Mbona umeacha

 
MBONA UMEACHA?
(Hakikisha unaanza tena)
Ulianza kusali vipi mbona umeacha? Ulianza biashara vipi mbona umeishia njiani? Ulianza kusoma kozi ile vipi mbona umekwama? Kwa nini umeacha kufanya mazoezi? Tatizo liko wapi? Hauoni kwamba, huu ni muda sahihi kwako kurejea kwa kishindo.
Katika siasa kuna neno maarufu liitwalo, “bouncebackability” ambalo linaelezea uwezo wa mwanasiasa kuinuka tena. Anaweza kuonekana ameishiwa sera au ameanguka kabisa, na ghafla anasimama na kushinda kwa kishindo. Ufufuko wa Yesu nao ulikuwa na sura hiyo. Kwa siku mbili na zaidi alizokuwa kaburini wengi walidhani ameshindwa kabisa, hata mitume wake walikata tamaa, siku ya tatu alifufuka na kutoka mzima.
Hii ni wiki yetu ya kusimama tena na kurejea katika nafasi zetu kwa kishindo.  Ni wiki ya kumwomba BWANA, afufue kazi zake ndani yetu. Inawezekana wewe ni mhubiri mfu, ni kiongozi mfu, ni mkristo mfu au ni mhandisi mfu. Lakini ni saa yako na yangu kumwambia, “EE BWANA FUFUA KAZI ZAKO NDANI YANGU”
Ni muhimu kumaliza ile kazi tuliyoianza, ni muhimu zaidi kuanza tena kutokea pale tulipoishia. Mwanariadha mmoja wa Tanzania akiwa katika mashindano ya Olimpiki aliendelea kukimbia na kumaliza mbio hizo ndefu licha ya kuumia. Napenda maneno ambayo mtangazaji alimpamba mwanariadha huyo aliyekuwa majeruhi alisema: “Sikutumwa na Nchi yangu kutoka mamilioni ya maili ili kuanza mbio, bali nimetumwa kumaliza mbio.”
Ni kweli kabisa hatukuitwa kuanza bali kumaliza, hatukuitwa kuwa washiriki tu wa maisha bali tumeitwa kuishi kama washindi. Je, Nguvu yetu inatoka wapi? Nguvu yetu si tu ile itokanayo na chakula tunachokula yaani, protini, vitamin, maji na vyakula vya nguvu. Nguvu yetu ni zaidi ya chakula tulacho, nguvu yetu yatoka kwa Bwana Mungu aliyeziumba mbingu na nchi. Kwa Yeye (Yesu Kristo) tunayaweza mambo yote na tunahakika tutamaliza.
Kwa kuwa bado tuko hai basi kila kitu kinawezekana. Napenda mchezo wa mieleka, somo kubwa katika mchezo huu ni kwamba, kuwekwa chini si kushindwa na kupigwa sana si kupoteza mchezo. Mara nyingi katika mchezo huu hata aliyechoka huweza kuibuka mshindi. Ni siku yako leo, toka kaburini, anza tena, maliza kazi yako, Mungu Baba na afufue kazi yake ndani yako katika jina la Yesu Kristo. Amen

