MWAKA 2018
UWE MWAKA WA KUJIHATARISHA ZAIDI ILI KUPATA MAFANIKIO
Wengi
wanashindwa kwa sababu hawafanyi kitu mpaka waone ni salama kabisa, hawaanzi
mradi mpaka waone ni faida tupu, tabia hii imezuia mafanikio ya wengi. Mwaka
jana niliingia kwenye biashara ya mtandaoni (online business) na kupata hasara
ya milioni nne, mwaka huo huo bila ya kukata tamaa nikaingia katika biashara
nyingine na kupata faida ya milioni nne! Ukipata hasara katika biashara moja
haina maana kwamba na biashara nyingine utapata hasara pia.
Kitabu
cha Mhubiri kinasema, “Mwenye
kuuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna” Mhubiri
11:4. Ukichunguza chunguza sana huji kufanikiwa katika uwekezaji na maendeleo.
Kuna wakulima ambao wakijua ni msimu wa kilimo wanalima na hawa ndio
hufanikiwa. Na kuna wale ambao hata kama ni msimu wa kilimo wao huchunguza
chunguza mawingu na mwishowe wanashindwa kupanda mbegu zao.
Tabia
ya kujihatarisha ni njema na imewasaidia wengi. Fanya kitu kwa wakati uchunguzi
utakuja baadaye! Amesema Ratan Naval Tata mwanzilishi wa kampuni ya kutengeneza
mitambo na magari aina ya TATA, “I don’t believe in taking right decision, I
take decisions and then make them right” kwa tafsiri yangu amesema, “Siamini
katika kuchukua maamuzi sahihi, bali nafanya maamuzi na baadaye nayafanya kuwa
maamuzi sahihi”
Kujihatarisha
inaweza ikawa ni kuachana na uhusiano mbaya, inaweza ikawa ni kuhama mji mmoja
kwenda mwingine, inaweza ikawa ni kufunga na kuomba licha ya dalili za vidonda
vya tumbo. Inawezekana ikawa ni kurejea nyumbani usiku kila siku kwa sababu za
msingi, au ikawa ni kuamka mapema. Pia kujihatarisha inaweza ikawa ni kufanya
kinyume na walio wengi, kwenda katika upekee wako au katika njia ya ubunifu
ambayo wengi hawapiti. Vyovyote vile kama hatukujihatarisha kabisa hatutapata
badiliko lolote.
Matajiri
wengi akiwemo Bill Gates na Oprah Winfrey wamekuwa na sifa ya kukatiza masomo
au kuacha kabisa ili kwenda kutumikia ndoto zao. Hii nayo ni kujihatarisha,
kuacha kile ambacho dunia inaamini ni ufunguo wa maisha ilikuwa ni sawa na
kuyafunga maisha yao. Lakini pamoja na hatari ya kuacha shule bado wamefanikiwa
na wamewaajiri waliohudhuria vizuri shuleni. Kama kunamafanikio nje ya elimu
basi ni muhimu tukajua elimu si ufunguo pekee. Maisha ni zaidi ya vidato!
Maskini
wote wanachukia vurugu na hatari, hawapendi biashara nje ya kiyoyozi hata mara
moja hawajitumi kutembeza bidhaa. Wanapenda usalama, kulala mapema na kuchelewa
kuamka. Hawapendi kusafiri juu ya magari aina ya Fuso yanayokwenda minadani,
wanapenda usafiri tulivu na salama, hawataki usumbufu wa wachuuzi wadogo wadogo
wenye kutembeza biashara. Hawawazi kuajiri, wao wanataka kuajiriwa tu!
Nakumbuka
mwaka 2015 baada ya sala na maombi niliamua kuondoka nyumbani umbali wa mikoa mitano na kuhamia jijini Dar-es-salaam
na ndani ya miezi miwili nilipata nilichokuwa nahitaji kwa muda ule. Si kila
mtu atafanikiwa mjini wengine wanahitaji kurudi vijijini na wengine kwenda
mjini ili kukutana na mafanikio yao. Ili kukutana na ndoto zao wengine
itawalazimu kutoka Ulaya na kurejea katika nchi zao.
