja na changamoto zote za malezi, mzazi mmoja au wawili bado kulea ni kuzuri kunampa mzazi au mlezi nafasi ya kukijenga kizazi kinachofuata. Katika ujenzi wa Taifa, familia ni sehemu ya kwanza na ya msingi.  Shule ya familia inatajwa kuwafanikisha wengi kuliko vyuo vikuu.
Shule ya familia ikikosewa inaweza kuwafelisha wengi kuliko wanaofeli katika madaraja mbali mbali ya elimu. Familia isipowajenga watoto kwamba matatizo yapo, basi watakapo kutana nayo watakata tamaa. Familia isipoamini katika uwepo na uhusiano na Mungu, basi watoto wataabudu vitu ambavyo kwa asili si Mungu.
Watoto wasiojengwa katika ibada wanaweza wasimwabudu shetani badala yake wakaabudu kazi, fedha, sinema na michezo. Rafiki yangu alipenda ibada kiasi kwamba alikuwa hakumbuki ni lini hakuudhuria ibada kanisani, lakini tunao vijana wengi ambao hawakumbuki ni lini walikwenda kanisani. Makosa haya ni ya mfumo wa malezi.  
Malezi ni jambo la pamoja mzazi hatoshi peke yake wala hapaswi kufikiri kwamba anatosha. Ndio maana Mungu amwetuwekea kanisa. Kanisa ni jumuiya ya waaminio ambapo ndani yake kuna walimu, wainjilisti, wachungaji, mitume, manabii na watu wenye matendo ya miujiza. Mtoto ni wa Mungu kwanza, wa wazazi na baadaye wa jamii yote.
Hitler kabla ya kuwa muaji alikuwa mtoto, Iddi Amini wa Uganda kabla ya kuwa dikteta alikuwa mtoto. Mtoto ni kama karatasi nyeupe isiyo na kitu chochote, mwandishi wa awali ni Mungu na baadaye wazazi wanapata nafasi ya kuandika upendo au ugaidi, amani au chuki, uvumilivu au kisasi.  Mithali 21:6

Mfumo wa zawadi

 
MFUMO WA ZAWADI.
(Nitapata nini? Mathayo 19:27)
Mwanadamu anafanya kazi kwa mfumo wa zawadi (Reward system). Wana raha sana wanaotumia mfumo huu ambao Mungu pia huutumia. Unapopanga malengo yako usisahau kujipa zawadi. Usisubiri watu watambue juhudi zako, wewe pia jitambue na jipongeze. Ikiwa nitafikia lengo fulani nitasafiri wakati wa majira ya joto kwenda mapumziko. Nikifanya kazi kwa bidii na kuzalisha vya kutosha nitakwenda kutembea hifadhi za taifa.
Mfumo huu ni mzuri hata kwa mahusiano ya wazazi na watoto. Ukimaliza kazi ya nyumbani nitakuruhusu utazame sinema, ukimaliza chakula nitakupeleka zuu (zoo) ukatazame wanyama. Mfumo huu unachagiza kutimia kwa malengo. Unamfanya mtu apende utendaji wake.
Wataalamu wengi wa sayansi na saikolojia wanaamini wazi kwamba, kuna furaha na nguvu mpya anayoipata mtu akiwa atapata motisha, atapandishwa cheo, atapongezwa au kufarijiwa kwa kazi yake njema. Si rahisi mtu kufanyakazi kwa bidii na ufanisi ikiwa anajua hatapata chochote kama taji, kutambuliwa na kukubalika, kupandishwa ngazi au kupewa fedha. Usiweke malengo bila zawadi, usijitaabishe bila ya kujiahidi furaha.
Akili ya mwanadamu hufikiri kwa picha, anapofanya kazi picha ya motisha au zawadi tarajiwa huwa akilini mwake. Kufanya kazi bila kujua utakacho pata huleta uchovu. Inatia moyo kufanya kazi ambayo matokeo yake ni dhahiri. Wanadamu wanapenda kujua watakachopata, Petro alimuuliza Yesu, “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?” Mathayo 19:27
Wakati mwingine si rahisi kuwalipa watu kwa fedha lakini tunaweza kutambua mchango wao na kuukubali. Na si wakati wote mtu anastahili kupata malipo chanya wakati mwingine anapaswa kupewa adhabu. Kanani kwa watii na Misri kwa wasiotii. Usijipongeze kwa kurudi nyuma, usile kwa anasa siku ambayo biashara yako haijazalisha faida. Jipongeze pale tu unapoona unastahili, wakati mwingine jipe adhabu ili utimize lengo. Haifai kuvuna tusipopanda. Reward for compliance and punishment for failure.
Baada ya kazi ngumu ni vema kujipa pumziko kama zawadi, ni vizuri kubarizi kando ya mito na bahari ili kuipa akili uwezo wa kuunganika na asili ya dunia. Mungu hutoa kazi na motisha, ni ajabu sisi tunasahau. Alipoamuru kutii alisema tutakula mema ya nchi, alipoamuru utoaji aliahidi Baraka hata pasipokuwepo nyumba yenye ukubwa wa kuchukua Baraka hizo.
Nikiwa Tabora mwaka 2013 na 2014 nilijifunza jambo la msingi kutoka kwa Michael Mambo, rafiki yangu huyu anayemiliki shule alikuwa akitoa kiasi fulani cha pesa katikakati ya mwezi (mid Month) kiasi hiki kilikuwa kikitoa motisha kubwa kwa walimu kwani hakikuwa sehemu ya mshahara wala hakikuwa sehemu ya mkataba bali ilikuwa ni motisha tu kwa watumishi. Wengi walijisikia kuhuishwa na kupata nguvu ya kazi baada ya kupata kiasi hiki. (Mid month package)
Jiahidi zawadi, itakupa hari na hamasa ya kutimiza malengo yako uliyoyaandika. Endelea kubakia kileleni.
Waunganishe rafiki zako katika mpango huu kwa kututumia email zao au kwa kuwaomba watembelee blog yetu na kujiunga. www.lifeminusregret.blogspot.com

