Baada ya kulitambua kusudi la kuumbwa kwako



BAADA YA KULITAMBUA KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO
Ukishafikia hatua ya kutambua kusudi la Mungu juu ya maisha yako hatua zifuatazo ni muhimu sana:
  1. Liandike
Ni muhimu sana kila mtu kuandika kusudi lake au maono yake katika aya yenye sentensi chache iwezekanavyo. Hii itakusaidia kulikumbuka daima kila unapoona sentensi hiyo na kukupa nguvu ya kuiendea hadi mwisho [Habakuki2:2—3].
“Ni vizuri kuibandika karatasi hiyo inayoelezea picha ya maono ya maisha yako ya baadae [kwa ufupi], chumbani au mahali popote pa wazi ili kila uisomapo uweze kukumbusha na kukuhamasisha”
Nimewahi kusoma mwandishi mmoja ambaye yeye anashauri sentensi  hizo zisizidi tatu, lakini kwa maoni yangu si mbaya hata zikifika tano. Tazama kusudi la Yohana mbatizaji lilivyo katika sentensi chache.Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeyeYohana 1:6
Ni vizuri kuibandika karatasi hiyo inayoelezea picha ya maono ya maisha yako ya baadae [kwa ufupi], chumbani au mahali popote pa wazi ili kila uisomapo uweze kukumbusha na kukuhamasisha. Kwa mfano zifuatazo ni sentensi ambazo nimeandika ili kuelezea kusudi la kuumbwa kwa watu kadhaa ukianza na mimi:
1.      “My purpose is to you use all I have, to give myself into the preaching of the gospel and inspire others to live for Christ” Alphonce Luhamba’s vision (purpose) statement
2.     “To uplift humanity consciousness through business”
3.     “To inspire and empower people to live their highest vision in context of love and joy”
4.     “To create and inspire one million millionaires who each will donate one million dollar to his or her church charity”
Ni vema kurahisisha kwa kuandika au kuchora alama zenye kuonesha picha ya kusudi la kuumbwa kwako. Mchoro huo au maneno hayo ni lazima yawe yanakuvutia, yaweze kukuhamasisha na kukupa changamoto ya kuyafanyia kazi katika kutimiza kusudi hilo.  [Your Vision or purpose paragraph must challenge your comfort zone.]
Ni vizuri kulisoma kusudi lako kila siku, ni vema kuliacha liimbe kichwani mwako kila dakika. Kama Ilivyokuwa kwa Yohana mbatizaji wewe pia umetumwa na Mungu, na umetoka kwa Mungu. Haupo duniani kitalii, upo kikazi. Muda wote tuwapo duniani tupo safarini kwa kazi maalumu. Badala ya Yohana, waweza kuweka jina lako. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake.....Yohana 1:6
  1. Achana na utafiti.
Ukishajua kusudi au maono yako haunabudi kuacha kujiuliza uliza maswali mengi. Hakuna haja ya kuogopa. Ni muhimu kudumu katika Neno la Mungu ambalo ndio chakula muhimu kwa kila mbeba maono na makusudi ya Mungu. Kusudi lako litaendana na Neno la Mungu hivyo usiache kulisoma.
“Kuachana na utafiti usio na tija kutakujengea ujasiri na uhakika wa kupata ushindi; na matokeo yake Imani yako kwa Mungu juu ya maono hayo itaongezeka”
Katika kusudi ushindi lazima. Kuachana na utafiti usio na tija kutakujengea ujasiri na uhakika wa kupata ushindi; na matokeo yake Imani yako kwa Mungu juu ya maono hayo itaongezeka. Achana na maswali ya nitaweza au sitaweza, Mungu aliyekuita atakuwezesha. Tunapokuwa katika kusudi la Mungu tuna uhakika na ushindi wala hatubahatishi.
Baada ya kuachana na maswali, unapaswa kubaki na maneno machache tu ya ushindi. “Nitaweza na nitafanya na nitakuwa vile ambavyo Mungu anataka niwe. Unapaswa kusema kama Daudi, Sitakufa mimi bali nitaishi, ili kufanya kazi niliyoitiwa na BWANA.
  1. Litende na kuimaliza kazi kwa gharama yoyote ile.