Unapopanga
mipango yako mipya weka na mipango yenye kukuhatarisha (bila kuvunja sheria) na ndiyo mipango ya mafanikio.
Take risks,
if possible take calculated risk……
2018
MWAKA WA MASAHIHISHO
Kama wanadamu tunakosea na kila mwaka
unatupa fursa ya kufanya mambo mawili mosi, unatupa fursa ya kufanya mambo
mazuri na sahihi; pili, unatupa fursa ya kukosea. Amesema mzaburi, “BWANA kama
wewe ungehesabu maovu yetu nani angesimama?” Kwa siku zaidi ya mia tatu za
mwaka 2017 yako mengi yasiofaa ambayo tumeyatenda na hayapaswi kuendelea
kufanyika; yako pia ya kufaa ambayo yanatakiwa kuendelezwa katika mwaka 2018. Yako
pia mazuri ambayo tulitakiwa kufanya na hatukuyafanya!
Kwa kuwa katika mwaka 2017 kulikuwa na
makosa na mapungufu ambayo kwa hekima ya kawaida huwa tunayachukua kama shule
kwa ajili ya mwaka 2018 basi mapungufu hayo yasituumize. Hatutegemei katika
mwaka 2018 kuendelea na makosa ya 2017 ambayo tumesha hitimu shule yake.
Tunaweza kutaka mabadiliko katika mwaka
2018 na tusiweze, pengine nguvu zetu ni kidogo na hutuwezi kugeuka, lakini uko
msalaba na iko damu ya Yesu! Nguvu ile iliyohuisha mwili wake kaburini naye
akafufuka mzima, yaweza kutuhuisha roho zetu na dhambi na kutufanya kuwa watu
bora kabisa katika mwaka 2018. Najua nguvu zetu ni kidogo lakini panapo msalaba
pana nguvu kubwa ya mageuzi.
Mamilioni ya watu wamekuwa wakipinduliwa
kwa nguvu ya msalaba toka utumwa wa dhambi mpaka utakatifu. Nguvu hii ni kwa
ajili yetu katika mwaka 2018. Kama tulikosea 2017 imetosha sasa, sasa
tumejifunza, sasa ni wakati wa kugeuka. Moja na malengo yako katika mwaka 2018
ni muhimu kuwa kufanya yale uliyotakiwa kuyafanya katika mwaka 2017 na
hukufanya. Hii pia ni lengo la kizazi cha sasa yaani, kufanya yale ambayo
vizazi vilivyopita vilitakiwa kufanya na havikufanya. Mwalimu Jim Rohn amesema
jambo la kufanana na somo hili, “Don’t
let learning from your own experiences take too long. If you have been doing it
wrong for the last ten years, I would suggest that’s long enough”
Masahihisho ni jambo jema kabla ya hukumu,
masahihisho yanatupa nafasi ya kujitathmini, kujikosoa na kuanza upya, kamwe
yasitazamwe kama hukumu. Katika kitabu nikipendacho cha, “The Virgin Way” kilichoandikwa na Richard Branson imesisitizwa kama
unafanya makosa na uyafanye haraka. Kipindi chako cha kukosea na kujifunza
kutokana na makosa kisiwe kipindi kirefu mno. Hii imepelekea kukusihi, mwaka
2018 iwe muda wako wa kuanza upya. If
you’re doing a mistake do it very quickly in these few days before 2018.
Tufikapo 2018
tuwe wapya tayari kwa ushindi.
Barikiwa!
Inachukua
Muda...
Tunaishi katika ulimwengu ambao karibu
kila eneo watu hutaka huduma kwa haraka; usafiri wa haraka (mwendokasi),
chakula cha haraka (fast food), mikopo ya haraka, huduma za kifedha na afya kwa
haraka (fast track) n.k ! Hakuna anayetaka kukaa muda mrefu kwenye foleni kusubiria
huduma. Maendeleo ya sayansi na tekinolojia yamerahisisha upatikana wa huduma
nyingi katika jamii na kwa haraka zaidi wakati huu, kuliko miaka kumi iliyopita.