Usioneshe kama hutaki kuigwa



USIONESHE KAMA HUTAKI KUIGWA
(Don’t show it if you don’t want to be imitated)
Watu wengi wanaonesha mambo ingawa nia yao ya ndani hawataki watu wengine wayaige mambo hayo. Katika mchezo wa mieleka (WWE) baada  ya kuonesha matangazo ambayo si salama kwa watoto eti wanasema, usijaribu nyumbani, “Don’t try this at home.” Ubongo wa mtu humuamuru kutenda na kutendea kazi kile akionacho.
Wale wa sigara nao baada ya kuandika mandishi makubwa yenye kusisitiza uongo, na kuweka vibwagizo vyenye kuonesha sigara ilivyotamu kama vile, “ni tamu, ni fresh, ni yako” ndipo wanaweka maandishi mengine madogo yasemayo, “uvutaji wa sigara ni hatari kwa maisha yako.” Wanasisitiza uongo kwa herufi kubwa na ukweli kwa herufi ndogo kabisa, mwandishi amefanya tofauti kidogo katika makala hii ili kukemea uvutaji wa sigari ambao kimsingi huleta saratani na magonjwa ya kifua.
Unadhani ni kwa nini makampuni yanawekeza mamilioni ya fedha katika matangazo? Fikiri ni kwa nini wasanii wanaofanya matangazo hayo hulipwa maradufu?  Hivi karibuni hapa Tanzania kampuni moja ya simu imeshindwa kuendelea kumlipa msaanii mmoja aliyedai kuongezewa pesa kwa ajili ya matangazo ya biashara anayoyafanya na kampuni hiyo. Jawabu ni moja makampuni yanaamini watu wakiona wanaamini, na huo ndio ukweli. Kampuni zinapata wateja lukuki kupitia matangazo kwa kuwa kile wateja waonacho huamini na kufanya.
Kila fainali za kombe la dunia zinapoisha vijana huanza tabia na mitindo mpya toka kwa wechezaji. Ukitazama mitindo yao ya kunyoa nywele na mavazi utajifunza kitu. Kuna nguvu katika kile walichokiona. Ukitambua hili utaona umuhimu wa kuonesha yale tu unayotaka yaigwe. Haijialishi ni mavazi, picha, matendo au maneno tusemayo. Ni vema tusema mambo ya kuigwa, tuishi kwa kuigwa na tuvae kwa kuigwa. Don’t show it if you don’t want to be imitated!
Si lazima watu waokolewe kwa kusoma neno na kuhubiriwa, wakati mwingine waokolewe kupitia mienendo yetu. Biblia inasema kuna nyakati unaweza kuoa au kuolewa na mtu asiye amini (mpagani) na kupitia wewe (matendo na maisha yako) atakayo tazama anaweza kuokoka. Kuna nguvu katika kile unachoona. No one in the bible had the bible.
Usitazame kile usichotaka kuwa. Nilimuulize mtoto mmoja anayetazama mieleka kwamba, unampango wa kupigana? Akasema, “Hapana, ila mtu akinichokoza nampiga za hivyo.” Somo hapa ni kwamba, ukitazama sana visivyofaa utatenda isivyofaa pia.
Rai yangu kwako, usione visivyofaa wala usioneshe usichotaka watu waige.