Kwa sababu ya hofu ya kulipa gharama mara kadhaa utajikuta katika nafasi ambayo ni rahisi kufanya kila kitu isipokuwa kusudi la kuumbwa kwako, hata hivyo unapaswa kulichagua kusudi lako hata kwa mateso. “Chakula change ndicho hiki niyatende mapenzi yake yeye aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake…”Yohana4:34. Jim Rohn anaandika, “Kama una nia ya kutaka kufanya jambo, utatafuta njia ili kulifanya; kama huna nia, utatafuta visingizio kwanini hauwezi kufanya” (Tafasiri isiyo rasmi)
Gharama inaweza kubwa lakini ni muhimu kuhakikisha kwamba kusudi linatendeka, maana gharama huakisi uzuri wa taji yako. Gharama inawezakuwa ya juu (steeper) kama vile: Kuacha kazi fulani, kurudi tena shule au kutengwa, kujikatalia mambo ya kidunia, kuonekana mshamba au kukosa muda wa kupumzika. Kusudi la Yesu lilimnyima hata muda wa kulaza ubavu wake. Ili kufanikisha jambo lenye kuleta maana duniani mwenye hekima mmoja anaandika, “Hakikisha kazi inafanyika kwa gharama yoyote”.
  1. Weka na kupanga  mipango
Maono au mipango ni ulinzi wako. Hatuhitaji “body guard” kama Rais, tunahitaji maono ili kutuokoka katika maangamizi. Mipango mizuri ya baadaye ni ulinzi tosha, itakuzuia na itakuruhusu pia. Pasipo maono na mipango dhabiti, watu huacha kujizuia na hivyo huangamia.
Mipango ni njia ya kuiendee hatima yako. Mipango ni hatua kuelekea katika hatima iliyowekwa mbele yako kwa sura ya maono [Mithali 16:9]. Ni vizuri mipango yako ikazingatia muda. Usikubali  kubahatisha au kupangiwa na mtu. Ni vizuri ukaweka mipango dhabiti ili kutekeleza kusudi la Mungu katika maisha yako. Mipango inakufanya uone mbele, inakusaidia usirejee nyuma. Mipango inakupatia nafasi ya kuishi maisha ulikwisha yafikiri. Pasipo mipango au maono watu hurejea nyuma na hivyo huangamia.
“Watu wanaopenda kufuata mkumbo hawapendi kupanga mipango yao wenyewe, wanaridhika kuwa mashabiki wa watu fulani au wa kikundi fulani”
Ukiwaruhusu watu wapange kwa ajili yako watakupangia kijisehemu kidogo; tofauti na wito au uwezo ambao Mungu ameweka ndani.  Mipango ni wajibu wako binafsi usioweza kukaimishwa [delegate] kwa mtu yeyote. Watu wanaopenda kufuata mkumbo hawapendi kupanga mipango yao wenyewe, wanaridhika kuwa mashabiki wa watu fulani au wa kikundi fulani. Usipopanga mipango yako, utaangukia katika mipango ya mtu mwingine; hii haikupi uhakika wa kufikia kilele cha mafanikio yako.  
“Utahitaji kuchochea kipawa chako; na hapa ni muhimu utafute maarifa na ujuzi sahihi ili kukuwezesha kutumia vyema kipawa chako”
  1. Tafuta maarifa
Wakati mwingine kusudi lako linaweza kukuhitaji utafute maarifa na weledi wa juu ili kulitekeleza kwa ufanisi.  Utahitaji kutoka kwenye “kipawa [gift/talent]” mpaka kwenye “ujuzi [Skills]”. Utahitaji kuchochea kipawa chako; na hapa ni muhimu utafute maarifa na ujuzi sahihi ili kukuwezesha kutumia vyema kipawa chako. Waweza kwenda shule ya muziki, au utahitaji kwenda shule ya sheria, au kurudi tena shule hata kama mwanzoni uliishia njiani, waweza kwenda shule ya Biblia ikibidi, waweza kuwa mfuasi wa mtu mwaminifu aliyefanikiwa katika eneo unalotaka kufanikiwa ili kujifunza kutoka kwake [mentorship/coaching].
Watu wengi wenye vipawa hufanana lakini juhudi, ujuzi na maarifa hufanya watofautiane; inawezekana wote ni waimbaji, lakini mmoja anaimba kwa ujuzi [skills] na mwingine hana ujuzi huo. Marafiki sahihi, usomaji wa vitabu na utazamaji wa vipindi vinavyolisha maono yako ni mambo yenye kukupatia msaada na kulifanya kusudi lako litendeke kirahisi, kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa.