Pamoja na mchango mkubwa wa sayansi na
tekinolojia katika upatikanaji wa huduma, watu wengi wamesahau baadhi ya kanuni
muhimu za mafanikio ya kweli; katika ulimwengu huu wa haraka haraka, jamii
imesahau kuwa mafanikio ya kudumu huchukua muda kuyajenga. Kanuni hii ni rahisi
sana kusahaulika katika ulimwengu wa haraka.
Ya kwamba mahusiano mazuri yanachukua muda kuyajenga, familia nzuri
inachukua muda kuijenga, mafanikio ya kifedha, huduma, taaluma pamoja na 'career'
haya yote huchukua muda kuyajenga.
Ni mwanafunzi anayeamini katika ulimwengu
wa haraka kwenye taalumu hufanya bidii aweze kuiba au kuibia kwenye mtihani, ni
kijana anayeamini tu katika ulimwengu wa haraka hushinda kijiweni "akibeti"
ili kufikia mafanikio ya kifedha. Ndio maana ni rahisi kwa mtu kwenda kucheza "desi"
ili apokee mara asilimia mia tatu (300%) kuliko kuwekeza kwenye ufugaji wa kuku,
kwa sababu anaona hatapata hiyo asilimia mia tatu haraka. Hutaka kupata kwa
haraka bila kufanyia kazi. Nitajie tajiri aliyeko kwenye orodha ya matajiri kwa
sababu alishida bahati nasibu au desi; go back to Work!!
Watu ambao hawajui kuwa mahusiano bora na
imara huchukua muda kuyajenga wakitofautiana kidogo huvunja uhusiano huo na
kama ni wana ndoa hutishia kutengana kabisa. Mzazi ambaye anayeamini katika
ulimwengu wa haraka katika malezi, hana muda wa kukaa na watoto kuwafundisha na kufuatilia malezi yao
kwa karibu; wakishapotea na kuharibika kimwenendo hukimbilia kwa watumishi
wamuombee ili wapone na kurudi kwenye njia sahihi kwa haraka, amesahau alikuwa
na nafasi katika kujenga mwenendo bora kabla.
Anayejenga nyumba juu ya mwamba hutumia muda
kuijenga, na kwa sababu hiyo nyumba hiyo itakuwa imara kuliko anayejenga juu ya
mchanga. Kuna baadhi ya maeneo ulimwengu
wa haraka hauleti matokeo bora, bali kanuni ya muda! Mwenyehekima mmoja amewahi kusema
"usikimbie mahali panapokutaka kutembea; na usitembee mahali panapokutaka
kukimbia "
Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka;
Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa-Mithali 13 :11
There's a place for you at
the top
MTU JASIRI
Katika ulimwengu wa sasa majasiri wengi
hawajulikani. Dunia ya leo imewatukuza wasemaji ikaacha wakimya, imemdharau mtu
mpole ikampa heshima mtu mkali. Katika vikao wasikilizaji wazuri hawatambuliwi
kama majasiri wa kusema. Kusikiliza si jambo jepesi, hakuna mtu mgumu
kumsikiliza kama mtu mkorofi na mtu asiyejua.
Si wengi wanauzoefu na uwezo wa
kusikiliza kwa makini, wengi hupenda kusikilizwa si kusikiliza. Huwezi
kusikiliza na huku unatazama televisheni au unasikiliza redio. Ni rahisi
kuukusanya mwili lakini si akili ya usikivu. Huwezi kusikiliza ikiwa unataka
kusema, unaweza kusikiliza ikiwa unataka kusikiliza. Alisema Winston Churchil,
“Courage is not only what it takes to
stand up and talk but courage is also what it takes to sit down and listen”
kwa tafsiri “Inamhitaji mtu jasiri kusimama na kuzungumza, lakini inamhitaji
mtu jasiri pia kukaa kimya na kusikiliza”.