Wito binafsi


WITO BINAFSI.
(Umeitwa kwa jina lako)
Wakristo, wanafunzi, wachungaji, waimbaji, wainjilishaji, wafanyakazi, wataalamu, wanaharakati n.k, ni majina ya vikundi ambayo hayatoi wajibu mkubwa kwa mtu binafsi. Ukweli ni kwamba wito ni ile sauti inayokuhamisha kutoka katika kikundi fulani, nchi yako, mipango yako binafsi na hata katika mwelekeo binafsi.
Wito si jambo jepesi, unaweza ukuleta usumbufu. Wito unahitaji aliyeitwa awe shupavu katika kukata kona (kuitikia wito), awe na uwezo wa kugeuka haraka. Pale mwanafunzi anapoteseka miaka zaidi ya mitano katika masomo yake ili awe daktari na baadaye sauti ya Mungu inamwita katika mwelekeo mwingine tofauti na udaktari, kunahitajika ushupavu na usikivu. Pamoja na kuwepo kwa gharama ya usumbufu, wale wanaotii sauti ya Mungu baadaye hufurahi na kufaidika.
Kuna wito ambao Mungu anamwita kila mtu, wito huu huhusisha aina na mtindo wa maisha tunaopaswa kuenenda nao hapa duniani. Uko wito wa kuishi maisha matakatifu, uko wito wa wokovu uko wito wa kumfuata Yesu yaani ufuasi. Wito wa ujumla haubagui kila mtu lazima aitikie sauti hiyo.
Katika makala hii ninalenga wito wa kipekee, wito ambao hauhusishi mke wala mume, hauhusu kikundi fulani cha watu bali unahusu mtu binafsi. Ameandika mchungaji mmoja, “Yuko wapi mke wa Petro?” Hatutazamii kumuona mwingine katika wito wako bali wewe peke yako.  Ibrahim aliacha nchi, baba na nduguze kwa ajili ya wito. “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.” Yohana 21:15
Yesu alimwita Petro kwa jina, na alimpa kazi kwa jina. Alimwita mara tatu kwa jina lake. Badala ya kusema mitume alisema, Simoni Petro lisha kondoo zangu, Baadaye akamtaja kwa jina kwamba, achunge kondoo zake.
Watu wenye wito wa pekee mara nyingi wanashangaa kwa nini hawasaidiwi au kupunguziwa mzigo, mara nyingi wanajiuliza, “kwani watu wengine hawaoni umuhimu wa jambo hili?” Yesu alipokuwa akiomba alishangaa mitume wake wakilala usingizi, alijaribu kuwaamsha mara kadhaa lakini bado walilala. Ninaamini ni kwa sababu wito wa wokovu si wa kwao, ulikuwa ni wa Yesu Kristo peke yake. Kwenye familia kunaweza kukawa na watoto wengi lakini si wote wanakuwa na mzigo wa kuwasaidia ndugu na jamaa, mara nyingi mzigo wa kusaidia wazazi na ndugu unaweza kumwangukia mmoja. Mwenye mzigo huo (wito wa kusaidia) huwa anatamani apate msaada na mara nyingi haiwi hivyo kwa kuwa ameitwa kwa jina lake.
Ili kijana afanikiwe ni muhimu ajue wazi kwamba kati ya vijana bilioni 1.8 waliopo duniani ni yeye tu ameitwa tena kwa jina lake. Ili mtu mwenye wito wa pekee afanikiwe ni lazima ajue kwamba katika dunia hii yenye watu bilioni nane ameitwa peke yake, tena kwa jina lake. John Wesley akitambua hili alisema, “Naona dunia nzima kama parokia yangu”.
Endelee kubakia kilele…..mpaka wiki ijayo shalom.