Umuhimu wa kutambua kusudi - II


UMUHIMU WA KUTAMBUA KUSUDI-II
Tofauti kati ya Kusudi (Purpose) na Maono (Vision)

Kusudi maana yake ni sababu iliyofanya au inayofanya kilichopo kiwepo au kitengenezwe jinsi kilivyo (design) ili kutimiza kazi maalumu; katika kufikia malengo yaliyokuwa yamekusudiwa awali kabla ya kitu hicho kuwepo au kutengenezwa.

ULIMWENGU MKAMILIFU


ULIMWENGU MKAMILIFU
“Imagine a world without a loser, a world without a purposeless person”
Dunia kamilifu inategemea sana ukamilifu wa mwanadamu. Kwa asili mwanadamu ni mkamilifu na mwenyehaki. Hebu jaribu kufikiri kwamba ulimwengu ungekuwa mkamilifu ungependeza namna gani; hata hivyo ukamilifu wake unategemea wanadamu. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”Mathayo 5:48

Umuhimu wa kutambua kusudi - I

UMUHIMU WA KUTAMBUA KUSUDI - I
Umezaliwa ili kufanikisha jambo mahususi katika maisha yako. Kuzaliwa kwako ni jibu la Mungu juu ya uhitaji ulipo katika kizazi chako. Kazi kubwa ya kwanza ulionayo ni kutambua jambo hilo ndipo uweze kuishi kwa ufanisi. Tafiti mbali mbali zinaonesha, watu waliofanya mambo makuu duniani, ndani ya mioyo yao walishawishika na ukweli huu, ya kwamba wameumbwa kwa ajili ya kufanikisha jambo fulani mahususi. Jambo hilo ndilo huitwa kusudi la kuzaliwa kwako.

Kusudi maana yake ni sababu iliyofanya au inayofanya kilichopo kiwepo au kitengenezwe jinsi kilivyo ili kutimiza kazi maalumu katika kufikia malengo yaliyokuwa yamekusudiwa awali kabla ya kitu hicho kuwepo au kutengenezwa.  Kutambua sababu ya kuwepo kwako ni jambo la msingi kuliko yote unayoweza kufanya.

Ile kwamba kila kitu kimeumbwa kwa kusudi maalumu haina maana kwamba kila kitu kinaishi kulingana na kusudi hilo la kuwepo kwake. Kumbuka jambo hili: Tumepewa muda wa kuishi; hatujapewa muda wa majaribio ya kuishi. Ni hasara kwa mtu kukutwa na mauti wakati bado yupo kwenye majaribio ya kuishi.

Kwanini kutambua kusudi la Mungu juu ya maisha yako ni jambo muhimu:

  1. Kusudi ndilo linalokupa kujua sababu ya kuumbwa kwako. Ni hasara kwa mtu kufanya kila kitu katika maisha yake isipokuwa kufanya alichokusudiwa kufanya.
  2. Kusudi ndio chanzo cha utoshelevu wa kweli katika maisha ya mtu (sense of fulfillment).
  3. Kusudi hutupa msukumo na ujasiri wa kusonga mbele katika maisha yetu ya kila siku bila ya kukwamisha na changamoto zinazojitokeza.
  4. Kusudi linakupa uhakika juu ya maisha yako ya kesho leo. Na hivyo hukupa msingi imara ya Imani isiyoweza kuyumbishwa na kitu chochote. Kukupa uhakika juu ya mambo yatarajiwayo. [Habakuki 2:3-4]
  5. Mungu hufanya kazi kwa kuliangalia/kuzingatia kusudi lake. [Waefeso 1:11].
  6. Mungu hufanya kazi kwa kuhakikisha kusudi lake linatimia (He is committed to His purposes) Isaya 14:24
  7. Unapotambua kusudi, hofu hutoweka. Unapotambua ulipokusudiwa kwenda inakupa kujua kuwa ulipo sasa ni kwa kitambo tu. When you know where you are going, where you are becomes an adventure.  [Zaburi 23:3-5]

Hizo ni baadhi ya sababu kwanini kutambua kusudi la Mungu katika maisha yetu ni muhimu. Ikiwa Mungu hufanya kazi kwa kuhakikisha kusudi lake linatimia, hii inatupa uhakika na ujasiri wa kutembea katika mafanikio ya kweli siku zote  kwa kuwa Mungu anakuwa upande wetu ili kutufanikisha.