Amenukuliwa mzee Kinana Katibu Mkuu CCM
akisema, “kiongozi lazima asikilize wananchi”. Kiongozi si lazima awe kwenye kampuni, kwenye
taasisi ya umma au kwenye siasa, badala yake anaweza akawa kwenye familia baba
wa familia, mama wa familia, kaka wa familia au dada wa familia. Siku chache katika nafasi ya uongozi jambo
kubwa nililojifunza ni kwamba, uongozi ni kusikiliza, It’s all about listening!
Ni raha kusikiliza, msikivu anaraha kwa
kuwa anauelewa mpana. Je, ungependa kuitwa mwongeaji sana au msikivu sana. Je,
ungependa mtu akitoka nyumbani kwako aseme hajawahi ona msemaji kama wewe au
aseme hajawahi kukutana na mtu msikivu kama wewe. Si vema mtu akushangae kwa kusema, “What a talker”
Ni mtu jasiri peke yake anaweza
kuwasikiliza waliotengwa, waliosetwa na wasio stahili katika jamii. Si rahisi
kuwasikiliza wahalifu, mtu jasiri pekee anaweza kufanya hivyo.
Kwa kiongozi mpya wa nafasi na ngazi yoyote
nasisitiza neno moja, sikiliza, sikiliza, sikiliza.
Tukutane kileleni wasikivu
wanapopatikana.
UMEITWA KUONGOZA
Mtu hafanyiki kiongozi kwa cheo au nafasi
aliyonayo katika Nyanja za siasa, taasisi, kanisa n.k; bali ni kusudi (purpose) linalozaa maono (vision) ndani yake. Sifa kuu ya kiongozi
ni kuwa na maono chanya kwa mustakabali wa anachokiongoza. Mahali ambapo hakuna
maono hakuwezi kuwa na uongozi, kunaweza kuwa na cheo lakini hakuna uongozi!.
Maono ndio hufanya kiongozi awe kiongozi.
Siku zote watu hawafuati mtu, wanafuata maono yake. Mahali ambapo nguvu hutumika
ili kufanya watu wafuate (follow) ni
kwa sababu hakuna maono yanayoshawishi watu kufuata kwa utashi na hiari yao.
Ikiwa kila mtu ameumbwa kwa kusudi maalumu,
basi ni ukweli uliowazi kuwa kila mtu ameitwa kuongoza katika eneo la kusudi
lake; kumbuka maono ndio yanayotengeneza kiongozi na sio kinyume chake, na
maono ni picha ya kusudi ndani ya mtu. Maono ndio yaliyotengeneza mtu anaitwa mama
Theresa, Nelson Mandela, J. K. Nyerere, Martin Luther King Jr n.k. Maono ndio
yanayotengeneza makampuni, mashirika, taasisi, ajira kwa watu, biashara, miradi
(projects) na sio kinyume chake.
Ninaposema kila mtu ameitwa kuongoza sina
maana kila mtu ameitwa kuwa mwanasiasa (wapo waliokusudiwa hapa pia); na wala
si swala la kuwa na cheo au kutokuwa nacho! Bali kwa kuwa umeumbwa kwa kusudi fulani,
inatosha kujua mahali uongozi wako unahitajika. Uongozi wako unaweza hitajika
kwenye eneo la biashara, eneo la tekinolojia, eneo la sanaa na michezo, eneo la
siasa, jamii (social leader), afya,
uchumi au madhabahu! (Your area of
gifting and passions)
Kwanini nasema umeitwa kuongoza? Kwa
sababu maono hutolewa kwa mtu mmoja kwanza kabla hayajapata wafuasi wengi; Na
pia kila mtu ana eneo au nafasi yake kwa kadri ya kusudi la kuumbwa kwako sawasawa
na maono aliyonayo; Ni kwa sababu ulichopewa si kwa ajili yako, ni kwa ajili ya
wengine (japo na wewe utanufaika), mfano.
Mwalimu hawi mwalimu kwa ajili yake, japo hupokea malipo ya kazi hio! Kumbuka, hakuna mti unakula matunda yake wenyewe!!
There's a place for you at the top