Ni atakayevumilia

 
NI ATAKAYEVUMILIA MPAKA MWISHO
(Endelea kufanya, anzia ulipoishia)
Taasisi ya taarifa za takwimu za kazi nchini Marekani (US Bureau of Labor Statistics Information) inaripoti hivi, “katika nyanja zote za biashara, asilimia arobaini na nne (44%) ya makampuni mapya hutoweka ndani ya miaka miwili na asilimia sitini na sita (66%) hutoweka ndani ya miaka minne ya uhai wa makampuni hayo.”
Mwisho wa siku si yule aliyeanza safari, wala si yule mwenye nguvu, bali ni yule aliyevumilia na kufika kileleni. Biblia haisemi ajuaye sana ataokoka, wala haisemi anayekaa karibu na kanisa ndiye atakaye okoka, badala yake imenena, “atakaye vumilia mpaka mwisho.” Kuanzia katika mafunzo ya kawaida kabisa ya maisha mpaka kwenye neno la Mungu ni mvumilivu ndiye aliyetabiriwa kushinda.
Kwenye ujasiliamali watu huambiwa, “winners never quit, quitters never win.” Uzoefu wa maisha unampa nafasi kubwa mvumilivu kuliko mtu mwenye akili kubwa lakini ana tabia ya kukata tamaa. Kaka mmoja alikuwa na nia ya kuwa daktari (medical doctor) na aliendelea na nia hiyo licha ya vikwazo vingi. Kikwazo kikubwa kilikuwa ni kupata sifuri (division zero) kidato cha sita. Lakini ilikuwa ni habari njema kwangu kusikia kwamba, mwakani atamaliza miaka yake mitano na kupata alichotamani maishani mwake kwa siku nyingi, udaktari. Daraja la mwisho limeshindwa kumkwamisha kwa sababu ya uvumilivu wake.
Rafiki yangu aliandika, “ukichoka usiache, jifunze kupumzika.” UKiwa kwenye uhusiano jifunze kutafuta njia ya kuendelea na si ya kutokea. Ukishindwa kupambana na changamoto katika uhusiano omba kupumzika ili upate muda wa tafakari na maombi. Moja ya changamoto ni tamaa isiyozuilika, ukikaa pembeni utakumbuka kwamba, kuna faida katika kumtii Mungu na raha ya ajabu hutokea ikiwa miili yetu itatumika kama mahekalu ya Mungu. Dakika moja ya tafakari ina maana zaida kuliko masaa mengi ya majibizano.
Mchana mmoja Dominick Mzonya, aliniomba nimsindikize ili akazungumze na kuwatia moyo wanafunzi. Katika moja ya mambo aliyowasisimua kwayo ni kumbukumbu ya tafiti ya makundi matatu ya watu. Makundi hayo matatu yalihusisha watu wenye uwezo wa juu (akili sana), wenye uwezo wa kati (kawaida), na wale wenye uwezo wa chini. Mwisho wa siku katika kutazama maisha ya watu hawa mafanikio yao hayakutokana na akili au uwezo wao bali yalitokana na uvumilivu wao. Wa kundi la mwisho alipovumilia alifanikiwa, wa kundi la kwanza alipovumilia alifanikiwa hatimaye hata wa kundi la katikati alipovumilia bila ya kukata tamaa alifanikiwa. Nguvu haipo katika akili kubwa (High IQ) bali katika kufanyia kazi upendacho, kujitoa, na kudumu bila ya kukata tamaa. Christiano Ronaldo anaonekana kusifiwa sana katika soka moja ya siri ya mafanikio yake ni hii, “Ni wa kwanza kuingia uwanjani kwa mazoezi kabla mchezaji mwingine awaye yote hajaingia na ni wa mwisho kutoka wakati wote wameshamaliza mazoezi.”
Washindi ni wavumilivu, sifa nyingine wanazopewa na watu ni urembo tu. Washindi hufanya mazoezi kila siku kwa uaminifu mkubwa. Mwanafunzi hawezi kufaulu mtihani kwa kusoma siku moja nzima yenye saa 24. Bali mwanafunzi atakayesoma kwa saa moja kila siku ndani ya siku 24 atakuwa bora kupita yule aliyesoma usiku na mchana. Ingawa wote watatumia saa ishirini na nne lakini yule wa kila siku saa moja anaonesha kudumu na kujizatiti katika maandalizi kwa siku ishirini na nne, wakati yule aliyekesha usiku na mchana anaonekana kudumu kwa siku moja tu.
Kila mtu ni mvumilivu lakini si mpaka mwisho, wengi ni mpaka katikati. Kila kitu ni kigumu ila ni lazima tudumu katika kukifanya. Usikate tamaa endelea kuomba kazi, endelea na kipaji chako, wekeza muda mwingi katika kazi zako. Hakuna kuchoka, hakuna kuzimia mpaka tumefika kileleni. Ili timu yetu, “Life minus regret program” iweze kutoa makala hizi kila wiki inatulazimu kusoma kila siku, kusali na kuandika kila wiki. Usisahau tuna majukumu yote kama wewe. Usiache, usirudi nyuma, na Mungu atakusaidia na kukusimamisha. Mapambona yanaendelea, well done is waiting for you.

Kuanzia viongozi .......