Kabla ya Mungu kukufunulia kusudi lake kwa maisha yako, Hujifunua kwako kwanzo; Hukukutanisha na U-Mungu wake. Ndio maana kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako ni Muhimu, si tu kwa ajili ya kwenda Mbinguni lakini pia unapata fursa ya kutambua kusudi la Mungu kwako na kukuwezesha kuishi maisha yenye ufanisi na mafanikio ya kweli.
See you at the top

Acha Kujipima Kimwili


ACHA KUJIPIMA KIMWILI

Unaweza kuwa na urafiki hai na Yesu na bado ukawa masikini wa mali na fedha wala si ajabu, unaweza kuugua na bado ukawa na urafiki mzuri na Yesu. Lazaro alikuwa masikini na alikuwa mgonjwa lakini bado urafiki wake na Yesu ulikuwa hai. Kamwe vitu na hali ya afya au fedha si jawabu la mwisho la kuonyesha uhusiano wa mtu na Mungu, Yohana 11:2. Pastor Chris Oyakhilome anaandika katika utenzi wake, “jambo muhimu kabisa katika maisha haya si umiliki wa mali, bali ni kugundua kusudi la Mungu na kulitimiza”.  Maisha hayahusu milki za mali, unaweza ukawa unamiliki kila kitu hapa duniani na bado isikufaidie chochote. Yesu Alishasema, “…maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyonavyo.” Luka 12:15
Unapompokea Yesu unapokea kwanza mambo ya msingi na ya lazima kama vile: uzima wa milele, Roho wake mwema, imani ya kweli, uponyaji na unafanyika makao yake. Haupokei aina mbalimbali za magari Toyota Carina, Vos wagon wala Isuzu, haya hata yakija huitwa ziada, cha msingi uzima wa milele. Vitu ni vitu na mtu ni mtu. Kamwe uzima wa mtu haumo katika mali au alama za juu katika tasnia fulani, bali umo ndani ya Kristo Yesu. Hata upewe ulimwengu mzima ni bure kabisa kama hautaweza kudumu katika kusudi la Mungu. Nafsi yako haiwezi kununuliwa na jumla ya utajiri wote wa dunia hii. “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Marko 8:36

Shabaha ya shetani ni kuwaona watu wakimlaani na kumlaumu Mungu wao, kwani adui anajua wazi Mungu hapendi kulaumiwa. Mafanikio ya kiroho hayapimwi kwa alama za juu darasani, nyumba gari au fedha nyingi. Baraka ni muhimu ila si kipimo sahihi. Kujipima kimwili ni sababu kubwa inayofanya watu wa kiroho wamlaumu Mungu na kujuta.

Ukikwepa kusudi la Mungu baadaye utajiona huna faida, hautaacha kulaumu kwa kuwa mazingira yatakuwa kinyume na wewe. Utaona umekuja duniani kama mtalii tu, wala hakuna ulichokamilisha. Mtu hana faida nje ya wito na kusudi aliloitiwa na Mungu. Maneno ya Solomoni kwamba, “mtu ana faida gani ya kazi yake…” yanafanana na yale ya nabii Malaki, “Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida;” haya ni maneno ya watu waliosahau kusudi la Mungu, na kujikuta wakipenda dini, mali, wake zao, serikali, vitu, marafiki au watoto kuliko kusudi la Mungu.

Nilijifunza mahali fulani kwamba watu wa ki-dunia huutafuta mkono wa Mungu (vitu) lakini sisi tunautafuta uso wa Mungu (uwepo). Ukiwa mtu wa kiroho jipime kiroho. Usijipime kwa kuangalia jinsi waovu au wasio mtii Mungu wanavyofanikiwa. Cha msingi angalie kama unalitendea kazi kusudi la Mungu kukuumba wewe.

Ukipenda kujilinganisha na watu na vitu matokeo utakayopata ni kuona utumishi wako hauna faida. Utaona kumtumikia Mungu hakuna faida, na matokeo yake ni kuleta laana katika maisha yako. Mungu anajua kila amtumikiaye anapata faida ndio maana hapendi watu wake waseme hakuna faida katika utumishi.

"Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani? Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi? Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.” Malaki 3:13-18

Hatupaswi kujipima kimwili bali na tujipime kiroho kwa kuzingatia kusudi la kuumbwa kwetu. Unaweza ukawa na fedha nyingi, cheo kikubwa, mavazi mazuri na mke mzuri, lakini kama hujatumikia kusudi la Mungu katika hayo basi ulichofanya ni bure tena ni sawa na kufukuza upepo. "Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua?” Mhubiri 1:2-3