KUANZIA VIONGOZI HADI WAFUASI WAO
(Sote tunamuhitaji Yesu)
Sote tunamuhitaji Yesu kuanzia viongozi wa dini kama Papa Francis mpaka Viongozi wa siasa kama Barack Obama sote kwa ujumla tunamuhitaji mwokozi. Hakuna wokovu kwa mtu awaye yote ila kwa Yesu Kristo tu. Nukuu za Alexender The Great ni simulizi zenye mafunzo tele. Kuna nyakati alinukuliwa akisema, “Nitakapokufa nataka jeneza langu libebwe na madaktari bingwa, waweke mikono yao juu ya jeneza langu ili watu wajue wazi kwamba kuna nyakati, hata madaktari wazuri hawataweza kuokoa maisha.”
Madaktari bingwa wanaposhindwa wanamfanya mwanadamu akumbuke kwamba, hakuna uzima kwa mtu awaye yote isipokuwa kwa Yesu Kristo. Bill Graham anasema, “Hata wanasayansi wasiomjua Mungu wala kumkiri wakishaugua saratani (cancer) huanza kukiri na kusema Mungu nisaidie”. Biblia inamfananisha mwandamu na ua ambalo leo lipo na kesho halipo tena. Hakuna la kudumu ndani ya mwanadamu.
Nje ya Yesu Kristo mwanadamu ni kama kivuli punde hayupo tena. Mwandamu anapata uzima ndani ya Kristo na si uzima tu unaokomeshwa na kifo bali uzima ulio juu ya kifo. Kifo hakiwezi kukomesha maisha ya mtu amwaminiye Kristo Yesu. Iko wazi katika 1Kor 15:55-56 Yesu Kristo alishinda kifo kwa ajili yetu hata ikaandikwa, Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako? 56 Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati.
Mauti imeshindwa, mauti imechoka na uzima wa Yesu Kristo umetawala tena. Mauti ilipata nguvu kupitia dhambi naye Yesu Kristo alipokwisha kutusamehe dhambi zetu basi aliivunja ile nguvu ya mauti. Ndio maana watu wengi waliokuwa karibu na kufa alipowaambia wamesamehewa dhambi waliponywa, maana nguvu ya mauti ni dhambi, dhambi ikiondolewa mauti hukosa nguvu. Wamwaminio hawaogopi kifo.
Je, unahisi kufa? Je, unaogopa kifo? Nguvu ya uhai inakuja kupitia msamaha. Wale wenye hakika kwamba, Mungu amewasamehe dhambi zao kamwe hawaogopi kifo. Biblia inasema, “anaraha aliyesamehewa dhambi”, kwa lugha nyingine anafuraha aliyesamehewa dhambi. Waliosamehewa dhambi wamebarikiwa tena biblia inasema wanayo heri. Zaburi 32:1-2
Yesu aliishinda mauti kwa kupitia kuishinda dhambi. Na hakuna mwandamu awaye yote aliyeishinda dhambi na kuiharibu pale msalabani isipokuwa Yesu Kristo peke yake. Madaktari, walimu, viongozi wa siasa, viongozi wa dini hawakuweza na hawataweza ni Yesu peke yake. Mhimili (mzizi) wa kifo ni dhambi, unapotubu unafukuza mauti na hofu zake.
Tumaini la uhai na uzima wetu ni Kristo peke yake. Kama tungelikuwa na uzima Yesu asingelikuja. Kama tungelikuwa wema asingekuja pia. Kwa hiyo amekuja kwa sababu tulikuwa wafu kwa dhambi, watupu kwa uovu wetu na wachafu kwa matendo yetu.
Mwimbaji mmoja anasema, “All I need is you” ni kweli tunamuhitaji Yesu peke yake. Tunamuhitaji kila saa na kila wakati. Ni vema tusogelee mahali anapokaa. Twende kitini pake kwa toba. Imeandikwa, “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. ” Waebrania 4:16
Yesu anapatikana katika kiti cha rehema na biblia inasema, “wakati wa mahitaji”. Je! ni wakati gani huo tunaohitaji neema na rehema? Ni kila saa na kila dakika. Mara kadhaa asubuhi nimekuwa nikipiga magoti na kuomba neema ya siku husika, kwa kuwa najua ninahitaji neema kila siku. Najua namuhitaji Yesu kwa uhai wangu.
Siku ukitenda dhambi unahitaji neema, na siku usipotenda dhambi unahitaji neema pia. Na kama tunahitaji neema kila siku na kila saa basi moja kwa moja tunamuhitaji Yesu kila siku na kila saa. Yeye ndiye mtoaji wa neema hizo. Pata muda wa kuomba sote tunahitaji neema...tukutane wiki ijayo mpendwa. Barikiwa

Rafiki yako ni nani?

RAFIKI YAKO NI NANI?
[Aina ya marafiki ni dalili ya hatima yako] 
Rafiki ni mtu ambaye mna vitu au mwelekeo unaofanana. Rafiki ni Yule ambaye mna mwelekeo wa pamoja katika imani, biashara au kazi. Rafiki ni yule umpendaye na ungependa kuwa na muda mwingi pamoja naye.
Unaweza kufanya urafiki na mtu, na cheo chake, na kitu au vitu. Urafiki na Kaizari ni urafiki na cheo ili upate manufaa  fulani, urafiki wa Yesu na Lazaro ni mfano wa urafiki kati ya watu na upendo kati ya Yuda Iskariote na pesa ni mfano wa watu ambao wako tayari kuwa peke yao ilmradi wawe na pesa.
Kuna nyimbo rafiki tunazozipenda ambazo mara nyingi tunazisikiliza, halikadhalika kuna video rafiki, kipindi cha televisheni rafiki na hata kaseti ya redio rafiki. Tuna kitabu rafiki tena kuna majarida na magazeti rafiki. Ukifanya urafiki na mpumbavu lazima uumie, nyimbo za kipumbavu zinaumiza mioyo, zinaondoa usafi wa moyo kwakuleta mawazo machafu. Biblia inasema, “Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.” Mithali 13:20
Kuna nyimbo za kipumbavu ambazo ukifanyo nazo urafiki lazima uumie, kuna video za kipumbavu, kuna vipindi vya redio vya kipumbavu halikadhalika kuna majarida na vitabu vya kipumbavu. Kuna magazeti ya kipumbavu [udaku] rafiki wa hayo lazima aumie. Moyo wake hautakuwa safi, utawaza uchafu wa picha ya mbele ya magazeti hayo. Msisitizo wangu uko hapa: Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.” Mithali 13:20b
Nimejikataza kuendelea kuitazama vitu kwenye “you tube” kwani picha za matangazo na picha chafu zinazowekwa makusudi zimekuwa kama mtego kwangu. Kuliko kumkosea Mungu kila siku ni bora nisiingie kabisa. Kila mtu ana eneo lake analojaribiwa kwalo, wengine ni urafiki na magazeti, wengine mitandaoni, wengine mavazi na wengine mazungumzo mabaya. Wengine hujaribiwa kwa kutaka kuvutia au kupendwa na watu, hawa huweka picha za mtego wakitegemea aonaye awape, “like” au awakubali.
Rafiki ni yule anayezungumza nawe, magazeti, vitabu, majarida na picha huzungumza nasi. Lengo la mwandishi ni kuona msomajia ua mtazamaji anapata ujumbe kusudiwa. Mara nyingi huwa sitazami wala kusikia nyimbo za kidunia [kipumbavu] lakini huwa inanilazimu nikiwa safarini. Nyimbo hizo hupigwa ndani ya basi na madhara yake ni hasi. Huwa nasafiri nikiwa na vitabu na majarida mazuri ya kusoma lakini bado kwa masaa kumi na nne au kumi ya safari nyimbo za kipumbavu huleta kero na uchafuzi wa moyo. Kama watu watapata ajali huku wakitazama nyimbo chafu basi mioyo yao itakuwa katika hali mbaya.
Tunaweza kujaribiwa kwa kuwa na makundi yenye mazungumzo mabaya lakini kwa kuwa na tabia ya kuchagua vitu vinachochea tamaa mbaya. Ni muda mzuri leo wa kuamua kuacha kabisa urafiki na kipindi kichafu cha redio au televisheni, ni muda mzuri wa kuvunja urafiki mbaya. Rafiki mpumbavu atafanya uangamie, napenda tafsiri hii: “The companion of fools will suffer harm
Mfano mzuri wa madhara yanayompata rafiki wa mpumbavu ni yale ya nchi ya Japani iliyoyapata kutoka Marekani kufuatia urafiki wao na Hiltrer wa Ujerumani. Japani walifanya urafiki na Ujerumani kwa kusaini mkataba wa ulinzi na usalama wa mwaka 1940 matokeo yake mbeleni walivamia kisiwa kimoja nchini marekani na kuambulia kupigwa mabomu ambayo mpaka sasa wanayaonja madhara yake. Yote hayo ni kwa sababu ya rafiki mpumbavu. Nakushauri achana naye na kesho yako itakuwa njema.